MABINGWA wa mwaka 1988 wa Ligi Kuu ya
Tanzania Bara, Coastal Union wamebaki msimu huu na kufuta desturi yao ya ‘waja
leo warudi’ leo, yaani kupanda na kushuka msimu huo huo.
Coastal ilikuwa tishio miaka ya 1980 hadi
1990 mwanzoni, lakini baada ya kuondoka kwa kizazi cha akina Razack Yussuf ‘Careca’,
Yassin Abuu Napili, Ally Maumba, Juma Mgunda na wengineo, timu hiyo iliyumba na
kuwa hohe hahe kisoka na kifedha.
Kutokana na ukweli kwamba ni timu ambayo
inapendwa mno mkoani Tanga, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitolea kuibeba kila
inaposhuka daraja- lakini kila inaporejea Ligi Kuu, msimu huo huo inashuka tena.
Hiyo ilisababisha Coastal ibatizwe jina ‘waja
leo, warudi leo’- lakini msimu huu hali imekuwa tofauti, nini siri ya mafanikio
ya Coastal?
Uongozi bora chini ya Mwenyekiti wake, Ally
Ahmad ‘Aurora’ uliotengeneza timu imara ya ushindani na kuajiri makocha bora
kama Juma Ramadhan Mgunda na Jamhuri Mussa Kihwelo.
Coastal msimu huu ilianza na kocha wa
zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hafidh Badru ambaye baada ya
mechi kadhaa za mzunguko wa kwanza timu ikifanya vibaya, ilimfukuza na
kumuajiri Julio.
Julio naye baada ya kuiwezesha timu
kushinda mechi nne za mwisho za mzunguko wa kwanza akaitelekeza timu na kwenda
Uarabuni- hivyo ikabidi Mgunda apewe kazi.
Lakini Julio alirejea na kuomba radhi,
hivyo kupewa nafasi yake tena, akishirikiana na Mgunda, hatimaye mwisho wa
msimu, timu imebaki Ligi Kuu, huku ikiwa na mikakati ya kufanya vizuri zaidi
msimu ujao, ikiwezekana kurejesha historia ya kuchukua ubingwa wa nchi.
Nyuma ya mafanikio ya Coastal msimu huu
kuna watu ambao wanastahili kuambiwa asante.
Miongoni mwao ni mfanyabiashara Mohamed Bin
Slum, mmiliki wa kampuni ya Bin Slum Tyres ambaye amekuwa akiisaidia timu hiyo
na nyingine ya Ligi Kuu, Villa Squad bila kupenda sifa za kujitangaza anafanya
nini.
Hiyo ndio desturi ya Bin Slum- si mpenda
sifa. Ni mtu anayependa kusaidia na ana mchango mkubwa katika michezo nchini,
lakini utaratibu wake ni ule ule- hapendi kujitangaza kama ilivyo kwa wafanyabiashara
au wafadhili wengi nchini.
Bin Slum ambaye amekuwa akitoa hadi misaada
binafasi kwa wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo Waandishi wa Habari,
ameahidi kuisaidia zaidi Coastal ili msimu ujao iwe tishio- na wakati huo huo
ameahidi kuendelea kuisaidia Villa irejee Ligi Kuu.
Taifa linahitaji watu kama Bin Slum kwa
maendeleo ya michezo. Huyu ni mfano wa kuigwa.
0 comments:
Post a Comment