• HABARI MPYA

    Monday, September 17, 2018

    UCHAGUZI WA SIMBA SC WAPIGWA ‘STOP’, TFF YASEMA TARATIBU NYINGI ZIMEKIUKWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UCHAGUZI wa klabu ya Simba uliopangwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu umesitishwa kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya taratibu za msingi.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Revocatus Kuuli amesema kwamba kwa kiasi kikubwa mchakato wa uchaguzi huo haujafuata taratibu zinazotakiwa.
    Kuuli amesema kwamba miongoni mwa mapungufu hayo ni ada ya uanachama kwa ngazi ya Uenyekiti pamoja na Wajumbe kutofautiana, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya klabu pamoja na TFF.
    Kiungo wa zamani wa Simba SC, Mtemi Ramadhani ni kati ya wagombea wawili tu wa nafasi ya Uenyekiti, mwingine Swedi Nkwabi na jumla ya watu 21 wamechukua kuwania nafasi mbalimbali, wengine wawili Ujumbe kwa Wanawake na 17 Ujumbe wa Bodi.

    Kaimu Rais wa klabu ya Simba SC, Salum Abdallah 'Try Again' (kushoto)

    Nafasi za Wajumbe wa Wanawake waliojitokeza ni Jasmin Badar Soud na Asha Ramadhani Baraka, wakati Wajumbe wa Bodi ni Hussein Kitta Mlinga, Iddi Noor Kajuna, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Mohammed Wandi, Suleiman Haroub Said, Abdallah Rashid Mgomba na Christopher Kabalika Mwansasu.
    Wengine ni Alfred Martin Elia, Mwina Mohammed Kaduguda, Ally Suru, Said Tully, Juma Abbas Pinto, Hamisi Ramadhani Mkoma, Abubakar Zebo, Omar Juma Mazola, Patrick Paul Rweyemamu na Suleiman Omar Suleiman.
    Fomu zilirejeshwa Jumamosi makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam na uchaguzi umepangwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu katika ukumbi ambao utatajwa baadaye mjini Dar es Salaam Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Boniphace Lihamwike. 
    Hiyo ni baada ya uongozi uliopita ulioingia madarakani juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wao.
    Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
    Na Julai 1, mwaka jana, Kamati ya Utendaji iliwateua Salum Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi Mkuu ujao.
    Katiba mpya ya Simba SC inaelekea Rais wa klabu awe na elimu ya kiwango cha Shahada ambaye ataongoza Bodi ya Wakurugenzi itakayokuwa na Wajumbe wanane chini yake.
    Na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
    Hiyo ni baada ya mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UCHAGUZI WA SIMBA SC WAPIGWA ‘STOP’, TFF YASEMA TARATIBU NYINGI ZIMEKIUKWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top