• HABARI MPYA

    Saturday, December 01, 2012

    HUYU NDIYE KIPA ASIYEFUNGIKA TUSKER CHALLENGE

    Ally Kimera asiyefungika

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    KIPA namba mbili wa Uganda, Ally Kimera ameendelea kushika vizuri mikoba ya kipa namba moja nchi hiyo, Abbel Dhaira kwa kuwa mlinda mlango pekee ambaye hajafungwa hadi sasa katika mashindano haya.
    Kimera alimpokea Dhaira kipindi cha pili katika mchezo wa kwanza wa Kundi A dhidi ya Kenya na ameendelea kudaka mechi mbili zaidi hadi kumaliza hatua ya makundi, akiwa hajaruhusu nyavu zake kuguswa hata mara moja.
    Huyu sasa anajitengenezea mazingira mazuri ya kuwa kipa bora wa mashindano haya, yaliyoanza Novemba 24 na yanatarajiwa kutia nanga Desemba 8, mwaka huu mjini hapa.
    Kipa wa Kenya, Duncan Ochieng ametunguliwa mabao mawili katika mechi tatu alizodaka, kipa wa Ethiopia, Samson Asefa Worku, ametunguliwa mabao matatu katika mechi tatu na kipa wa Sudan Kusini, Juma Ginaro anashika rekodi ya kufungwa mabao mengi, saba na timu yake imetolewa.    
    Kipa wa Burundi, Arthur Arakaza amefungwa bao moja katika mechi mbili, kipa wa Tanzania, Juma Kaseja amefungwa bao moja pia, tena kwa penalti, katika mechi mbili, kipa wa Sudan, Abd Elrahman Ali amefungwa mabao mawili katika mechi mbili, wakati kipa wa Somali, Moalim Abdullahi amefungwa mabao sita.
    Kipa wa Zanzibar Mwadini Ally amefungwa bao moja, kipa wa Rwanda, Jean Claude Ndoli amefungwa mabao mawili, kipa wa Malawi, Charles Swini amefungwa mabao manne na kipa wa Eritrea, Fitsum Kelati amefungwa mabao matatu.
    Lakini makipa wa timu za Kundi B na C wana jukumu la kulinda milango yao katika mechi za mwisho za makundi yao, ili kuzilinda rekodi zao pia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HUYU NDIYE KIPA ASIYEFUNGIKA TUSKER CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top