• HABARI MPYA

  Saturday, January 24, 2009

  NDIKUMANA WA SIMBA AULA UBELGIJI


  MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Suleiman Yamin Ndikumana (PICHANI KUSHOTO)amenunuliwa na klabu ya daraja Pili nchini Ubelgiji, Lierse S.K. kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu, akitokea klabu ya Molde FK ya Ligi Kuu ya Norway.
  Mchezaji huyo aliuzwa kwenye klabu ya Molde FK na wakala wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kutoka Tanzania, Mehdi Rehmtullah baada ya kung’ara kwenye michuano ya Kombe la Challenge iliyofanyika Dar es Salaam, Desemba mwaka juzi.
  “Ndikumana yupo katika klabu hii ya Ubelgiji, alisaini mkataba tangu Desemba 8 mwaka jana,”kilisema chanzo chetu cha habari kutoka Ubelgiji.
  Mshambulaji huyo aliyeikimbia Simba na kurejea kwao Burundi mwaka 2006 baada ya kuichezea kwa mwaka mmoja, alikwenda Norway Januari mwaka jana baada ya Challenge sambamba na kiungo Uhuru Suleiman Mwambungu, ambaye hata hivyo alifeli na kurejea nyumbani.
  Kwa mujibu wa Mehdi, Uhuru alirejeshwa kwa sababu hana nguvu za kutosha ingawa kipaji chake kiliivutia Molde FK, hivyo alipewa muda wa kufanya mazoezi ya kujenga mwili, japokuwa hadi sasa bado ‘anaota jua la Bongo’.
  Ndikumana anafanya orodha ya wachezaji wa Burundi wanaocheza Ubelgiji kufika watano, baada ya beki David Habarugira wa R.S.C. Anderlecht, viungo Dugary Ndabashinze wa KRC Genk, Emmanuel Ngama wa FC Dender na mshambuliaji Christian Nduwimana wa Herk F.C.
  Wachezaji wengine wanaocheza Ulaya wa Burundi ni mshambuliaji Kassim Bizimana wa BV Veendam ya Uholanzi, kipa Janvier Ndikumana wa Randaberg IL ya Norway, kiungo Faty Papy Trabzonspor ya Uturuki wakati beki Valery Nahayo anachezea Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDIKUMANA WA SIMBA AULA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top