• HABARI MPYA

    Saturday, January 24, 2009

    TFF INAPOLEA MADUDU, SOKA ITAENDELEA KWELI?

    Rais wa TFF, Leodegar Chilla Tenga


    na mahmoud zubeiry
    MAPEMA kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, inayodhaminiwa na kampuni ya Vodacom kwa pamoja na GTV, Agosti mwaka jana, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa marekebisho ya kanuni zake yaliyolenga kuboresha ligi hiyo.
    Japokuwa marekebisho hayo bado yalikuwa na dosari chache, ikiwamo kuruhusu klabu kusajili wachezaji 10 wa kigeni, kutoka watano, lakini haidhuru ilikuwa na vipengele vingine vyenye mwelekeo mzuri katika kuipeleka kwenye sayari nyingine kandanda ya nchi hii.
    Dhahiri ulikuwa ni mwanzo wa mapinduzi katika soka ya Tanzania, katika kuelekea kuwa na Ligi ya nidhamu, msisimko, ushindani na msingi wa uzalishaji na ukuzaji wa vipaji.
    Moja ya kanuni ambazo zilipokewa kwa shangwe na wapenda maendeleo ya soka Tanzania ni ya 62, inayozungumzia klabu zote za Ligi Kuu kuwa na vikosi vya timu za watoto na vijana.
    Kanuni hiyo inasema: “ 1. Kila Kilabu kinatakiwa kuunda na kudumisha timu za pili au za watoto ikiwa ni Sharti la kushiriki Ligi na kwa manufaa ya Kilabu na kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla. Endapo Kilabu itashindwa kutimiza sharti hili itaondolewa katika Ligi na kushushwa daraja.
    2. Kila Kilabu kitaruhusiwa kusajili wachezaji wa timu za watoto wasiyopungua 18 na wasiyozidi 25 wenye umri usiyozidi miaka 20.
    3. Kilabu zinatakiwa ziwe zimekamilisha usajili wa timu za watoto ifikapo tarehe 15/8/2008.
    4. Wachezaji wa timu za watoto wanaweza kutumika katika mashindano ya Ligi Kuu.
    5. Usajili na uhamisho wa timu za watoto utazingatia kanuni za Ligi Kuu.
    6. Waraka maalumu utatolewa kuhusiana na usajili wa wachezaji wa timu za watoto ambao utasomeka pamoja na kanuni hizi.”
    TFF ilikuwa chungu katika kuhakikisha kila klabu inasajili kwanza kikosi cha pili kwa mujibu wa maelekeo ya kanuni, ndipo ipate haki ya kushiriki Ligi Kuu ya Bara.
    Lilikuwa ni jambo lenye kutia faraja kwamba, klabu zote zilikidhi matakwa hayo na kilichofuata ni Ligi Kuu inayokwenda sambamba na Ligi ya vijana, ambayo hata hivyo, siku chache tu baadaye iliyumba na kupoteza mwelekeo.
    Klabu hazikuweza kusafiri na vikosi vya pili kwenda kwenye mechi za mikoani, jambo ambalo lilifanya Ligi hiyo iwe kichekesho kitupu. Wakati mwingine, Simba inacheza na Kagera Sugar ya Bukoba, lakini timu za vijana zinazomenyana ni Villa Squad na Simba.
    Sababu kubwa iliyokuwa ikielezwa na klabu kushindwa kusafirisha timu mikoani ni ukosefu wa fedha na kwa kuwa TFF ilishindwa kuzibana klabu katika hilo, hali ilibakia kuwa hivyo.
    TFF ilishindwa kuelewa kwamba, wapuuzi wana mbinu nyingi za kuwapumbaza watu, ili mradi wafanikishe azma yao ya kupuuza jambo na hivi ndivyo ilivyoonekana kufanywa na klabu nyingi katika hilo.
    Kweli kuna baadhi ya klabu ambazo unaweza kuzielewa katika hilo la kutokuwa na fedha za kusafirisha timu mikoani, haswa mikoa ya mbali kama Mbeya, Mwanza na Kagera, lakini kwa nyingine hakika ilikuwa ni hila za kukwamisha mpango huu.
    Baada ya TFF kulainika katika hilo na kufanya sasa Ligi ya vijana iwe ya hivyo hivyo tu, kwa timu zinapocheza nyumbani ndio ziingize timu zao uwanjani, hatimaye sasa wapuuzi hao wamepiga hatua nyingine kubwa mbele.
    Ni kwamba, hivi sasa hata kwenye mechi zao za nyumbani kuna baadhi ya klabu haziingizi timu zao za vijana kucheza.
    Mfano katika mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu, ilisikitisha kuona kwamba mabingwa hao watetezi hawakuingiza timu yao ya vijana. Siku hiyo, ilicheza Polisi Morogoro na Azam.
    Kwa Yanga ni kwamba, habari zilizopo timu hiyo imekwishakufa, kwani aliyekuwa kocha wake, Waziri Mahadhi aliamua kuachana nayo baada ya kuwa halipwi posho wala mshahara na sasa yuko Oman anafanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Seeb kama mchezaji.
    Jack Chamangwana aliyekuwa akiinoa timu hiyo kabla, sasa amerejea kwao Malawi ambako amepewa kazi na chama cha soka cha nchi yake, kama Mkurugenzi wa Ufundi.
    Kocha mwingine, Yvojnov Seran aliyeletwa na mfadhili wa timu hiyo, Yussuf Manji kutoka Serbia, hivi sasa naye ameungana na Waserbia wenzake, Dusan Kondic na Spaso Sokolovski katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
    Kwa sababu hiyo, kinachojitokeza hapa ni udhaifu unaoanzia ndani ya TFF, kwamba inajiwekea kanuni yenyewe, lakini inashindwa kusimamia na kutilia mkazo utekelezaji wake, matokeo yake ndio haya.
    Kimsingi mashindano ya vijana yalianzishwa mwaka 1977 (chini ya umri wa miaka 20, yakifuatiwa na chini ya umri wa miaka 17, mwaka 1985) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa lengo kubwa la kuwaandaa nyota wa baadaye katika utaratibu ulio mzuri na ndio maana dunia ya leo vijana wadogo kuanzia umri wa miaka 16 wananunuliwa kwa bei chafu na klabu za Ulaya.
    Kwa Tanzania ambayo inapigana kuhakikisha inakuwa na nyota wanaocheza soka Ulaya, haina budi kutilia mkazo soka ya vijana kwa kuhakikisha watoto wanashindanishwa ili kukomaa kisoka.
    Nchi nyingi duniani zina ligi za ushindani za vijana, ambazo zimekuwa chimbuko la kuibua nyota wanaokwenda kucheza mashindano ya kimataifa ya vijana.
    Kisingizio cha eti tusijilinganishe kiuchumi na nchi nyingine ni kikwazo cha utekelezaji wa sera za maendeleo, ambacho hakika TFF kama itaendelea kukipa uzito, basi zoezi la kuinua mchezo huu Tanzania litakuwa sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.
    Kama huo ni utaratibu ambao TFF imeuweka, haina budi kuushikia bango ufuatwe, utekelezwe na asiyeweza kuufuata, basi hakidhi sifa za kushiriki Ligi Kuu na kwa nini asiondolewe?
    Hata wazee wetu walituachia urithi wa neno; Samaki Mkunje Angali Mbichi, hivyo hata kwenye soka ni vyema vijana wakafundwa kiukamilifu wangali wadogo ili kuwaepushia kero wataalamu baadaye, kuwakabidhi watu ambao wamekwisha komaa na hawafundishiki.
    Ndio, kwani hizo ndio kauli za makocha wengi wanaokuja nchini kufundisha klabu mbalimbali, husema wazi kwamba wachezaji wa nchi hii hawafundishiki. Sasa atafundishika vipi mtu tayari ana miaka zaidi ya 27?
    TFF inapaswa kuelewa kwamba, inaposhindwa kusimamia utekelezaji wa kanuni zake ni sawa na kulea matatizo, ambayo yanapokomaa yanakuwa kero kubwa.
    Ni TFF iliyozoea kuzidekeza Simba na Yanga, kiasi kwamba zinajiona zenyewe ndio kila kitu katika soka ya nchi hii, wakati huo si ukweli, siku zote mtoto hawezi kuwa zaidi ya baba, hiyo itakuwa ni sawa sikio kuzidi ukubwa wa kichwa.
    Ni kwa sababu ya kudekezwa zinafikia hatua ya kufanya uamuzi wenye kuutia aibu mchezo wa soka nchini kama kugoma kuingiza timu uwanjani kwa sababu zisizo na msingi.
    Ukweli ni kwamba kama ambavyo inaelezwa kwenye kanuni ya 63 kwamba TFF inawajibika kutafuta wadhamini wa Ligi Kuu na ikiwa ligi ya vijana ni sehemu ya ligi hiyo, shirikisho hilo linapaswa pia kupigana kuhakikisha anaptikana mdhamini wa ligi hiyo.
    Lakini huo udhamini hauwezi kusubiriwa upatikane kwanza ndipo ligi ya vijana wa klabu za Ligi ianze rasmi, la hasha, TFF inapaswa kuendesha ligi yake hiyo ya ushindani kama kawaida na hao wadhamini watakuja badaaye.
    Kwani hata Ligi Kuu ya Bara haikusubiri wadhamini ili kuanza, hata michuano ya Kombe la Taifa, haikusubiri wadhamini ndio ianze. Kwa sababu hata mdhamini anawekeza fedha zake sehemu ambayo amekwishaona ladha yake.
    Ni kwa hoja hiyo nasisitiza kwamba, kisingizio cha klabu kutoweza kusafiri kwa sababu ya fedha hakina maana, bali ni kikwazo cha sera za maendeleo. Na zaidi klabu zimekuwa zikifanya upuuzi huu, kutokana na udhaifu ambao dhahiri unaanzia TFF.
    Kwa mfano, azimio la Bagamoyo mwaka juzi lilizaa kanuni safi ya Ligi Kuu, kwamba ili klabu ishiriki ligi hiyo ilipaswa kwanza kukamilisha Katiba mpya kulingana na maelekezo ya azimio hilo.
    Ni katiba inayoelekeza klabu kujiendesha kisasa, jambo ambalo mbali na kuepuka migogoro kwenye klabu pia inatoa mwongozo wa maendeleo. Lakini baada ya klabu kushurtishwa zikamilishe katiba mpya ili zishiriki ligi hiyo, TFF inaona kama imemaliza kazi, suala la utekelezaji wake haliwahusu tena wao.
    Hii unaweza kuifananisha na wapenzi wapya wanapokutana mwanzoni wanahimizana kutumia kondomu, lakini baadaye hata kabla hawajapima wanaiweka kando, eti wamekwishazoeana, kwani kipimo cha ukimwi ni wapenzi kuzoeana?
    Hivyo hivyo, TFF inapaswa kujiuliza kama Katiba mpya zimetengenezwa lakini hazifuatwi, kama timu za vijana zimesajiliwa lakini hazichezi mashindano kuna faida gani? Alamsiki, hadi wiki ijayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF INAPOLEA MADUDU, SOKA ITAENDELEA KWELI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top