• HABARI MPYA

  Thursday, January 22, 2009

  GEOFFREY BONIFACE NAMWANDU: Injini mpya Yanga


  GEOFFREY BONIFACE NAMWANDU:  NINAPOMTAZAMA akicheza, huwa ninatamani ningekuwa nikicheza naye, nikiwa aidha beki wa kushoto au wa kulia.
  Nina uhakika nisingezomewa na shabiki yeyote kwa kuboronga hata kama kiwango changu cha soka ni kidogo.
  Hali hiyo inatokana na uwezo wake wa kutafuta nafasi na kuwapo katika wakati mwafaka popote mpira utakapokuwa.
  Akitoa pasi, basi yeye atakuwa ni wa kwanza kuomba pasi ile, na kuitawanya kwa mwingine ambako pia nako atakuwa ni wa kwanza kuwapo katika nafasi murua ya kupasiwa.
  Hakika Geofrey Bonny anazijua kanuni za soka, ambazo mojawapo inasema kuwa mtoaji pasi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kuipokea pasi ile.
  Mpira ukiwa kwa beki wa kushoto, atakayekuwa katika nafasi nzuri ya kupewa pasi atakuwa ni Bonny, kama itakavyokuwa iwapo mpira utakuwa kwa beki wa kulia.
  Hakika, uchezaji wa Bonny unalingana kwa karibu na ule wa viungo waliowahi kutamba nchini kama Hussein Marsha, Salvatory Edward, Seleman Matola na wengineo wa aina yao. Kiungo huyo wa dimba la chini wa Yanga na Taifa Stars, ni moja ya vipaji halisi vya soka la Tanzania, lakini akichelewa kuitumikia nchi ipasavyo kama alivyokiri mwenyewe.
  “Ninamshukuru sana Marcio Maximo (Kocha Mkuu wa Stars- timu ya taifa), ndiye aliyenitoa gizani na kunileta katika ulimwengu wa soka, na leo hii ninafurahia maisha yangu ya soka tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuja Stars,” alisema Bonny.
  Kiungo huyo aliyeitwa Stars mwaka jana na kujinyakulia namba katika kikosi cha kwanza cha Maximo, pia alielezea masikitiko yake kutokana na kuchelewa kujiunga na Yanga, ambayo kwa kiasi fulani, imemwezesha kubadilisha maisha yake tofauti na alivyokuwa Prisons ya Mbeya.
  “Ninafurahia kila kitu ndani ya Yanga. Kuna utofauti mkubwa kati ya timu hizi kubwa na zile za mikoani, hapa wachezaji wanalipwa mishahara, viongozi na wapenzi wanawajali wachezaji.
  “Pia timu zinapata wafadhili ambao hutoa fedha zao nyingi tu kwa wachezaji. Mfano Yanga tuna mfadhili wetu Yusuph Manji, na bado kuna TBL (Kampuni ya Bia Tanzania) ambayo nayo imeifadhili timu, timu za mikoani hali si kama hii,” alisema Bonny na kuongeza:
  “Hakika ninajuta kwa nini nilichelewa kuja Yanga. Soka langu na hata hali yangu kimaisha imebadilika kwa kiasi kikubwa tofauti na zamani.”
  Akizungumzia maisha yake ndani ya Stars, Bonny alisema kuwa kikosi hicho kimempa somo muhimu mno la uchezaji wa soka. “Zamani nilikuwa nikicheza ninavyotaka kulingana na uwezo wangu, lakini ndani ya Stars, Maximo amenifundisha kitu kikubwa sana, kucheza kitimu, hali inayohitaji kutumia akili zaidi kuliko nguvu kama nilivyokuwa nikifanya zamani,” alisema.
  Alisema kuwa Stars imempa uzoefu mkubwa katika maisha yake ya soka na kwamba kuna baadhi ya mechi alizoichezea timu hiyo zimempa changamoto ya kutosha maishani mwake.
  “Mechi ambayo nitaendelea kuikumbuka ni ile kati ya Stars na Cameroon, iliyochezwa kwenye Uwanja Mpya (wa Taifa, Dar es Salaam). Ingawa tulitoka sare, lakini ilikuwa ni muhimu mno kwangu, kucheza na wachezaji kama Samuel Eto’o si kitu kidogo, kwani ni miongoni mwa wachezaji bora duniani,” alisema.
  Kama ilivyo kwa wachezaji wengi, Bonny alianza kucheza soka tangu alipokuwa mdogo, akishiriki katika mashindano mbalimbali ya shule wakati akisoma katika Shule ya Msingi Tukuyu Polisi na baadaye Sekondari za Ndembela ya Mbeya na Makongo ya Dar es Salaam.
  Mbali na timu za shule, pia aliwahi kuzichezea Tukuyu Stars, 44 KJ Mbalizi, Prisons aliyodumu nayo miaka mitano na hatimaye Yanga.
  Huyo ndiye Geoffrey Bonny, ambaye ni mtoto wa pili katika familia ya watoto wanne wa Mzee Boniface Namwandu na mama Zelia Sigonda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GEOFFREY BONIFACE NAMWANDU: Injini mpya Yanga Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top