• HABARI MPYA

  Thursday, January 29, 2009

  DIMBA, BINGWA WADHAMINI ONYESHO LA LADY IN RED

  Hawa Ismail, mmoja wa wanamitindo maarufu wa Kitanzania,
  anayeishi Afrika Kusini kwa sasa, je atakuwepo kwenye Lady in Red?

  KAMPUNI ya New Habari (2006) Limited imedhamini onyesho la mavazi la Lady in Red litakalofanyika Februari 6, mwaka huu kwenye hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, Dar es Salaam.
  Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Burudani cha New Habari, Petter Mwendapole alisema jana mjini Dar es Salaam kwamba wameamua kudhamini onyesho hilo ili kutoa mchango kwa wasanii wa Tanzania.
  “Tumedhamini onyesho hili kupitia magazeti yetu mawili ya michezo Bingwa na Dimba ambapo mbali ya kutoa matangazo lakini pia tutasaidia katika kuhakikisha kazi za wabunifu na wanamitindo watakaoshiriki kwenye onyesho hilo zinatangazwa na kufahamika vyema,” alisema.
  Onyesho la Lady in Red linaandaliwa na mbunifu mkongwe Asia Idarous kupitia kampuni yake ya Fabark Fashion.
  Katika onyesho hilo wabunifu 11 wa Tanzania wanatarajia kuonyesha nguo zao ambapo kila mmoja anatarajia kuonyesha nguo tatu tatu.
  Mwendapole alisema hii si mara ya kwanza kwa New Habari kudhamini onyesho la namna hii kwani hivi karibuni pia ilidhamini shindano la Malkia wa Ngwasuma kwa kushirikiana na kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
  “Lengo letu ni kuwasaidia wasanii na makundi mengine katika jamii…pamoja na kutoa Habari lakini kuna muda ambao inabidi pia kurudisha shukrani kwa jamii na watu wengine ambao tunashirikiana nao,” alisema.
  Mbali na New Habari wadhamini wengine ni pamoja na kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, kinywaji cha Redd’s, kituo cha televisheni cha Channel Ten, DTV, Clouds FM, Magic FM, TBC1.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: DIMBA, BINGWA WADHAMINI ONYESHO LA LADY IN RED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top