• HABARI MPYA

    Wednesday, September 10, 2014

    SIMBA SC KUCHEZA NA URA IJUMAA TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC Ijumaa itacheza mechi ya tano ya kujipima nguvu dhidi ya URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mabingwa hao wa zamani Uganda, wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam kesho kwa ajili ya mchezo huo, ambao kocha Patrick Phiri atakifanyia tathmini ya mwisho kikosi chake kabla ya Ligi Kuu kuanza.
    Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii mjini Dar es Salaam kwamba maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri.
    Mwendo wa vipara; Kocha Patrick Phiri kushoto akiwa na Msaidizi wake, Suleiman Matola

    “Maandalizi yanaendelea vizuri na URA ambayo ni moja ya timu bora kabisa katika ukanda wetu itawasili hapa kesho tayari kwa mchezo wa keshokutwa,”amesema Kaburu.
    Kaburu amewaomba wapenzi wa Simba SC kote Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi Ijumaa kuishuhudia timu yao kwa mara ya mwisho kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
    “Lengo la mechi hizi ni kuuthibitisha uwezo wa wachezaji wetu na timu yetu kwa ujumla kabla ya ligi kuanza, sasa tunaomba na wapenzi waje tusaidiane katika hili,”amesema.
    Kwa sasa Simba SC imepiga kambi Mbezi Beach mjini Dar es Salaam kujiandaa na Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.
    Tayari Simba SC imecheza mechi nne chini ya Phiri za kujipima nguvu na kushinda zote, dhidi ya Kilimani FC 2-1, Mafunzo 2-0, KMKM 5-0 zote Zanzibar na Gor Mahia ya Kenya 3-0.
    Phiri alirithi mikoba ya Mcroatia, Zdravko Logarusic aliyetupiwa virago mwezi uliopita baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na ZESCO United ya Zambia katika mchezo wa kirafiki Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUCHEZA NA URA IJUMAA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top