• HABARI MPYA

    Friday, September 21, 2018

    SIMBA SC KUFANYA MAAMUZI MAGUMU BAADA YA KOCHA MBELGIJI KUSHAMBULIWA NA MASHABIKI JANA

    Na Mwandishi Wetu, MWANZA
    KUFUATIA kocha Mbelgiji wa Simba SC, Patrick J Aussems kushambuliwa kwa chupa na mawe na mashabiki jana Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza baada ya kufungwa 1-0 na wenyeji, Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uongozi unataka kufanya maamuzi magumu.
    Msemaji wa mabingwa hao wa nchi, Hajji Sunday Manara alisema jana usiku kwamba uongozi pia umeumizwa na kipigo cha jana na watafanya maamuzi sahihi bila presha. 
    “Bodi ya Wakurugenzi, Sekretarieti, Benchi la Ufundi na wachezaji wa klabu ya Simba wanawaomba radhi wanachama na mashabiki wetu kwa matokeo ya leo (jana). Tumeumia sote na tunawaomba mjue hii ni mechi ya nne tu. Tutafanya maamuzi sahihi bila presha kwa maslahi makubwa ya timu na klabu, ninawaomba mtulie katika kipindi hiki," alisema Manara.

    Patrick J Aussems alishambuliwa na mashabiki jana Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza baada ya Simba kufungwa 1-0 na Mbao FC  

    Mashabiki waliwatupia chupa na vitu vingine vigumu wachezaji wa Simba SC na kocha huyo aliye katika mwezi wake wa pili tu tangu aanze kazi Msimbazi baada ya mchezo huo ambao walifungwa 1-0 na wenyeji wao.
    Na wakati wanatupa mawe walikuwa wakiimba; “Masoud haondoki”, wakimaanisha kocha Msaidizi wa klabu huyo, Masoud Juma arejeshwe kwenye timu baada ya kutosafiri na timu katika mechi mbili, kabla ya jana mjini Mtwara timu ikitoa sare ya 0-0 na Ndanda FC.
    Na Mechi zote ambazo Masoud hajasafiri timu haijashinda baada ya mwanzo mzuri wa ushindi wa mechi mbili nyumbani Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam dhidi ya Tanzania Prisons 1-0 na Mbeya City 2-0 zote za Mbeya.
    Masoud aliabaki Dar timu ikienda Mtwara huku uongozi ukisema ameachwa ili kuwachunguza wapinzani wao wa timu ampe taarifa kocha mkuu, Auussems na pia awasimamie wachezaji ambao hawajasafiri na timu.   
    Lakini upande wa pili, kuna taarifa kwamba Masoud ametofautiana na uongozi wa klabu na ni kama amewekwa kando kwa manufaa ya timu huku taratibu za kuachana naye moja kwa moja zikiendelea.
    Juma aliwasili nchini Oktoba 19, mwaka mwaka jana akitokea Rwanda alipokuwa anafundisha timu ya Rayon Sport, kuchukua nafasi ya aliyekuwa kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliyeng’atuka.
    Alianza kazi chini ya Mcameroon, Joseph Omog lakini akafukuzwa, akaletewa Mfaransa, Pierre Lechantre aliyemalizia msimu na timu ikatwaa ubingwa kabla ya kufukuzwa – na Mbelgiji, Patrick J Aussems anakuwa kocha wa tatu mkuu wa Mrundi huyo.
    Lakini wakati Lechantre anaondoka alimtupia lawama Juma akidai alimsaliti na inaelezwa alitafuta nafasi ya kuzungumza na Aussems kumueleza juu ya kocha huyo wa Burundi. 
    Bado uongozi wa Simba SC unasubiriwa kutoa hatma ya Masoud ambaye tangu Oktoba mwaka jana amekuwa Kaimu Kocha Mkuu mara mbili na timu ikaendelea kufanya vizuri.    
    Huenda vurugu za jana ambazo zilishuhudia hadi Kaimu Rais wa timu, Salum Abdallah ‘Try Again’ na Msemaji Hajji Manara wakishambuliwa pia zinaweza kubadili upepo. 
    Hiyo ni kutokana na taarifa jana usiku kwamba klabu inataka kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya timu.
    Bao la Mbao FC jana lilifungwa na kiungo Said Khamis Said dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti, kufuatia mshambuliaji Pastory Athanas kuangushwa na kipa wa Simba SC, Aishi Salum Manula wakati anakwenda kufunga.
    Kwa matokeo hayo, mabingwa hao watetezi, Simba SC wanabaki na pointi zao saba baada ya kucheza mechi nne, wakishinda mbili dhidi ya timu za Mbeya, Tanzania Prisons 1-0 na Mbeya City 2-0, sare moja 0-0 na Ndanda FC na kipigo cha leo cha Mbao FC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUFANYA MAAMUZI MAGUMU BAADA YA KOCHA MBELGIJI KUSHAMBULIWA NA MASHABIKI JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top