• HABARI MPYA

    Wednesday, August 01, 2012

    MTAKATIFU TOM AREJESHA ENZI ZA UKUTA WA BERLIN YANGA ULIOJENGWA NA GUTENDORF



    Ujuta wa Yanga ulioiongoza vyema kombe la Kagame
    OLIVER ALBERT ,
    GAZETI LA MWANASPOTI.
    BEKI ya Yanga inayofananishwa na 'Ukuta wa Berlin' ilikuwa ndiyo siri ya klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame wikiendi iliyopita.
    Yanga iliibuka kidedea katika mashindano hayo baada ya kuifunga Azam mabao 2-0 kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
    Baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Atletico ya Burundi, kocha wa Yanga, Tom Saintfiet, aliusuka ukuta wake na kuufanya kuwa mgumu kupitika.
    Haya ni mapinduzi makubwa aliyoleta raia huyo wa Ubelgiji, kwani Yanga msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara iliruhusu mabao 27 wakati Simba iliyotwaa ubingwa ilifungwa mabao 12 huku Azam iliyoshika nafasi ya pili ikifungwa mabao 15.
    Yanga inaelekea ilijifunza tatizo la beki yake kwani imemnasa beki wa Simba, Kelvin Yondani na kuwabomoa wapinzani wao wa jadi, Simba ambao wanalia na beki mbovu kama ilivyodhihirika kwenye Kombe la Kagame.
    Ingawa kuna wengine wanaweza kutafsiri kuwa Yanga walikuwa 'wanapaki basi', hiyo ni mbinu inayoruhusiwa kwani timu nyingi duniani zimekuwa zikifanya hivyo.
    Yanga iliyocheza mechi za mashindano hayo ilirekebisha makosa na kumaliza mashindano ikiwa imeruhusu mabao manne tu.
    Hata hivyo, Atletico ndiyo timu iliyoruhusu mabao mawili tu na kuwa timu iliyofungwa mabao kidogo zaidi ingawa haitakuwa haki kuishindanisha na Yanga kwani ilicheza mechi nne baada ya kutolewa katika robo fainali.
    Azam ilichapwa mabao matano, Simba ilitandikwa mabao sita wakati APR ya Rwanda na Vita ya Congo zimefungwa mabao saba kila moja.
    Waliounda ukuta wa Yanga ni pamoja na kipa Yaw Berko, ambaye aliumia na mechi nyingine alisaidiwa na kipa wa pili, Ali Mustapha `Barthez' wakati mabeki walikuwa Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani 'Vidic' na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
    Ili kuongeza ugumu wa beki hiyo, Saintfiet aliwapanga mabeki Stephano Mwasika na Godfrey Taita kama viungo ili kusaidiana na mabeki wa pembeni.

    Ukuta wa Berlin
    Saintfiet sasa amerudisha enzi za `Ukuta wa Berlin' wa Yanga wa mwaka 1983, ambao ulifanya timu hiyo imalize Ligi Kuu Tanzania Bara bila ya kupoteza mechi.
    Yanga katika kipindi hicho ilikuwa inafundishwa na kocha Mjerumani, Rudi Gutendorf na alitengeneza beki ngumu iliyokuwa inawajumuishwa kipa Hamisi Kinye, Yussuf Bana, Ahmed Amasha, Athumani Juma `Chama', Alan Shomari waliokuwa wanasaidiwa na viungo Juma Mkambi na Charles Boniface Mkwasa.
    Kutokana na Gutendorf kuwa, raia wa Ujerumani basi beki ile ikabatizwa jina la `Ukuta wa Berlin'.
    Ukuta wa Berlin uko nchini Ujerumani na ulijengwa na Serikali ya Ujerumani Mashariki mwaka 1961 wakati nchi hiyo imegawanyika ili kuhakikisha raia wake hawaendi upande wa Ujerumani Magharibi.
    Ukuta huo, ambao ulijengwa kwa matofali mazito na kuzungushiwa waya za umeme, ulivunjwa mwaka 1989 baada ya mataifa hayo kuamua kuungana tena na kuwa nchi moja ya Ujerumani .
    Saintfiet hivi karibuni amefanya kazi ya kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa na akili ya kulinda hadi kuwabadili viungo Haruna Niyonzima `Fabregas', Rashid Gumbo ambao mara nyingi walikuwa wavivu wa kukaba timu inapokuwa haina mpira.
    Mfano katika mechi ya fainali dhidi ya Azam, viungo wa Azam walishindwa kumpenyenyezea mipira mshambuliaji wao John Boko 'Adebayor' kwani kila walipojaribu kupita pembeni walikuwa wanakutana na mabeki wa pembeni na mawinga wa Yanga ambao walikuwa wanatibua mbinu zao na hata walipokuwa wakimpa pasi za juu Boko walikutana na kizingiti cha Yondani na Canavaro.
    Njia moja iliyobaki ilikuwa kumpenyezea Boko pasi katikati ya uwanja lakini hata huko nako wakakutana na kizingiti cha Niyonzima, Chuji na Gumbo ambao walikaba ipasavyo kuwasaidia mabeki wao.
    Boko aliingia katika mchezo huo akitazamiwa kutesa kwani katika mechi zilizotangulia aliifunga Simba mabao matatu wakati timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-1 na pia alifunga bao moja kwenye mechi na Vita.
    Lakini siku alipokutana na ukuta wa Yanga alishindwa kufanya mambo.
    Yanga ilianza michuano hiyo kwa kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi na baadaye kuiangushia mvua ya magoli Wau Salaam ya Sudan Kusini kwa kuwacharaza mabao 7-1.
    Kisha ikaitandika APR mabao 2-0 katika hatua ya makundi kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Mafunzo kwenye mchezo wa robo fainali na kufanya mchezo huo kwenda hatua ya penalti. Yanga ikashinda 5-3.
    Yanga iliendeleza wimbi lake kuibanjua APR bao 1-0 kwenye nusu fainali na baadaye ikaichapa Azam mabao 2-0 na kutwaa ubingwa.
    Saintifiet aliiambia Mwanaspoti kuwa amefurahishwa na safu ya ulinzi ya timu yake inavyofanya kazi na hiyo inampa moyo kuwa watakuwa tishio katika mashindano yoyote yale ya ndani na hata nje ya nchi.
    "Timu yangu sasa iko vizuri na nafurahia wachezaji wananielewa, ila napenda kuipongeza safu yangu ya ulinzi kwani iko makini na inacheza kwa uelewano mkubwa," alisema.

    "Kama wakiendelea hivyo timu pinzani zitapata shida kutufunga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara."

    Washambuliaji
    Saintfiet alisema licha ya beki wake kuwa nzuri, kipaumbele chake ni kuweka sawa safu ya ushambuliaji.

    "Upande wa ushambuliaji pia wachezaji wangu wanafanya vizuri ingawa wanatakiwa kuongeza bidii kwani muda mwingine tunakosa mabao mengi ya wazi, wanatakiwa kuwa makini kipindi wanapolifikia lango ili tuweze kufunga mabao mengi," alisema Saintfiet, ambaye amewahi kufundisha soka katika nchi za Afrika za Namibia, Zimbabwe na Ethiopia
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTAKATIFU TOM AREJESHA ENZI ZA UKUTA WA BERLIN YANGA ULIOJENGWA NA GUTENDORF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top