• HABARI MPYA

    Tuesday, January 20, 2009

    AMBANI: INJINI YA MABAO YANGA


    BONIFACE NGAIRAH AMBANI:
    Baba Dantee, Shantee anayewaadhibu atakavyo makipa wa Ligi Kuu ya TZ Bara


    MABAO matatu aliyofunga katika mechi mbili za Ligi Kuu ya Tanzania Bara yanamfanya aonekane kuwa ni chaguo sahihi katika usajili mpya wa klabu ya soka ya Yanga.
    Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Prisons, alifunga mabao mawili kati ya manne yaliyofungwa na timu yake, huku akifunga moja katika ushindi wa mabao 2-1 iliyoupata katika mchezo wa pili wa Ligi hiyo dhidi ya JKT Ruvu.
    Ukiangalia katika usajili wa mwaka huu wa Yanga, hakuna nafasi iliyosheheni wachezaji wengi kutoka mataifa matatu, huku wakiwa na vipaji vya hali ya juu katika usakataji soka kama nafasi ya ushambuliaji.
    Wapo wachezaji kutoka Kenya, na ‘wazawa’ kutoka hapa nchini. Kwa bahati mbaya, mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mukandile Piere (Laurent Kabanda) ‘alitorokea’ Ubelgiji kujaribu bahati ya kucheza soka la kulipwa.
    Wote hawa wanawania namba nne tu za ushambuliaji ndani ya klabu hii kongwe nchini, kila mmoja anatajitahidi kuonyesha uwezo wake uwanjani ili aweze kumvutia Kocha Mkuu, Profesa Dusan Kondic.
    Akiwa ni mmoja kati yao, tayari alionyesha uwezo mkubwa katika mchezo wake wa kwanza akiwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo dhidi ya Mbagala Market na kufanikiwa kufunga bao moja kati ya mawili iliyoshinda Yanga katika mchezo huo.
    Ana mwili wa wastani uliojengeka kimazoezi na mwepesi awapo uwanjani, huku akiwa na urefu wa futi 6”4, ni mrefu na hodari wa mipira ya kichwa anayeweza kuchezea na kupiga mashuti kwa miguu yote miwili.
    Anaitwa Boniface Ngairah Ambani, mshambuliaji mpya wa Yanga ambaye ni raia wa Kenya, aliyezaliwa miaka 31 iliyopita huko nchini Kenya.
    Ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto saba ya Mzee Ernest Ambani na mama Josephine. Nduguze ni Fred, Vincent, Betty, Caro na wengineo.

    ILIKUwAJE AJIUNGE NA SOKA?
    “Ni mchezo uliokuwa katika damu yangu tokea nilipokuwa mdogo, ingekuwa ngumu kwangu kujiunga na mchezo mwingine nje ya soka,” anasema Ambani.
    Alianza kucheza soka ngazi ya klabu mwaka 1995, katika klabu ya Eldoret Cereals, kisha kuhamia Eldoret Rivatex, kabla ya kutua AFC Leopards mwaka 1998 katika ligi kuu ya Kenya.
    Unaweza kuanzia AFC Leopards mwaka 1998, lakini mwenyewe anapenda kusema hapo napo alikuwa anaendelea kukuzwa katika soka, lakini atakwambia Oseriana Fastac ya Kenya mwaka 2000-2002.
    Labda unaweza kushangazwa kidogo na jambo hili, ni kwamba wakati Ambani anacheza katika klabu hii, mshambuliaji wa sasa wa Yanga, Ben Mwalala, alikuwa ni mmoja wa mashabaki wake kiasi cha Mwalala kuruka ukuta katika moja ya mechi za timu hiyo ili aweze kumshuhudia Ambani akifanya vitu vyake.
    Mwaka 2003 alijiunga na Kenya Pipeline, lakini hakudumu sana katika klabu hiyo na kutimkia Oman mwishoni mwa mwaka huo na kusajiliwa katika klabu ya Helal kwa msimu wa mwaka 2003/2004. Alirudi tena Pipeline mwaka 2005 na kuiacha tena katika mataa klabu hiyo na kwenda Vietnam mwaka huohuo katika klabu ya Binh Duong.
    Alirudi tena Kenya mwaka 2006 na kujiunga na Tusker, kabla ya kutimkia India mwaka uliofuata katika klabu ya East Bengal ya India na kuihama mwaka huohuo na kujiunga na Sporting Club De Goa nchini humo.
    Mwaka huu mwanzoni, alijiunga na Salgaocar Sports Club, ambayo hata hivyo ameihama na kujiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili.


    AMBANI NA SOKA LA KENYA NA TANZANIA:
    “Kenya timu zinacheza vizuri kama ilivyo kwa Tanzania, lakini kutokana na kuwa katika adhabu ya FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), Kenya kidogo ililegalega katika maandalizi mbalimbali, lakini sasa mambo ni sawa,” anasema Ambani.
    Lakini anafafanua kuwa mapinduzi makubwa katika soka yaliyotokea katika miaka ya hivi karibuni angalau sasa nchi hizo za Afrika Mashariki zinaweza kutoa ‘maprofessional’ wengi katika siku za usoni.

    SOKA LA INDIA:
    “Wapo juu zaidi ya nchi yoyote ya ukanda huu wa Afrika (Mashariki na Kati) hasa baada ya makampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini ligi na timu zinazocheza ligi hiyo, wana viwanja vizuri sana kwa mpira,” anasema.
    “Najua kila mtu anaweza akashangaa jinsi nilivyotoa maamuzi ya kustaajabisha kwa kujiunga na Yanga, lakini lazima ifahamike mimi ni mchezaji niliye na malengo yangu maalumu katika soka na maisha kwa ujumla,” anasema Ambani.
    Anasema amejiunga na Yanga ili apate nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa barani Afrika, ambako timu hiyo itawakilisha Tanzania baada ya kuwa mabingwa wa Tanzania Bara mwaka huu.
    Sababu nyingine aliyoitoa Ambani ni kuwa kitendo cha kuwa mbali na familia yake kilimfanya kuwa mnyonge huko ugenini, hivyo alivyopatiwa nafasi Yanga aliona ni vyema akajiunga nayo ili aweze kuwa karibu na familia yake iliyopo Nairobi, Kenya.
    “Ni bora pia kucheza ligi kuu ukiwa na Yanga kuliko kucheza daraja la tatu katika klabu yoyote ya Ulaya, kwani hapa unapata kila kitu unachohitaji, ya nini ukapate tabu kana kwamba unaanza kucheza soka,” anasema.

    KIPI KIPYA ALICHOKILETA YANGA?
    “Naijua Yanga tokea kabla, sasa nini nitafanya naomba mashabiki watulie na kuangalia kile nitakachofanya, mimi ni mchezaji kama ilivyo kwa wengine, nafikiri kwa kushirikiana na wenzangu natumai nitashinda,” anasema Ambani.
    Anasema anaweza kutumia kasi na uwezo wake wa kumiliki mpira na kupiga mashuti kwa miguu yake miwili wakati wowote.
    Ambani aliweza kuisaidia vilivyo Yanga katika michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mpaka kuifikisha klabu hiyo katika hatua ya Nusu Fainali ilipotolewa katika hatua hiyo na Tusker ya Kenya, ambao baadaye waliibuka mabingwa wa michuano hiyo.
    Katika Ligi Kuu ya Tanzania mwaka huu, ndiye anaongoza kwa kufunga akiwa amefunga mabao 13 hadi sasa, wakati Yanga inaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 10.

    MATAJI BINAFSI ALIYOWAHI KUTWAA:
    Aliwahi kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Kenya mwaka 1995, akiwa na klabu ya Cereals, baada ya kuzifumania nyavu mara 22. Akiwa na AFC Leopard, mwaka 1998 alishika namba mbili kwa ufungaji wa mabao katika ligi hiyo, baada ya kufunga mabao 14.
    Alipata pia kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Kenya msimu wa 2005/2006 kwa kufunga mabao 26, baada ya kucheza mechi 38, pia aliwahi kushika nafasi ya pili ya ufungaji bora wa ligi kuu ya Oman mwaka 2004, baada ya kufunga mabao 16.

    MATAJI ALIYOTWAA NGAZI YA KLABU:
    Ndani ya mwaka wake wa kwanza kucheza ligi kuu ya Kenya, mwaka 1995 Ambani aliiwezesha Cereals kutwaa ubingwa wa Kenya na mwaka uliofuata alitwaa taji la ubingwa wa Moi Golden akiwa na klabu ya Eldoret Rivatex ya Kenya.
    Ubingwa wa Kenya (1998) akiwa na AFC Leopard, akiwa na Oserian Fastac alitwaa ubingwa wa Kenya miaka miwili mfululizo (2000, 2001) pamoja na ule alioupata akiwa na Tusker mwaka 2005.

    MECHI 33 MABAO 15:
    Mpaka sasa amecheza mechi 33 akiwa na timu ya taifa na kuifungia mabao 15, hii inamaanisha ana wastani wa bao moja katika michezo miwili aliyocheza katika kikosi cha kwanza cha Harambee Stars.
    “Ni furaha na fahari kwangu kucheza mechi hizo katika ngazi ya klabu na timu ya taifa,” anasema Ambani.

    MECHI ZA KIMATAIFA AKIWA NA HARAMBEE STARS:
    Alionekana kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa mwaka 1998, katika mchezo dhidi ya Djibouti na kufanikiwa kufunga mabao mawili katika mchezo huo.
    Amewahi kuchezea Harambee Stars katika mechi ngumu kama zile zilizowakutanisha dhidi ya Nigeria, Afrika Kusini, Tunisia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nyinginezo.
    Alipata heshima ya kuwa nahodha wa Harambee Stars mwaka 2006 katika mchezo ulioikutanisha Kenya na Angola Novemba.
    “Ni nzuri endapo itaendelea na kasi iliyonayo sasa, ni lazima iwe mahala ilipo, hasa baada ya Rais Kikwete (Jakaya) kujitolea katika michezo, Kenya tulishindwa kupiga hatua katika muda muafaka baada ya kugubikwa na migogoro ndani ya Chama iliyopelekea kufungiwa na FIFA huko nyuma,” anasema Ambani.
    Kama ilivyo kwa mchezaji yeyote yule duniani, Ambani ana malengo ya kuitumia michuano ya ligi ya mabingwa kama njia yake ya kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.

    NUSURA NDOTO YAKE IFIFIE:
    Baada ya Yanga kutopeleka timu katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa kombe la Kagame dhidi ya Simba, timu hiyo ilipigwa faini ya dola za Marekani 32,000 na Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ikiwa sambamba na kutoshiriki michuano hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, tena ambayo timu hiyo itakuwa inafuzu kushiriki.
    Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) nalo likaiongezea adhabu Yanga kutokana na kosa hilo kwa kuifungia kushiriki michuano ya kimataifa, ikiwemo Ligi ya mabingwa ambayo klabu hiyo ilitakiwa kushiriki mwakani. Hapo ndipo ndoto za kucheza michuano ya kimataifa kwa Ambani ilipoanza kuweka wingu jeusi, lakini baada ya muda kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo kukaa na kuipitia rufaa ya klabu hiyo, iliiamuru TFF ‘kuitoa kifungoni’ Yanga na kuiruhusu kushiriki Ligi ya mabingwa.

    KUTOKA KWA SUNDAY KAYUNI 1998 HADI KONDIC 2008:
    Ambani amewahi kufundishwa na makocha wengi wa Kiafrika na wale wanaotoka nje ya Afrika, miongoni mwao ni: Tahir Muhiddin (Oseriana Fastac ya Kenya mwaka 2000-2002), Sunday Kayuni (AFC Leopard, Kenya 1998), Bernard Lama, Christian Chukwu, Reinard Fabisch, Tom Olaba wote katika timu ya taifa na yule wa sasa katika timu hiyo, Francis Kimanzi, pia aliwahi kufundishwa na Jacob ‘Ghost’ Mulee katika klabu ya Tusker na timu ya taifa.
    Akiwa India alifundishwa na makocha Roberto Perreira (kutoka Brazil) katika klabu ya East Bengal, Clifford Chukuama (Sporting Club de Goa), Carlos Medeira (Salgoacar FC) mpaka wa Profesa Dusan Kondic mwaka huu akiwa na Yanga.

    MHASIBU ALIYEHAMISHIA HESABU ZAKE KATIKA SOKA:
    “Najua ninaonekana wa ajabu kuacha kazi niliyosomea na kucheza soka, lakini Mungu amenipa kipaji cha soka, wacha nikitumikie kwanza halafu baadaye nitahamia katika uhasibu,” anasema Ambani.
    Alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Shikondi na Nanyuki kuanzia mwaka 1983 mpaka 1990. Elimu ya sekondari aliipata katika shule za sekondari za Makhokho na Nanyuki kuanzia mwaka 1991 mpaka 1994.
    Mwaka 1996 alijiunga na taasisi ya sayansi na teknolojia ya Rift Valley kwa ajili ya msomo ya uhasibu na kutunukiwa cheti (Certified Public Accountant – CPA Part II).

    FAMILIA:
    Amemuoa mfanyakazi wa hotelini aitwaye Hellen Anyango na kufanikiwa kupata watoto wawili ambao ni Dantee (6) na Shantee wa kike, mwenye miaka mitatu.
    Mwisho
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMBANI: INJINI YA MABAO YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top