• HABARI MPYA

  Tuesday, January 27, 2009

  NGASSA AIPAISHA YANGA LIGI KUU

  Mrisho Ngassa mfungaji wa bao pekee la Yanga

  BAO pekee la Mrisho Khalfan Ngassa, leo Jumanne limeiwezesaha Yanga kuzidi kuusogelea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuilaza Mtibwa Sugar 1-0, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ngassa alifunga bao dakika ya nane tu ya mchezo, kwa shuti kali kwa guu lake la kulia, baada ya kupokea pasi ya Mkenya, Ben Mwalala na kumchambua kipa Shaaban Kado wa Mtibwa, aliyepishana na mpira ukiingia nyavuni wakati akitoka kuuwahi.
  Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 39 na sasa inasubiri ushindi katika mechi tatu tu zijazo, ili kutangaza rasmi ubingwa, kwani itatimiza pointi 48, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.
  Simba, inaweza kutimiza pointi 47 iwapo tu itashinda mechi zake zote kuanzia leo, wakati Kagera inaweza kumaliza na pointi 47, Mtibwa 45 na Toto Afrika ya Mwanza 44 sawa na JKT.
  Yanga itashuka tena dimbani Februari 4, kumenyana na Moro United, Machi 19 dhidi ya Polisi Morogoro, zote zikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kama itashinda mechi zote hizo, basi ikishinda dhidi ya Toto pia mjini Mwanza, Machi 24, itakuwa imejitwalia rasmi ubingwa kabla ya sikukuu ya Pasaka.
  Katika mchezo huo, pamoja na ushindi huo, Yanga ilikosa mabao kadhaa ya wazi, likiwamo lile la nyota wa mabao Ligi Kuu, Boniphace Ambani, ambaye tangu kuanza kwa mzunguko wa pili hajafunga bao, licha ya kucheza mechi zote tatu.
  Mwamuzi Methew Akrama wa Mwanza, aliwapa kadi za njano wachezaji wawili wa Mtibwa, Abdallah Juma aliyeunawa mpira kwa makusudi na Salum Ussi, aliyemchezea rafu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga.
  Baada ya mechi hiyo, kocha wa Yanga, Profesa Dusan Kondic kutoka Serbia, aligoma kuzungumzia mchezo huo, akidai kukerwa na uchezeshaji mbovu wa Akrama, lakini Salum Mayanga wa Mtibwa, alikiri kuzidiwa ujuzi na mabingwa hao watetezi.
  Watani wa jadi wa Yanga, Simba kama watateleza mbele ye Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, watakuwa wameipunguzia safari ya kutwaa ubingwa, kutoka mechi tatu hadi mbili.
  Yanga: Obren Curkovic, Nsajigwa Shadrack, Nurdin Bakari, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Wisdom Ndhlovu (Malawi), Geoffrey Boniface, Mrisho Ngassa, Athumani Iddi/Mike Barasa, Ben Mwalala (Kenya)/Abdi Kassim, Boniphace Ambani (Kenya)/Amir Maftah na Shamte Ally.
  Mtibwa: Shaaban Kado, Mecky Mexime, Idrisa Rajabu, Chacha Marwa, Salum Sued, Shaaban Nditi, Zahoro Pazi/Zahoro Pazi, Rashid Gumbo, Abdallah Juma/Salum Ussi, Uhuru Suleiman na David Mwantobe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA AIPAISHA YANGA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top