• HABARI MPYA

    Saturday, June 01, 2019

    NI ESPERANCE BINGWA TENA AFRIKA, YAIPIGA WYDAD 1-0 TUNISIA

    WENYEJI Esperance wamefanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco bao pekee la mshambuliaji Mualgeria Mohamed Youcef Belaili dakika ya 41 akimaliia pasi ya kiungo Mtunisia, mzaliwa wa England Ayman Ben Mohamed Uwanja wa OlImpiki mjini Rades, Tunisia.
    Lakini mchezo huo haukumalizika baada ya Wydad kugomea dakika ya 60 na ushei wakishinikiza Teknolojia ya Mstari wa Goli itumike kutazama bao lao lililokataliwa ambalo lilifungwa na Walid El Karti kwa kichwa.
    Wydad walikataa kuendelea na mchezo dakika ya 60 hadi VAR itumike kufanya maamuzi juu ya bao lao, lakini ikaelezwa kwamba teknolojia hiyo haikuwepo uwanjani jana na refa Papa Bakary Gassama baada ya majadiliano huku timu ya Casablanca ikiendeleza mgomo akamaliza mchezo kabla ya Esperance kupewa Kombe.
    Kwa matokeo hayo, Esperance inayofundishwa na kocha Mtunisia, Moine Chaabani inabeba taji hilo kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Prince Moulay Abdallah mjini Rabat.
    Siku hiyo, wageni Esperance wakitangulia kwa bao la dakika ya 44 la Fousseny Coulibaly kabla ya Cheick Comara kuisawazishia Wydad dakika ya 79, wafungaji wote raia wa Ivory Coast.

    Wachezai wawili tu walionyeshwa kadi za njano usiku wa kuamkia leo, kiungo Muivory Coast, Coulibaly dakika ya 10 na Belaili dakika ya 42.
    Hilo linakuwa taji la pili mfululizo kwa Esperance na la nne jumla kihistoria, baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 1994, 2011 na 2018 ikiungana na timu kama Al Ahly ya Misri, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Enyimba ya Nigeria zilizofanikiwa kutetea taji hilo.
    Kikosi cha Esperance kilikuwa; Rami Jeridi, Mohamed Ali Yakoubi, Anice Badri, Mohamed Youcef Belaili/ Hamdou Elhouni dk61, Taha Yassine Khnissi, Khalil Chamam, Fousseny Coulibaly, Saad Beguir, Ayman Ben Mohamed, Sameh Derbali na Franck Kom.
    Wydad Athletic Club; Ahmed Reda Tagnaouti, Salaheddine Saidi, Ismail El Haddad, Aouk Badi, Walid El Karti, Aymane El Hassouni, Ayoub El Amloud, Yahya Jabrane, Abdelatif Noussir, Comara Cheick Ibrahim na Mohammed Nahiri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI ESPERANCE BINGWA TENA AFRIKA, YAIPIGA WYDAD 1-0 TUNISIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top