• HABARI MPYA

  Thursday, January 29, 2009

  MASHABIKI YANGA WAWAJERUHI WACHEZAJI MTIBWA

  Kipa wa Mtibwa Kado aliyedaka mpira


  WACHEZAJI wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado, Salum Ussi na Uhuru Suleiman wamejeruhiwa baada ya basi lao kushambuliwa kwa mawe na mashabiki wa Yanga baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juzi uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Imedaiwa baada ya mechi hiyo, mashabiki wa Yanga, walilifuata basi hilo na kuanza kulishambulia kwa mawe na kuvunja vioo, ambayo viliwajeruhi nyota wa klabu ya kijiji cha Lusanga, Turiani mkoani Morogoro.

  Akizungumza kutoka Hospitali ya Aga Khan, alikolazwa Kado alisema kwamba vioo vya dirisha vilimkata sehemu za usoni ikiwemo machoni hali inayomfanya ashindwe kutazama vizuri.
  "Kwa sasa inanipa tabu kuangalia hata mwanga, jicho linatoa machozi wakati wote…unajua jiwe lilipopiga kioo cha basi chupa zikanifikia, nadhani zimeharibu retina…," alisema.
  Baada ya kuona mawe yanazidi, wachezaji wa Mtibwa waliteremka kwenye basi lao kwa ajili ya kupambana nao lakini walishindwa na kurudi kwenye gari ndipo polisi walitokea na kuanza kupiga mabomu ya machozi kwa ajili ya kuwatawanya watu.
  Wachezaji ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo ni Kipa Shaaban Kado ambaye amejeruhiwa jichoni, Uhuru Suleiman ameumizwa kwenye goti na Salum Ussi amepata majeraha kichwani.
  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke Emmanuel Kandilahabi alikiri viongozi wa Mtibwa kufika wakiwa na mtuhumiwa Daud Mkunde ambaye ni shabiki wa Yanga wanaodhani kuwa ndiye aliyeharibu gari lao.
  Hata hivyo Kamanda huyo alisema kuwa ndani ya gari hilo ambalo limepasuliwa vioo na namba zake za usajili ni T 324 ADK aina ya Isuzu Journey kulikuwa na wachezaji wa Mtibwa na shabiki wa Mtibwa aitwae Adolf Shaaban, ambaye alikuwa ameumizwa maeneo ya kichwani.
  Kamanda huyo alisema kuwa polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo iliwapate mashahidi kamili wa tukio hilo.
  Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela alisema kwamba uchunguzi unafanyika na adhabu kali itawakabili wahusika.
  "Tutalifikisha suala hili kwenye kamati ya mashindano na hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa…sisi kama TFF tunalaani mashambilizi ya wachezaji, huu ni uhuni na sheria zitachukua mkondo wake," alisema.

  BONGOSTAZ:
  bongostaz inalaani vikali kitendo hiki, kwani si cha kimichezo, ushabiki wa aina hii ulikwishapitwa na wakati na ndio maana FIFA inasistiza juu ya mchezo wa kiungwana (Fair Play).
  Mashabiki wa Yanga wanapaswa kuzingatia kwamba, mchezaji wa Mtibwa Sugar anaweza akawa mchezaji wa klabu yao wakati wow0te.
  Leo hii kwenye kikosi cha Yanga kuna Kiggi Makasy na Amir Maftah ambao awali wa likuwa Mtibwa, kwa sababu hiyo uadui ambao mashabiki wa Yanga wanataka kuujenga dhidi ya timu ya kiungwana kama Mtibwa, unaweza ukawagharimu wao wenyewe baadaye.
  Uongozi wa Yanga unapaswa kuiomba radhi Mtibwa kwa tukio hili na pia kulipa fidia ya matibabu ya wachezaji waliojeruhiwa na uharibifu wa mali uliofanywa. Michezo ni furaha, amani na upendo na wala si uadui kama walivyofanya mashabiki hawa wa Yanga.
  POLENI MTIBWA SUGAR:
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MASHABIKI YANGA WAWAJERUHI WACHEZAJI MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top