• HABARI MPYA

    Thursday, January 22, 2009

    Rollingston: Kituo kilichotoa nyota wa soka Tanzania

    na dina ismail
    UWEPO wa vituo vingi vya kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji soka hapa nchini vimekuwa vikisaidia kwa namna moja au nyingine maendeleo ya soka katika miaka ya hivi karibuni.
    Matunda ya vituo hivyo yamekuwa yakionekana kwa namna moja ama nyingine kwani wachezaji wengi ambao wanatamba sasa hapa nchini wengi wao wamepitia katika vituo hivyo.
    Rollingston ni moja ya kituo ambacho naweza kusema kimekuwa kikitoa mchango mkubwa kwa kusaidia kuazalisha wachezaji ambao kwa namna moja ama nyingine wanaonekana wamepikwa na wakaiva kisawasawa.
    Kituo hicho chenye makazi yake mkoani Arusha, hakiishii kwa kukuza na kuendeleza vipaji kwa kuwakutanisha pamoja vijana bali pia huandaa michuano ya vijana yanayohusisha nchi za Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa sasa.
    Katika mahojiano na gazeti hili, Mkurugenzi wa kituo hicho, Ally Mtumwa anasema lengo la kufanya hivyo si kukuza na kuendeleza vipaji vyao tu, bali pia huwaongezea ujuzi zaidi na kuwafundisha kuwa na Uzalendo.
    Mtumwa anasema, ili mchezaji aweze kufamnikiwa zaidi kwanza anatakiwa awe na uzalendo wa kufahamu jukumu alilonalo katika kazi yake hiyo hivyo itamfanya kuelekeza akili yake katika kazi hiyo.
    Kituo hicho kinalea wachezaji zaidi ya 75 lakini ni 15 tu ndio wanaokaa kituoni hapo huku wengine wakikutana na kurudi makwao na hilo linatokana na uwezo mdogo walionao katika kuendesha kituo hicho.
    Mtumwa anasema kituo hicho kipo chini yake kama Kocha Mkuu huku akisaidiana na David Nyembele na Ramadhani Salim ambao wote kwa pamoja wamewahi kupata mafunzo ya fani hiyo ndani na nje ya nchi.
    Pamoja na matatizo iliyonayo lakini, Rollingstone imeweza kutoa wachezaji kadhaa ambao wamekuwa wakichezea timu za Taifa, yaani ile ya wakubwa nay a Vijana chini ya miaka 17 na 20, pamoja na vilabu vikubwa vya Simba na Yanga.
    Kwa upande wa Stars, Rollingstone inajivunia Amir Maftah, Erasto Nyoni na Kiggi Makassy, huku kwa upande wa timu ya Vijana ya chini ya miaka 20, imetoa chipukizi kama, Mahsen Salim, Habib Muhina, Mussa Babu na Babu Ally.
    Rollingstone pia imetoa wachezaji wawili walipo kwenye Tanzania Soccer Academy iliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao ni Hamis Mroki na Zakayo John, huku pia ikitoa wachezaji nane katika mpango wa soka la Vijana wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.
    Mbali na timu ya Taifa timu hiyo pia imetoa wachezaji wanaocheza katika klabu ndani na nje ya nchi wakiwemo Kiggi Makasi, Amir Maftah (Yanga), Erasto Nyoni ambaye anacheza Vital’ O ya Burunbdi, Salvantory Ntebe aliyepo pia Burundi, pia wachezaji wengine ambao wamepelekwa bara la Ulaya kwa njia zisizo rasmi.
    Aidha kupitia mashindano yao ya Vijana, ambayo mwaka huu yatafanyika kwa mara ya nane kuanzia August 3 hadi 14 mjini Arusha kwa kushirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 14 na 20, baadhi ya wachezaji wanaovuma katika Ukanda wa Afrika mashariki na Kati waliwahi kupitia katika michuano hiyo.
    Wachezaji hayo ni pamoja na Beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alishiriki michuano hiyo kwa miaka mitatu mfululizo akiwa na timu ya Vijana ya Zanzibar, pia mshambuliaji wa zamani wa kimataifa Simba, Seleman Ndikumana aliwahi kushiriki michuano hiyo akiwa na timu ya Burundi, pamoja na mchezaji mwibngine wea Burundi anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Valencia.
    Akizungumzia mashindano ya mwaka huu, Mtumwa anasema yatashirikisha timu 24 kutoka katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zanzibar na Tanzania.
    Kwa upande wa wenyeji Tanzania itawakilishwa na bingwa mtetezi, timu ya DYOC, Rollingstone, Tanga, Morogoro, Mwanza na Kigoma, huku mwaka huu kwa mara ya kwanza kutakuwa na timu za Wanawake, moja kutoka nchini Kenya na nyingine Tanzania.
    Anasema lengo la kuandaa mashindano hayo ni kuwasaidia Vijana kuanza kuona na kuzoea michuano ya kimataifa mapema ili katika siku za usoni wasiweze kupata tabu watakapopata nafasio hizo.
    Aidha anasema michuano hiyo inasaidia kuwakutanisha pamoja Vijana hao na hivyo kubadilisha uzoefu kwa namna moja ama nyingine kwani wenyewe kwa wenyewe hupata fursa ya kuona nani ana fanya nini na nini cha kujifunza.
    Kituo hicho pia kipo katika hatua ya kufanikisha kusajili Shirikisho la Academy za Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati na tayari wameshapeleka maombi kwa msajili hivyo wanasubiri majibu.
    Akizungumzia matatizo wanayokumbanna nayo katika mchakato wao huo, Mtumwa anasema, ni pamoja na ukosefu wa wafadhili wa kuwezesha maendeleo ya kituo hicho pamoja na kukosekana kwa wadhamini wa kufanikisha michuano yao kwa kila mwaka.
    Anasema kutokana na kukosa fedha za kutosha wamekuwa wakiendesha mashindano hayo kwa kuishia kutoa zawadi za vikombe tu, lakini hata hivyo analishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuweza kukisaidia kituo hicho kwa namna moja ama nyingine.
    Mbali na hilo pia, timu nyingi zimekuwa zikiwachukua wachezaji wao bila kutoa malipo yoyote kama ilivyo taratibu za kisoka kwa klabu kutakiwa kulipa fedha wanazokubalina kabla ya kumchukua mchezaji wanaye muhitaji.
    Hata hivyo anaipongeza klabu ya Yanga kwa kuweza kulipa kiasi cha fedha kwa ajili ya kumsajili mchezaji aliyepikwa katika kituo hicho, Kiggi Makassy.
    Mtumwa anatoa wito kwa wadau wa soka hapa nchini kuchukulia kitendo hicho kama ni jambo zito ambalo linahitaji ushirikiano mkubwa ili kuleta mafanikio zaidi.
    Pia amewataka wadau wa soka kutumia michuano hiyo kusaka wachezaji watakaowatumia kwenye timu zao na hasa zile za ligi Daraja la kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: Rollingston: Kituo kilichotoa nyota wa soka Tanzania Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top