• HABARI MPYA

    Friday, January 23, 2009

    UDHAMINI WA KILIMANJARO: Simba sasa mambo poa

    Makamu Mwenyekiti wa Simba, Omar Gumbo akimuonyesha kocha wa Simba, Patrick Phiri jezi za wadhamini wao, Kilimanjaro.



    TANGU kumpoteza mdhamini wake aliyewatoa gizani, Mohamed Enterprises Limited (MeTL), klabu kongwe ya soka nchini, Simba imekuwa ikisota kupata wadhamini wengine.
    Imejaribu bila mafanikio kupata mdhamini mwingine, jambo ambalo kwa hakika liliiweka klabu hiyo kwenye wakati mgumu.
    Simba ilijikuta inapoteza hadi baadhi ya wachezaji wake vipenzi, walioamua kuhamia klabu nyingine kufuata maslahi.
    Lakini kilio cha Simba, sasa kimepata jibu, baada ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake maarufu, Kilimanjaro Premium Lager kujitokeza kuipa udhamini mnono klabu hiyo, inayoitumia jezi za rangi ya nyekundu na nyeupe.
    Mkataba huo, wenye thamani ya Sh. Bilioni 3, utakaodumu kwa miaka mitatu, ikiwa kila mwaka Kilimanjaro itakuwa ikitoa Sh. Bilioni 1, kwa klabu hiyo kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa timu.
    Mapema tu wakati wa hafla ya uzinduzi wa mkataba huo, iliyofanyika Agosti 18, mwaka 2008 kwenye hoteli ya Movenpick, mjini Dar es Salasam, Kilimanjaro Premium Lager ilitoa hundi ya sh. 25,000,000 kwa klabu hiyo, ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji wake.
    Kilimanjaro Premium Lager, pia imetoa udhamini kama huo kwa klabu ya Yanga.
    Akitoa mchanganuo wa mkataba huo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Oscar Shelukindo alisema kwamba klabu hiyo itavuna sh. Milioni 16, kila mwezi kwa ajili ya mishahara ya wachezaji, hiyo ikiwa ni mbali na kupatiwa basi dogo la kusafiria wachezaji.
    Shelukindo alisema kwamba, Kilimanjaro Premium Lager maarufu kwa jina la ufupi kama Kili, imeamua kuzisaidia klabu hiyo, kwa sababu ina mwelekeo wa kweli wa kuendeleza soka ya Tanzania.
    Aidha, Kili pia itatoa zawadi kwa timu hiyo iwapo itafanikiwa kushika moja ya nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikiwa bingwa itapata Sh. Milioni 25 na ikishika nafasi ya pili, itapewa Sh. Milioni 15.
    “Tunaamini kwa kufanya hivi, tutaiongezea morali klabu hii, italeta ushindani wa kweli kwenye ligi, kwa sababu mkataba huu unawanufaisha wachezaji moja kwa moja, watapata mishahara na posho kwa wakati mwafaka,”alisema Shelukindo.
    Alisema Simba pia inayojulikana kwa majina ya utani kama Wekundu wa Msimbazi, Mnyama na Taifa Kubwa, itapewa vifaa vya thamani na vya kisasa vya michezo, lengo likiwa ni kuifanya iwe bora na mfano wa kuigwa katika ligi hiyo.
    Akizungumzia udhamini huo, Mwenyekiti wa klabu ya Simba, ‘Filed Marshal’ Hassan Dalali, alisema kwamba anashukuru kwa Kilimanjaro Premium Lager kujitolea kuwasaidia, kwani hiyo itawawezesha kuwa imara zaidi hivi sasa.
    Unapozungumzia Simba, unamaanisha klabu kubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, ambayo ilianzishwa mwaka 1936, enzi hizo ikijulikana kwa jina la Queens.
    Baadaye Simba ilibadilisha jina na kuwa Eagles, kabla ya kuanza kutumia jina lingine, Sunderland ambalo lilidumu hadi mwaka 1971 lilipobadilishwa na kuwa Simba.
    Sababu ya kuachana na jina la Sunderland ni aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume, ambaye wakati anaweka jiwe la Msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la klabu hiyo, liliopo Mtaa wa Msimbazi, mwaka huo 1971.
    Rais Karume, aliwaambia Simba waachane na majina ya kizungu na watumie jina la asili ya Afrika na ndipo jina la Mnyama tishio zaidi porini, Mfalme wa Nyika, Simba lilipowavutia hata ukawa mwanzo wa Simba SC.
    Ikiwa inaitwa Sunderland, iliweza kutwaa ubingwa wa Tanzania mara mbili tu, ikiweka rekodi ya kuwa klabu bingwa ya kwanza nchini mwaka 1965 na kuutetea mwaka 1966 na baada ya hapo haikuutia tena mikononi hadi ilipobadilisha jina na Simba, ndipo ilipourejesha mwaka1972.
    Simba ilifanikiwa kutetea taji lake mwaka 1973, ingawa ililipoteza kwa watani wao wa jadi, Yanga mwaka uliofuata kwa kipigo cha mabao 2-1 katika fainali ya kihistoria iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
    Adamu Sabu (sasa marehemu) aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Saad Ali, aliifungia Simba bao la kuongoza kabla ya Sunday Manara kuisawazishia Yanga na Gibson Sembuli (sasa marehemu pia) kufunga la ushindi kwa Watoto wa Jangwani.
    Ubingwa wa Tanzania mwaka 1975 kwa mara ya kwanza ulikwenda nje ya Dar es Salaam, ukichukuliwa na Mseto ya Morogoro iliyokuwa ikinolewa na kocha maarufu, Mohamed Msomali.
    Simba iliurejesha ubingwa wake mwaka mwaka1976 na kutetea kwa miaka minne mfululizo, 1977, 1978, 1979 na 1980. baada ya hapo, Simba iliyumba na kupoteza makali kabla ya kuibuka mwaka 1993 na kutwaa tena ubingwa huo. Iliutetea mwaka 1994 na 1995. iliutwaa tena katika miaka ya 2001, 2002, 2004 na 2007.
    Ukiachana na utawala wa Simba katika soka ya Tanzania, kwenye medani ya kimataifa klabu hiyo ndio inayoongoza kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
    Simba ndio klabu pekee iliyoweza kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika, mwaka 1974 ikiitoa timu ngumu ya Ghana katika Robo Fainali, Hearts Of Oak kwa jumla ya mabao 2-0.
    Yalikuwa ni mabao ya Sabu na Abdallah ‘King’ Kibadeni, Wakenya wakimuita Ndululu kutokana na ufupi wake, mjini Accra yaliyoipa timu hiyo ushindi wa 2-0, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Dar es Salaam.
    Hata hivyo, baada ya kushinda 1-0 mjini Dar es Salaam dhidi ya Mehala El Kubra, Simba ilikwenda kufungwa pia 1-0 na Waarabu hao mjini Cairo, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako Wekundu wa Msimbazi waling’olewa.
    Simba pia ni klabu pekee ya Tanzania, iliyoweza kucheza fainali ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Hiyo ilikuwa ni mwaka 1993, ilipofanikiwa kutinga fainali ya Kombe la CAF, (sasa limeunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho) na kufungwa na Stella ya mjini Abidjan, Ivory Coast.
    Bahati haikuwa yao Wekundu wa Msimbazi, kwani baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana ugenini, wengi waliamini kwenye mechi ya marudiano, Stella hawatapona Dar es Salaam, lakini matokeo yake, wenyeji walilala 2-0 kwa mabao ya Boli Zozo.
    Klabu hiyo pia ilifanikiwa kuwa klabu ya pili Tanzania kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, baada ya Yanga kuwa ya kwanza mwaka 1998. Lakini Simba ilitinga hatua kiume zaidi, ikiwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri, kwa mikwaju ya penalti.
    Hiyo ilifuatia ushindi wa 1-0 mjini Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 1-0 na yenyewe pia Cairo, lakini mchezo ulipohamia kwenye mikwaju ya penalti, Juma Kaseja, mtaalamu wa kuokoa michomo hiyo, aliibeba Simba baada ya kucheza penalti mbili.
    Aidha, Simba pia ndio klabu iliyoweza kutwaa mara nyingi zaidi Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002.
    Katika michuano mingine midogo ya Afrika Mashariki, Kombe la Tusker, Simba tena ndio timu iliyotwaa mara nyingi zaidi taji hilo, mara nne kati ya michuano sita ya Kombe hilo, katika miaka ya 2001, 2002, 2003 na 2005. ilikosa 2006 lilipochukuliwa na Kagera Sugar na mwaka 2007 lilipochukuliwa na Yanga.
    Naam, hao ndio Simba SC, Wekundu wa Msimbazi wanaokuja na nguvu mpya ya Kilimanjaro Premium Lager.

    REKODI ZA SIMBA:
    UBINGWA WA LIGI KUU:
    Imechukua mara 16 katika miaka ya 1965, 1966, 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2004 na 2007 (Ligi Ndogo)
    LILILOKUWA KOMBE LA NYERERE:
    1984, 1995 na 2000
    KOMBE LA TUSKER:
    2001, 2002, 2003 na 2005
    KOMBE LA CAF:
    Ilifika fainali mwaka 1993
    KOMBE LA KAGAME:
    1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002


    KIKOSI CHA SIMBA 2008:
    MAKIPA:
    Amani Simba
    Deo Bonaventure
    Ally Mustafa

    MABEKI:
    Salum Kanoni
    Anthony Matangalu
    Juma Jabu
    David Naftali
    Meshack Abel
    Victor Costa
    Kelvin Yondan
    Ramadhan Wasso

    VIUNGO:
    Henry Joseph
    Nico Nyagawa (Nahodha)
    Juma Said Nyoso
    Ramadhani Chombo
    Edwin Mukenya (Kenya) (amefukuzwa)
    Nassoro Masoud
    Mohamed Banka
    Ulimboka Mwakingwe
    Mussa Hassan Mgosi
    Jabir Aziz
    Adam Kingwande

    WASHAMBULIAJI:
    Emmanuel Gabriel (ameuzwa)
    Mohamed Kijuso
    Haruna Moshi
    George Nyanda
    Emeh Izichukwu (Nigeria)
    Orji Obinna (Nigeria)
    Moses Mwazembe
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UDHAMINI WA KILIMANJARO: Simba sasa mambo poa Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top