• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 22, 2009

  Kondic: Bado kidogo tu niwasajili Mgosi, Yondani

  Yondani akichuana na Tonny Mawejje wa URA ya Uganda katika Kombe la Tusker. Kulia anasaidiwa na Henry Joseph.
  na mahmoud zubeiry
  “Kuweza kuwa kileleni baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi, haikuwa kazi nyepesi, tumepigana kwa nguvu zetu zote tangu ligi ilipoanza Agosti (mwaka huu).
  Wakati nakuja hapa (Yanga), mwaka jana niliikuta timu katika hali mbaya, lakini nimeanza kuisuka taratibu, imekuwa inaongzeka ubora siku hadi siku, nimefanya usajili mzuri, timu ni nzuri sasa.”.
  Ndivyo alivyoanza kuzungumza kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Profesa Dusan Kondic katika mahojiano na bongostaz.blogspot.com yaliyofanyika hoteli ya New Afrika mjini Dar es Salaam, Novemba mwaka jana.
  Kondic anasema kwamba anamshukuru mno mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yussuf Manji ambaye amekuwa akimuunga mkono katika kila mpango wake.
  “Manji anaunga mkono programu zangu kwa asilimia 100, na yeye ndiye chachu ya mafanikio yetu, mechi kumi zilizopita, tulipigana kiume, pamoja na mafanikio haya, Yanga haijakuwa ninavyotaka mimi, tunahitaji muda ili wachezaji wapate kunolewa zaidi na waweze kuelewana,”anasema Kondic.
  Mtaalamu huyo kutoka Serbia, alisema kwamba kabla ya kuanza kwa mashindano, timu inahitaji kupata maandalizi ya muda usiopungua wiki sita, lakini Yanga iliingia kwenye michuano ya Kagame bila ya kupata maandalizi ya kutosha.
  Katika michuano hiyo, iliyofanyika Julai mwaka huu, Yanga ilitolewa hatua ya Nusu Fainali na Tusker ya Kenya, iliyoibuka bingwa, kabla ya kugomea mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya watani wao wa jadi, Simba.
  “Kombe la Kagame tulikurupushwa, tulikuwa tumefanya mazoezi kwa wiki mbili tu, sikutaka kabisa kucheza mashindano yale, nilitaka timu iende Ulaya kufanya mazoezi, lakini TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) lililazimisha na sisi tulishindwa kugoma,”anasema Kondic.
  Anasema aliichukulia michuano ya Kagame kama sehemu ya maandalizi yake katika Ligi Kuu na ndio maana baada ya hapo walipokwenda kuweka kambi ya wioki tatu kisiwani, Pemba waliingia kwenye Ligi Kuu na timu imara kidogo.
  “Katika mechi kumi tumeshinda tisa, tumefungwa moja ugenini, mchezo ambao kwa kweli sisiti kumlaumu refa, alituvunja nguvu, alikataa goli letu la mapema, aliwapa wapinzani penalti mapema tu, ilitunyong’onyesha sana,”anasema kuhusu dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba, ambayo Yanga ililala 2-0.


  YANGA ILIBEBWA NA VICTOR MWANDIKE?
  Oktoba 26 mwaka huu, Kondic aliiongoza Yanga kuifunga Simba kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu ya Bara, tangu ilipoifunga kwa mara ya mwisho, Agosti 5, mwaka 2000 2-0 mjini Dar es Salaam.
  Alikuwa ni Ben Mwalala katika dakika ay 15, akiunganisha kwa guu lake la kulia pasi ya Mkenya mwenzake, Boniphace Ambani, ingawa baada ya mechi hiyo wapinzani wao walimlalamikia mwamuzi Victor Mwandike kwamba aliwabeba Yanga.
  “Nashangaa wanaomlaumu refa eti aliiumiza SImba, vipi kuhusu penalti zetu mbili za wazi alizokataa kutupa, vipi rafu za makusudi ambazo wachezaji wa Simba walikuwa wanawachezea wachezaji wangu.
  Haukuwa mchezo wa kiungwana waliocheza Simba dhidi yetu, yote haya hayakuonekana. Vipi kadi nyekundu aliyopewa Ben Mwalala, ilikuwa halali ile? Mwalala alifanya nini, alikuwa anatoka, Meshack akamfuata kumfanyia fujo, Mwalala aligeuka kujilinda, alitaka kujua Meshack anataka kumfanya nini.
  Lakini matokeo yake refa alitoa kadi kwa wote, je ni sawa hiyo? Tusiwe mashabiki kupita kiasi, tuzungumzie hali halisi, nasikitika hadi viongozi wa serikali wanasema ovyo,”anasema Kondic.


  USAJILI DIRISHA DOGO HAUJATULIA:
  Anazungumzia usajili wa dirisha dogo, ambao huanza Desemba nchini na kusema kwamba mpango huo haujatulia hata kidogo.
  Anasema TFF inapaswa kurudisha nyuma muda wa usajili kwa manufaa ya klabu ambazo zitaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika mwakani.
  “Ligi inamalizika Novemba mapema, kwa nini usajili upelekwa hadi Desemba? Ni mbali sana, angalau sisi (Yanga) na Prisons kwa sababu tunaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Afrika, tupewe ruhusa maalum ya kuanza usajili kabla ya Desemba,”anashauri.

  ANAWANYEMELEA WANIGERIA WA SIMBA?
  Kumekuwa na tetesi kwamba, Kondic anawamezea mate nyota wawili wa Simba kutoka Nigeria, Emeh Izuchukwu na Orji Obinna, lakini anaruka kimanga juu ya tuhuma hizo.
  “Nazifahamu taratibu na ninaziheshimu sana, siwezi kufanya hivyo, kama ninataka mchezaji Simba, nitasubiri muda wa usajili ufike nianze harakati. Msimu huu nilitaka wachezaji watatu Simba, Mussa (Hassan Mgosi) Henry (Joseph) na yule beki (Kelvin Yondani), lakini sikufanikiwa,”anasema.
  Kondic anasema alizungumza na wachezaji hao na kukubaliana nao, lakini alipokwenda kuwoamba kwa klabu yao, iligoma kuwauza hivyo mpango huo ukazimika naye akaachana nao.
  Je bado anawahitaji? “Siwezi kusema chochote kwa sasa, muda wa usajili ukifika nitajua kam,a ninawahitaji au la, ila hata Simba na wao walifanjya mazungumzo na wachezaji wetu.
  Walizungumza na Mrisho Ngassa, Shadrack Nsajigwa, hata mimi siwazuii Simba kuchukua wachezaji kwangu, kama wana hela waje kumchukua yoyote,”anasema.
  Kondic anasema kwamba kabla ya hapo, SImba iliwachukulia mchezaji wao mmoja, Edwin Mukenya na Yanga ilimruhusu kuondoka.

  VIPI OWINO, NURDIN NA KASEJA?
  Wakati anasema alizungumza na Henry, Mgosi na Yondani pekee ndani ya kikosi chake msimu huu kuna wachezaji watatu ambao msimu uliopita walikuwa Simba, kipa Juma Kaseja na mabeki Nurdin Bakari na Mkewnya George Owino, walifikaje?
  “Sijui chochote kuhusu Kaseja, nililetewa tu, nikampokea kwa sababu najua ni kipa mzuri, Nurdin Bakari alikuja kuomba mwenyewe, aliletwa kwangu na Credo Mwaipopo, nikaona kwa sababu namjua ni mchezaji mzuri, acha nimchukue,”anasema Kondic.
  Kuhusu Owino, Kondic anasema kwamba alikwenda Kenya kushuhudia mchezo kati ya timu ya taifa ya nchi hiyo, Harambee Stars na baada ya mechi alimfuata kumpongeza.
  “Alicheza vizuri, nikamuuliza vipi unabaki Simba? Akasema yeye ni mchezaji huru, ndio nikazungumza naye aje Yanga, akakubali,”anasema Kondic aliyezaliwa Aprili mwaka 1947 mjini Banatski Kariovac, Yugoslavia.

  YANGA ITAWIKA AFRIKA 2009?
  Baada ya kuifanya iwe tishio katika Ligi ya Bara, kiu ya wana Yanga ni kuona timu yao inawika Afrika, je Kondic ataweza kuikata?
  “Hakuna linaloshindikana, baada ya ligi nakwenda kupika timu yangu Afrika Kusini, nitaongeza wachezaji wawili watatu, mmojawapo ni mshambuliaji hatari sana, sitaki kuzungumza zaidi, tutakaporudi kwenye mzunguko wa pili, mtatuona,”anasema.
  Kondic aliiongoza Yanga kwa mzunguko wote wa pili wa Ligi Kuu Bara mnsimu uliopita na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Bara, wakati msimu huu hadi sasa ameiwezesha kushinda mechi tisa kati ya kumi, hivyo kuwa kileleni mwa Ligi Kuu ya Bara.
  Lakini kwenye michuano ya Afrika, bado hajaonyeasha makali kwani msimu huu timu hiyo ilitolewa Raundi ya Pili na Al-Akhdar ya Libya katika Kombe la Shirikisho la soka Afrika.
  “Wana Yanga wawe na subira, mambo mazuri hayataki haraka, nafanya kazi sana, nashukuru Manji anaunga mkono jitihada zangu zote, Manji ni mtu muhimu mno kwa Yanga, sasa hivi anaumwa, kwa kweli tunamuombea apone haraka na apate afya njema, ni mtu muhimu kwetu, muhimu kwa maendeleo ya Yanga,”anasema Kondic.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: Kondic: Bado kidogo tu niwasajili Mgosi, Yondani Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top