• HABARI MPYA

  Jumamosi, Januari 24, 2009

  TWANGA PEPETA YATIMKIA MUSCAT


  Wanenguaji wa Twanga Pepeta wakifanya vitu vyao

  BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars maarufu kwa jina la Twanga Pepeta International, imeondoka Dar es Salaam leo kwenda Muscat, Oman kushiriki tamasha la muziki lijulikanalo kwa jina na Oman Music Festival.
  Safari hiyo imejumuisha wanamuziki wote 26 wa bendi hiyo pamoja na viongozi wawili kwa mujibu wa Mwenyekiti wa African Stars Entertainment Tanzania (ASET), Msiilwa Baraka.
  Baraka alisema kuwa safari hiyo imetoa mwanga halisi wa maendeleo ya bendi hiyo hapa nchini na kimataifa kwani hii ni mara ya tano kushiriki.
  Alisema kuwa waandaaji wa tamasha hilo la Mfalme wa Oman wanajua kile ambacho wapenzi wa muziki wanataka katika kukata kiu ya burudani na kuifanya Twanga Pepeta kuwa bendi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kushiriki mara nyingi zaidi kwa upande wa muziki wa dansi.
  Mwenyekiti huyo alisema kuwa Twanga Pepeta imeandaa nyimbo mbalimbali mpya na za zamani ili kuwapa burudani na kutoa taswira kuwa muziki kwa kampuni yao ni kazi na ndiyo maana imeajiri wanamuziki wengi zaidi hapa nchini.
  Alisema kuwa tamasha hilo linashirikisha vikundi mbalimbali vya buridani kutoka barani Afrika, Mashariki ya Mbali na Ulaya, ikiwa ni moja ya tukio kubwa la mwaka nchini Oman.
  Katika tamasha hilo la Muscat, Twanga Pepeta pia itatumia fursa hiyo kuitangaza kampuni ya simu za mkononi ya Zain yenye mtandao katika nchi 23 barani Afrika na Mashariki ya Kati.
  Twanga Pepeta inayodhaminiwa na Zain Tanzania, imeondoka leo alfajiri (kuamkia Jumatatu) baada ya onyesho maalumu la Usiku wa Zain, kwa ndege ya Kenya Airways tayari kufanya mambo makubwa katika tamasha hilo na wanamuziki hao wanatarajiwa kurejea nchini Februari 14.
  Baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo walioondoka ni pamoja na Saulo John 'Ferguson', Khalid Chuma 'Chokoraa' Charles Gabriel 'Chaz Baba', Kalala Junior, Luiza Mbutu, Saleh Kupaza, Dogo Rama, Janeth Isinika, Msafiri Said 'Diouf', Hamis Kayumbu 'Amigolas'.
  Wengine ni Abuu Semhando, Jumanne Said 'Jojoo', James Kibosho, Ismail Mzunga 'Kizunga', Miraji Shakashia 'Shakazulu', Soud Mohamed 'MCD', Gody Kanuti, Victor Mkambi, Hassan Mussa 'Nyamwela', Bakari Kisongo 'Mandela', Abdilahi Zungu, Lilian Tungaraza 'Internet' na Mwantumu Othman.
  Nyimbo mpya ambazo Twanga Pepeta itaporomosha zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu ya 10 ya bendi hiyo itakayozinduliwa mwaka huu ni pamoja na Sumu ya Mapenzi ambao ni utunzi wa Chokoraa, Shida Darasa na Mwana Dar es Salaam (Chaz Baba) na Nazi Haivunji Jiwe (Thabit Abdul).
  Twanga Pepeta hivi sasa inawachengua mashabiki kwa staili zake mpya za 'Sugua Kisigino' ya Ferguson, 'Nimeokota Kidude', Ronaldo za Chokoraa na Weka Selo, Kitumbua mbona wauza usiku, Obama, Wizi Mtupu na Mambo Maregea za Diouf.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TWANGA PEPETA YATIMKIA MUSCAT Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top