• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 26, 2009

  SARAKASI YA ZAIN YAHAMIA BIAFRA

  Archelle Eric: Mkufunzi kutoka Ubelgiji, Archelle Eric (kulia) akitoa
  maelekezo wakati wa mazoezi ya viungo kwa wacheza sarakasi wa kikundi
  cha Zain Mama Afrika Sarakasi, Dar es Salaam jana. Maonyesho hayo
  yamehamishiwa viwanja vya Biafra, Kinondoni.

  MAONYESHO kabambe ya sarakasi ya kwanza ya aina yake barani Afrika yanayojulikana kama Zain Sarakasi Mama Afrika, yamehamishiwa kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam na yataanza kuonyeshwa leo (Januari 27, 2009).
  Mkurugenzi na mwandaaji wa maonyesho hayo, Winston Ruddle alisema Dar es Salaam jana kuwa maonyesho hayo yaliyoanza kuonyeshwa Dar es Salaam Novemba mwaka jana, yataendelea kurindima hadi Machi 8, mwaka huu na yatafanyika maonyesho nane kwa wiki kuanzia Jumanne hadi Jumapili.
  Ruddle alisema bei ya tiketi kwa ajili ya maonyesho hayo pia zimepunguzwa ili kuwawezesha watu wengi zaidi kumudu gharama na kufurahia shoo, na akabainisha wameamua kuyahamishia Biafra ili kuleta hamasa zaidi miongoni mwa mashabiki wa madaraja yote.
  Kwa maonyesho ya Jumanne hadi Alhamisi, kategoria ya kiti kimoja inayojulikana kama viti vya rangi nyekundu tiketi zake zitauzwa kwa sh. 14,000, kategoria ya viti viwili vya bluu tiketi zitauzwa sh. 10,000 wakati kategoria ya viti vitatu vya rangi ya kijani zitauzwa kwa sh. 6,000.
  Kwa maonyesho ya Ijumaa hadi Jumapili kategoria ya kiti kimoja ya rangi nyekundu tiketi zake zitauzwa kwa sh. 16,000, kategoria ya viti viwili vya bluu tiketi zitauzwa sh. 12,000 wakati kategoria ya viti vitatu vya rangi ya kijani zitauzwa sh. 8,000. Tiketi zitauzwa nusu ya gharama kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 12.
  Ruddle alisema kila Jumatano usiku utakuwa ni usiku wa wanawake na wote watatazama onyesho kwa nusu ya bei ya tiketi kwa kategoria ya kwanza na ya pili.
  Alhamisi utakuwa ni usiku wa familia ambako watoto wote watalipa kiingilio cha sh. 1,000.
  Maonyesho hayo yaliyofunguliwa Novemba 26, 2008 na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, yalikuwa yakifanyika kwenye Uwanja wa Jeshi Masaki hadi Januari 18, mwaka huu. Meneja Masoko wa Zain, Costantine Magavilla alisema anaamini mashabiki wengi zaidi watajitokeza kwenda kushuhudia maonyesho hayo.
  Magavilla alisema Zain inaona fahari kusaidia kuleta shoo hiyo Tanzania, na baada ya kumalizika Dar es Salaam, yatahamia katika miji ya Mwanza na Arusha.
  Magavilla alisema kutazama onyesho kama hilo Ujerumani inamgharimu mtu kati ya Euro 56 hadi 99 ambayo ni sawa na sh. 100,680 hadi 178,002, lakini akabainisha wameweka kiingilio kidogo ili kuwawezesha watu wengi kumudu kushuhudia.
  Kikundi hicho kilichoundwa mwaka 2001 kina wasanii 65, wengi wao wanatoka Tanzania na wengine wachache kutoka Afrika Kusini, Kenya na Ethiopia ambao huonyesha vionjo mbalimbali na vikaragosi, mazingaombwe na mavazi zaidi ya 500 ya kitamaduni kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SARAKASI YA ZAIN YAHAMIA BIAFRA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top