• HABARI MPYA

    Friday, January 23, 2009

    JUMA NASSOR PONDAMALI: Kipa aliyeweka rekodi kwa mbwembwe, ngumi na vituko uwanjani

    Pondamali (kushoto) akiwa na Ivo Mapunda


    na mahmoud zubeiry
    INGAWAJE bado anapenda kuvaa mavazi ya ujana, lakini hivi sasa ni mtu mwingine kabisa.
    Ni mtu asiyependa ukorofi wa aina yoyote, akitumia muda mwingi katika shughuli zake za ukocha na ibada.
    Huyu ni mmoja wa makipa maarufu kabisa kuwahi kutokea katika ulimwengu wa soka Tanzania, Juma Nassor Pondamali, kwa jina la utani ‘Mensah’.
    Ni kipa aliyetamba Afrika kutokana na uhodari wake wa kuokoa michomo mikali kwa mbwembwe za aina yake, ambazo mara kwa mara ziliwaacha mashabiki wake midomo wazi.
    Wakati anacheza soka, ilikuwa ni kawaida yake kuvunja mechi kabla ya muda, kwa sababu ya aidha kumvamia mchezaji mwenzake au mwamuzi na kuwarushia makonde au kuwapiga kwa staili ya kung-fu.
    Leo, takriban miaka 10 tangu astaafu soka, mwenyewe anasema kwamba matukio hayo, ambayo yalimfanya atumikie adhabu mara kwa mara za kufungiwa kwa utovu wa nidhamu, yalitokana na yeye kuchukia kuonewa.
    “Sikuwa mtu wa kupenda kuonewa hata kidogo.” Anasema. “Nilikuwa tayari kumchapa mtu bila ya huruma. Nilikuwa ninajiamini, nina uwezo wa kupigana na hata watu 15.
    “Mimi ninacheza karate, nilianza mazoezi nikiwa mdogo sana wakati nasoma shule ya msingi.”
    Kutokana na umahiri wake, makipa wengi walijaribu kumuiga Pondamali, lakini hakuna hata mmoja aliyebahatika kufikia hata nusu ya mbwembwe alizokuwa akifanya enzi zake.
    Mengi yanazungumzwa kuhusu yeye, lakini mwenyewe anasikitika kwa madai kwamba yote ni upotoshaji wa ukweli.
    “Unaweza kukuta mtu anazungumza mambo ya Pondamali kwa kujiamini, lakini anasema uongo,” anasema.
    “Kama matukio kadha niliyafanya ya kishujaa na kushangaza umma wa wlaioshuhudia, lakini yanapotoshwa.”
    Kwa mfano, anasema katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980, akiwa kipa wa timu ya taifa, Taifa Stars, walimenyana na Cote d’Ivore.
    Kaitka mechi hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Surulere, mjini Lagos, Nigeria, Pondamali anasema alidaka mpira na kuuficha, kiasi cha kumfanya mwamuzi adhani ni bao na kuamuru mpira uwekwe kati.
    “Sasa watu wanasema mpira ule niliuweka ndani ya jezi, si kweli.
    “Jamaa alipiga shuti kali sana, nikalidaka na kuuficha mpira chini ya mapaja, nikiwa nikekaa kama natoa shahada huku nimeshika tama.
    “Refa akadhani bao, akapiga filimbi mpira uwekwe kati, mimi nikautoa na kuwaonyesha mashabiki. Walishangilia sana kwa kunipigia makofi.
    “Refa alikasirika, akanipa kati ya njano. Sasa kwa kuwa alishapiga filimbi ya bao, ikabidi abuni sheria yake mpya. Aliamuru mpira upigwe goal-kick, hadi mwisho tulikuwa 1-1” anasema Pondamali akikumbushia vituko alivyofanya uwanja wa Surulere mjini Lagos, Nigeria.
    Pondamali anasema kwamba baada ya tukio hilo, FAT ilimwonya apunguze mbwembwe kwa sababu hata Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lililalamikia hali hiyo.
    Tukio jingine ambalo anadai linapotoshwa, ni katika fainali ya Kombe la Challenge mjini Khartoum, mwaka huo huo 1980, wakati Bara ilipomenyana na wenyeji Sudan.
    “Nahodha wa Sudan, Mustapha Nagal alipiga shuti kali. Nilidaka, halafu nikamrudishia. Alipiga tena, nikatoa nje ikawa kona.
    “Hiyo, (wenzangu) walishindwa kuvumilia. Kina Jellah Mtagwa, Leodgar Tenga na Juma Mkambi walikujajuu na kutaka kunitoa roho. Niliwaomba msamaha, yaliisha.”
    Tukio la mwisho analosema linapotoshwa, ni katika mechi ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu ya Vodacom) kati ya Yanga na African Sports ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa, 1989.
    Katika mechi hiyo, Pondamali alikuwa akiichezea Yanga, ambayo anakiri aliifungisha bao la kipuuzi kutokana na kufanya mbwembwe.
    “Hadi half-time (mapumziko), tulikuwa tunaongoza 1-0. Kipindi cha kwanza nilipigiwa shuti kali. Nililidaka kwa miguu, nikauchezea mpira, halafu nikauweka mgongoni nikaurudisha ka mbele, nikaanza. Ulichezwa bila ya madhara yoyote.
    “Sasa kipindi cha pili (katika) dakika za lala salama. Kenny Mkapa alinirudishia mpira. “Victor Mkanwa alikuwa mbele yangu, nikafanya kama ninadaka, nikaucheza kwa miguu.
    “Basi Mkanwa alinivamia, alinipiga push nikahama kwenye mpira, akaenda kufunga bao. Ikawa 1-1.
    “Pale pale beki wa kulia Fred Minziro akanifuata eti anipige. Nikamwambia wewe, usipende sifa, usijione kama umebeba bango la Yanga mgongoni,” nenda zako.
    “Alinywea, akaondoka kwa sababu mimi sikuwa mtu wa kuchezea na yeye alikuwa anajua.”
    Mbali na hayo, Pondamali anazungumzia pia matukio ya yeye kufungiwa.
    Anasema kuwa mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1980 mjini Mwanza, wakati timu yake ya Pan African ilipomenyana na Tumbaku ya Tabora katika mechi ya ligi, wakati huo ikichezwa kwa makundi katika hatua ya kwanza.
    “Mshambuliaji mmoja wa Tumbaku, (alikuwa) Jumanne Kigozi. Nakwenda kudaka mpira hewani, alinikumba, nikapoteza mwelekeo na kuanguka chini,” anasema.
    “Basi nilipoamka, nikamkata ngwala na kumrushia ngumi. Ugomvi ulizuka, mechi ikavunjika. Nilifungiwa miezi mitatu.
    “Kwa kuwa Stars ilikuwa na majukumu makubwa ya kwenda katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, mwaka huo 1980, FAT ilinifungulia. Nikaenda Lagos.
    Baada ya kurejea Lagos, mwaka 1981, Pondamali alifungiwa tena baada ya kumpiga mwamuzi.
    “Ilikuwa mechi kati ya timu yangu ya Pan na Maji Maji mjini Songea,” anasema.
    “Ilipigwa krosi langoni kwetu, Ally Boimanda wa Maji Maji akanisukuma, mwenzake Peter Mhina akafunga bao.
    “Nililalamika kwa refa, (lakini) hakujali. Basi ile anaandika andika. Nilimtwanga makonde, mpira ukavunjika.
    “Nilichukuliwa na FFU hadi nje ya Uwanja. Niliwaambia nirudisheni uwanjani, kweli bwana wakaniachia. “Nilirudi kudaka hadi mwisho. Nikafungiwa miezi sita.
    Adhabu ya mwisho kwa Pondamali, ilikuwa mwaka 1982 katika mchezo baina ya Pan na Simba kwenye Uwanja wa Taifa.
    Adam Sabu alinivamia na kunisukuma. Mwenzake Jumanne Masimenti akafunga bao.
    “Maana yake mimi hivi hivi nilikuwa sifungiki, ndiyo maana walikuwa wakinifanyia upuuzi huo.” “Kwa hiyo, mimi nilikuwa sikubali. Ndiyo maana nilikuwa nafungiwa kila mara.
    “Sasa baada ya bao hilo nilikwenda kulalamika kwa refa, hakujali. Nilimvamia na kumpiga sana. “Alinipa kadi nyekundu, nikagoma kutoka uwanjani, mechi ikavunjika. Hata viongozi wa Pan, walikuwa wakiniogopa. Kwa hiyo hawakuthubutu kuniambia nikubali kosa.
    Mwenyekiti wa FAT enzi hizo, Said El-Maamry alikuwapo uwanjani akanifungia miaka mitano. Lakini haikufika hata nusu yake, nikafunguliwa.”
    Mbali na vituko hivyo, Pondamali alikuwa hodari. Mwenyewe anasema mambo mengi aliiga kwa aliyekuwa kipa wa Simba na Taifa Stars, Athumani Mambosasa (sasa marehemu).
    “Nilikuwa naiga vitu vya Mambosasa, halafu mimi nilikuwa nakarabati viwe hata zaidi, kama vile kudaka mpira kwa mkono mmoja.” “Mimi naweza kudaka, huku natetemeka, ilionekana (mbwembwe)”.
    Anasema mechi iliyo katika kumbukumbu yake kutokana na kudaka kwa umahiri mkubwa, anasema ni ile ya mwishoni mwa mwaka 1980 ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia baina ya Stars na Nigeria, wakati huo ikiitwa Green Eagles.
    “Mechi ya kwanza kule Lagos, nilidaka sana tukatoka 0-1”, anasema.
    “Lakini uroho wa FAT, (uliifanya) iandae mchezo wa kirafiki kati yetu (Pan African) na Yanga, bila kujali kuwa zimebaki siku tatu kabla ya kurudiana na Nigeria.
    “Matokeo yake, katika ile mechi ya kirafiki, mlinzi tegemeo wa Stars Leodgar Tenga, akapamiana na Kitwana Manara wa Yanga.
    “Tenga aliumia, ilibidi hiyo mechi acheze Isihaka Hassan ‘Chukwu’, (chipukizi aliyekuwa akiinukia vizuri Yanga).
    “Isihaka alishindwa kuhimili vishindo kama ilivyokuwa kwa Tenga kule Lagos, basi tulifungwa 2-0”.
    Pondamali alizaliwa mwaka 1958, Ilala, Dar es Salaam na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Tabata na baadaye Mlimani, kabla ya kwenda kumalizia Karume.
    Anasema kwamba alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Mzizima, ambako hata hivyo anadai kwamba kutokana na matatizo yasiyoweza kuzuilika alikomea Kidato cha Pili na kujikita katika soka.
    Wakati akiwa anasoma, alikuwa akichezea timu ya mtaani Danger Hunters na Biafra za Mburahati, Scotland Yard ya Kariakoo iliyomfanya aonekane Yanga Kids iliyokuwa ikifundishwa na Profesa Victor Stanculescu, Mromania ambaye sasa anaishi Marekani.
    Mwaka 1972, alipandishwa hadi Yanga B iliyokuwa ikifundisha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Athumani Kilambo kabla ya Tambwe Leya kumpandisha kikosi cha kwanza mwaka 1974.
    Aliingia kikosi cha kwanza cha Yanga wakati ikiwa na makipa hodari kama vile Elias Michael ‘Nyoka Mweusi’, Muhidini Fadhili na Patrick Nyaga. Hivyo, mbele ya nyota hao, Pondamali alijikuta akiwa kipa wa ziada.
    Anasema kwamba mambo yalibadilika mwaka 1975, baada ya kutokea mgogoro baina ya wachezaji na viongozi.
    “Wachezaji wote walifukuzwa, wale wakubwa tuliowakuta Yanga A, walikwenda kujiunga na Nyota Afrika ya Morogoro,” anasema.
    “Sisi watoto tulichukuliwa na TBL (Kampuni ya Bia Tanzania).”
    Pondamali anawataja nyota ambao anakumbuka chipukizi wenzake aliokwenda nao TBL kuwa ni Adolph Rishard, Mohamed Yahya “Tostao”, Kassim Manara, Mohamed Mkweche na wengineo.
    Anasema miaka miwili baadyae, walifuatwa na viongozi wa Pan African, akiwamo pia Mzee Tabu Mangara (sasa marehemu) aliyekuwa amejiengua Yanga.
    “Tulienda Pan. Tulikutana na wale waliokimbia Nyota, tukaunda timu. Ilikuwa tishio sana,” anasema.
    Pondamali ambaye alifiwa na babayake mzazi akiwa bado anapakatwa na mama yake ambaye mpaka sasa yuko hai, anasema kwamba aliichezea Pan hadi mwaka 1985 aliporejea Yanga, ambako aliidakia hadi mwaka 1990 alipoachwa.
    Baada ya kuachwa Yanga 1990, alikwenda kuipandisha Pan kutoka daraja la tatu ilikokuwa imeshuka, hadi la kwanza mwaka 1993.
    “Ilipopanda, nikaonekana sifai, nikaachwa. Nilienda zangu Kenya, nilitafutiwa timu na rafiki yangu kipa wa zamani wa Harambee Stars, Mahmood Abbas.
    “Nilijiunga na AFC Leopard, ambayo niliidakia hadi mwaka 1996 nilipoamua kustaafu soka.”
    Pondamali alichaguliwa kikosi cha Taifa Stars mwaka 1976, ambayo aliichezea hadi mwaka 1982 alipoachwa kutokana na ukorofi wake na si kushuka kwa kiwango chake.
    Baada ya kustaafu, Pondamali hakupenda kuupa kisogo mchezo huo. Aliamua kujifunza ukocha mwaka 1997, alipata kozi ya awali.
    Mwaka 1998, alisoma kozi ya Intermediate na baadaye mwaka huo aliongezea kozi ya CAF, kabla ya kupata kozi za FIFA, Futaro One na Advaned mapema mwaka huo.
    Kabla ya kufikia hapo, Pondamali alikwenda Marekani katika Chuo cha Kajumulo World Soccer, kinachomilikiwa na Mtanzania anayeishi huko, Alex Kajumulo.
    Timu ya kwanza kuifundisha ni Yanga mwaka 1997, akiwa chini ya Sunday Kayuni. Alikaa Yanga hadi mwaka 1999, alipokwenda Sigara (Kajumulo).
    Kajumulo alimpa Pondamali ukocha mkuu katika timu hiyo, lakini hakukaa nayo, baada ya kuhama kabla ya ligi kuanza.
    “Nilihama kwa sababu (Abdallah) Kibadeni na Jamhuri Kihwelo waliingilia kazi yangu,” anasema.
    “Mimi nilipokuwa Marekani, nilikuta wameshasajili timu, halafu wamechukua wachezaji ‘wazee’ watupu. Niliona hii kazi siiwezi, nilijiengua,” anasema Pondamali ambaye kwa sasa yupo Azam FC kama kocha wa makipa na pia ni kocha wa makipa wa timu za taifa za Vijana.
    Alijiunga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, lakini kutokana na kuhitilafiana na uongozi wa timu hiyo, Pondamali anasema aliamua kujiengua mwanzoni mwa mwaka huo na ndipo alipochukuliwa na Kariakoo United ya Lindi, ambako baaadaye alihama na kwenda kuipandisha Pallson ya Arusha Ligi Kuu kabla ya kuitema.
    Pondamali anasema lengo la baadaye ni kujiendeleza zaidi juu ya taaluma yake ya ukocha, na kwamba ana mpango wa kushauri uongozi wa Kariakoo uanzishe timu za watoto, kwa kuwa hata yeye aliibukia huko.
    Anazungumzia soka ya Tanzania na kusema imeshuka mno, kutokana na uongozi mbovu, mfumo mbovu, rushwa na kufa kwa Kombe la Taifa, wachezaji kushindwa kujituma uwanjani na kuweka mbele pesa.
    Pondamali ni baba wa watoto watano, ambao anawataja kuwa ni Njui, Masika, Nassor na Fami, mkewe anaitwa Mwajuma ambaye amefunga naye ndoa mwaka 1999,” na amezaa naye Fami tu.
    Pondamali anasema yeye ni mcheza karate hodari, amabye darasani alifikia kiwango cha kuwa na mkanda wa kijani, lakini katika kujiendeleza mitaani, anadai ameshafikia mkanda mweusi.
    “Ila sasa hivi sipendi ugomvi, nafanya mazoezi kwa ajili ya self-defense tu,” anasema.
    Pondamali ana mengi ya kujivunia katika soka ya Tanzania, ikiwamo kudaka katika mechi ngumu iliyoipa Taifa Stars tiketi ya kwenda Lagos kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980.
    Katika mechi hiyo mwaka 1979 mjini Ndola, Zambia, Pondamali aliokoa michomo mingi ya hatari kutoka kwa washambuliaji wenye uchu wa Zambia, Godfrey Chitalu na mwenzake Alex Chola (sasa marehemu).
    Hakuna ubishi wowote kwamba Pondamali, ni miongoni mwa makipa bora kuwahi kutokea Tanzania na Afrika kwa ujumla.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUMA NASSOR PONDAMALI: Kipa aliyeweka rekodi kwa mbwembwe, ngumi na vituko uwanjani Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top