• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 22, 2009

  SIKU KONDIC ALIPOJISHUSHA KITAALUMA YANGA...  na mahmoud zubeiry

  KOCHA Hassan Shehata aliona timu yake inayvocheza na kugundua mapungufu yako wapi na anatakiwa kufanya nini, ili kuweka mambo sawa.
  Kwa sababu hiyo, Shehata hivyo aliamua kufanya mabadiliko, akimtoa mshambuliaji nyota na kipenzi cha Wamisri, Hossam Hassan ‘Mido’ na kumuingiza chipukizi Amri Zaki.
  Hiyo ilikuwa ni katika Nusu Fanali ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2006 (CHAN) mjini Cairo, Misri ikimenyana na Ivory Coast, wakati huo timu hizo zikiwa hazijafugana na dakikaka zimeyoyoma.
  Hata hivyo, wakati mwamuzi wa akiba amefika kwenye mstari wa uzio wa Uwanja na kuinua kibao kinachoonyesha jezi namba ya mchezaji anayetoa na anayeingia, Mido ambaye ndiye alikuwa anatolewa alihamaki na kuja juu akigoma kutoka.
  Kocha Shehata alisistiza kwamba ni Mido wa kutoka na Zaki ataingia kuitafutia ushindi Misri, jambo ambalo liliendelea kupingwa na mshambuliaji huyo anayecheza klabu ya…..
  Labda Mido alijiona yeye ni bora kuliko Zaki kwa sababu yeye anacheza Ulaya na mwenzake anacheza pale pale Misri, pengine alij0ona bora kuliko hata kocha wake, kwa sababu yeye anafundishwa na Wazungu Ulaya.
  Lakini mwisho wa yote, Mido alitoka uwanjani na kwenda kumtolea maneno machafu kocha wake, jambo ambalo kwa hakika liliwakera Wamisri wengi.
  Lakini kwa sababu Shehata alikwsihaona kwa nini timu yake haipati bao hata akaamua kufanya mabadiliko yale, alifanikiwa, kwani ni Zaki aliyekwenda kuwafungia Misri bao lililowapeleka fainali na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano hiyo baadaye.
  Chama cha Soka Misri kilimuadhibu Mido kwa kitendo chake na baadaye aliwajibika kuomba radhi kwa kocha, uongozi na mashabiki kwa upumbavu wake aliofanya mbele ya maelfu waliokuwa wakitazama mchezo huo na wengine waliokuwa wakiufuatilia kwa njia ya Televisheni.
  Kwa makocha wa Kiafrika ambao kwa kiasi kikubwa hudharauliwa na nyota wa Ulaya, tukio lile walilipokea kwa furaha mno, kwani walijua huo ni mwanzo wa wao kuheshimiwa na wachezaji wa Ulaya.
  Kwa Mido ilimvunjia heshima mno na kuonekana ni mchezaji fedhuli na limbukeni, kwani hata angekuwa hajaridhishwa na maamuzi ya kocha, hakupaswa kupingana naye hadharani, alikuwa ana nafasi ya kuzungumza naye taratibu baadaye.
  Huo ndio ukweli kwamba, mchezaji hawezi kuwa juu ya kocha, ambaye amepewa dhamana na chama cha nchi kuiongoza timu au uongozi wa klabu kuiongoza klabu husika.
  Ingawa ni kweli kwamba dunia ya leo kuna wachezaji wengi mafedhuli wanaojiona wapo juu ya makocha wao, kwa sababu tu pengine wanalipwa zaidi ya makocha wao, ama wanajiona wao ni bora zaidi ya makocha wao, lakini ukweli utabakia pale pale kocha ni zaidi ya mchezaji.
  Wachezaji wengi wamepita mikononi mwa Sir Alex Ferguson katika klabu ya Manchester United na walikuwa wana majina makubwa na maslahi pia kuliko mwalimu wao huyo, lakini leo wameondoka na kocha huyo ameendelea kuipa mataji klabu hiyo, likiwamo la dunia ililolitwaa mwishoni mwa mwaka.
  Kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 Korea na Japan, kivutio kikubwa kilikuwa kwenye kambi ya Brazil ambako kocha Luiz Filippe Scolari alikuwa analazimishwa kumjumuisha kwenye kikosi chake mshambuliaji mkongwe Romario.
  Lakini kocha alishikilia msimamo wake wa kubakia na wachezaji anaoona yeye wanafamfaa enzi hizo akiwastaajabisha wengi kwa kumchkua Ronaldo Lima aliyekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na Ronaldinho aliyekuwa anainukia.
  Lakini ni nyota hao waliokuwa chachu ya Brazil kutwaa ubingwa kwenye fainali hizo, hivyo kumjengea heshima kubwa kocha huyo ambaye kwa sasa anainoa Chelsea ya England.
  Wabrazil walikuwa wanamuamini Romario na waliona ni muhimu akawamo kikosini, lakini Scolari aliona wa kazi gani na akashilkia msimamo wake kiasi cha kuwa tayari kuachia ngazi iwapo ataendelea kushinikizwa ambebe mkongwe huyo.
  Nimeikumbuka hadithi ya Mido katika CAN ya 2006 na Romario Kombe la Dunia 2002, baada ya tukio la mechi ya mwisho ya Kundi A, Kombe la Tusker kati ya Mtibwa Sugar ya Morogoro iliyoibuka bingwa baadaye dhidi ya Yanga iliyovuliwa ubingwa mapema kwa kutolewa kwenye hatua ya makundi.
  Siku hiyo kocha wa Yanga Dusan Kondic wakati timu yake ikiwa nyuma kwa 1-0, aliamua kumuinua chipukizi Ally Msigwa kuingia uwanjani kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.
  Lakini wakati akiwa kwenye harakati hizo, wachezaji kadhaa wa Yanga wakiongozwa na George Owino walimfuata kocha wao na kumpinga juu ya mabadiliko hayo, kwamba Msigwa asiingie bali aingie mchezaji mwingine wanayemtaka wao, Vincent Barnabas.
  Inasikitisha kuona kwamba kocha wa Yanga, anayejiita Profesa, Dusan Kondic alijishushia hadhi nyake mno siku hiyo baada ya kutulizwa na mkwara wa wachezaji wake na kumrudisha benchi Msigwa na kumuingiza mchezaji chaguo la wachezaji.
  Barnabas aliingia na kucheza hadi filimbi ya mwisho, lakini hakuweza kubadilisa chochote katika mchezo huo na Yanga ilibaki kucheza vile vile, ovyo na hatimaye kulala 1-0.
  Moja kwa moja Yanga ilifungwa kwa sababu ya ujuaji wa wachezaji walio juu ya kocha, ambaye hana maamuzi ndani ya timu. Hii inamshawishi mtu kuamini kwamba, hata vikosi vinavyopangwa Yanga kila mechi, havitokani na kocha, bali matakwa ya wachezaji.
  Sasa huyu Profesa ana faida gani katika timu ikiwa kazi inafanywa na wachezaji wenyewe?
  Profesa wa Kiserbia mwenye maskani yake Afrika Kusini analipiwa malazi katika hoteli ya kitalii, New Africa, inasemekana mshahara wake si chini ya dola za Kimarekani 7000 kwa mwezi (zaidi ya Sh. Milioni 8 za Kitanzania) ana faida gani?
  Kocha anayekubali kutawaliwa na wachezaji ni yule asiyejiamini pekee, lakini mwalimu yeyote mwenye kujiamini, kama Scolari na Shehata daima hawezi kukubali kuyumbishwi na mchezaji wake.
  Alichokifanya Kondic kwenye mechi dhidi ya Mtibwa, ni sawa na kuonyesha kwamba kiasi gani anashikiwa akili na wachezaji wake na huo unaweza ukawa mwanzo wa kusababisha matatizo makubwa zaidi ndani ya timu.
  Kwani wachezaji wengine wanaweza wakajiona nafasi yao ni ndogo mno japokuwa kisoka wana uwezo mkubwa, kwani tayari kocha amekwishaonyesha kuzidiwa nguvu na wachezaji fulani.
  Hakika ni udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na kocha wa Yanga na hii pekee inaweza ikawa sifa tosha ya uongozi kumuwajibisha mwalimu wa aina hii.
  Mfumo wa utawala bora unaelekeza kwamba, kila mtu anawajibika kwa bosi wake, ingawa ndani ya mfumo huo kidemokrasia kushauriana katika misingi ya kitaalauma inaruhusiwa, hivyo basi Kondic anapaswa kujua kwamba yeye ni bosi wa wachezaji.
  Wachezaji wana nafasi ya kushauriana na kocha, katika tukio kama la Yanga na Mtibwa, walioona mwalimu amekosea kwa sababu naye si malaika, walipaswa kumuita Nahodha wao na kumuambia, ambaye ndiye angekwenda kumuita kocha na kuzungumza naye, hatimaye wakafikia mwafaka.
  Lakini ni walichokifanywa wamemgharimu mno kocha wao, kwani heshima yake mbele ya wataalamu wa soka nchini imepungua kwa kiasi kikubwa mno, tena hata mbele ya mashabiki wenye upeo mkubwa.
  Kondic anapaswa kufahamu kwamba yeye anawajibika kwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu yake, ambaye kwa sababu hayupo, anajikuta anawajibika moja kwa moja uongozi wa Yanga.
  Kwa sababu hiyo Mserbia huyo amewaonyesha njia viongozi wa Yanga kwamba wanapaswa kufanya nini dhidi yake kuelekea kwenye mchakato wa kutengeneza timu imara, yenye nidhamu itakayofanya vizuri kwenye michuano ya Afrika.
  Yanga inahitaji kocha atakayesimamia nidhamu ndani ya timu, kujenga umoja na mshikamano kwa wachezaji, kukuza viwango vya wachezaji na kuiwezesha timu kucheza kandanda safi yenye kuzaa ushindi na kuwapa burudani mashabiki wake.
  Je, Kondic ana sifa hizo? Hilo ni swali ambalo viongozi wa Yanga wanapaswa kujiuliza kwa kurejea utendaji wa mwalimu huyo na jinsi timu yao ilivyo.
  Kuna kauli moja ambayo Mbrazil Marcio Maximo hupenda kuitumia kabla ya mechi za timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya timu timu yoyote; kwamba yeye hawezi kuahidi ushindi, bali anaahidi soka safi.
  Kweli, ukienda kutazama mechi ya Taifa Stars utaona soka safi ambayo huazaa mabao, ushindi na kuwapa burudani mashabiki wa soka nchini.
  Wakati yote hayo yanatokea chini ya Maximo, kikosi cha Stars kinakuwa kinaundwa na aslimia kubwa ya wachezaji wa Yanga, ambao wakiwa kwenye klabu hiyo hawafanyi vitu vile ambavyo wanafanya timu ya taifa.
  Sasa hapo tatizo ni nini, Jerry Tegete awe mfungaji tegemeo wa Stars, lakini ashindwe kuifungia Yanga, Kiggi Makasi ang’are timu ya taifa, lakini asing’are kwenye klabu yake!
  Kondic anataka kuwa mtu wa kusajili kila kipindi kinapowadia wakati wachezaji wengine alionao kikosini ni bora na hawatumii ipasavyo, je huo ndio ukocha wa dunia ya ngapi?
  Kondic alitaka kuwasjili Wakenya Joseph Shikokoti kwa ajili ya beki ya kati, wakati tayari kwenye nafasi hiyo kuna George Owino, Hamisi Yussuf na Wisdom Ndhlovu, je anataka kulundik mabeki wote hao wa nini?
  Ameshindwa kuboresha viwango vya nyota wengine, ambao chini ya makocha waliomtangulia walikuwa lulu kwenye klabu hiyo.
  Hamisi Yussuf ambaye uwezo wake umeshuka hivi sasa kutokana na kutupwa benchi muda mrefu, ndiye aliyekuwa sentahafu tegemeo wa Yanga chini ya Milutin Sredojevic ‘Micho’ hata Jack Chamangwana, kiasi cha kupachikwa jina la Waziri wa Ulinzi.
  Alitaka kumsajili John Njoroge wa Kenya pia kucheza beki ya kushoto, wakati tayari kwenye nafasi hiyo ana Abuu Mtiro, Amir Maftah na Nurdin Bakari, wakati huo huo hata Ndhlovu anaimudu nafasi hiyo, kwani hata timu yake ya taifa ya Malawi hucheza namba hiyo.
  Amemleta Mike Barasa kuimarisha safu ya ushambuliaji wakati tayari ana wasambuliaji alioshindwa kuwatumia vyema kama Tegete, Gaudence Mwaikimba na Iddi Mbaga. Unaweza kukata tama juu ya Mwaikimba, lakini si Mbaga na Tegete, wachezaji hao wakipata mwalimu wa ‘ukweli’ wanaweza kutengeneza safu kali ya ushambuliaji ndani ya Yanga.
  Lakini kwa sababu Yanga haina Mkurugenzi wa Ufundi, hakuna wa kuhoji sawasawa masuala haya kwa kocha, amekuwa akiwazima kwa visingizio kibao, zaidi akimsukumia lawama Maximo kwamba anamharibia programu zake.
  Kondic anasahau kwamba alikwenda kuiweka Yanga kambini Afrika Kusini mwaka jana na iliporejea ikaboronga kwenye Kombe la Mapinduzi, je huko nako aliingiliwa na Maximo?
  Huyu ndiye mwalimu anayejinasibu ataipa Yanga ubingwa wa Afrika, kama ndio huyu wa namna hii, Yanga waendelee kusubiri ubingwa wa Afrika kutoka kwa Profesa wao wa Kiserbia
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIKU KONDIC ALIPOJISHUSHA KITAALUMA YANGA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top