• HABARI MPYA

    Sunday, September 23, 2018

    BOCCO AFUNGA MAWILI NA KUFIKISHA MABAO 100 LIGI KUU SIMBA SC YASHINDA 3-1

    Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
    NAHODHA John Raphael Bocco amefunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1 wa mabingwa watetezi, Simba SC dhidi ya wenyeji, Mwadui FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga – lakini akatolewa kwa kadi nyekundu.
    Ushindi huo unarejesha amani Simba SC baada ya timu kucheza mechi mbili zilizopita bila kushinda, ikitoa sare ya 0-0 na Ndanda FC mjini Mtwara na kufungwa 1-0 na Mbao FC mjini Mwanza.
    Simba SC sasa inafikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi tano kuelekea pambano dhidi ya watani wa jadi, Yanga Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Bocco ambaye atakosa mechi dhidi ya Yanga Septemba 30, alifunga bao la kwanza kwa penalti dakika ya 41 baada ya kiungo Shiza Kichuya kuangushwa na Miraj Maka kwenye boksi dakika ya 40.
    Bocco akaweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 100 kwenye Ligi Kuu tangu imeanzishwa mwaka 1996, baada ya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 45, akimalizia pasi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe kufuatia krosi ya mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere.
    John Bocco (kushoto) amefunga mabao mawili lakini ametolewa kwa kadi nyekundu PICHA YA MAKTABA


    Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza tangu amewasili kutoka Gor Mahia ya Kenya akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 50 kwa shuti kali kutoka umbali wa mita 16 baada ya kuwazidi mabeki wa Mwadui FC.
    Nahodha Bocco akatolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 80 baada ya kumpiga ngumi beki wa Mwadui FC, Revocatus Richard wakati wawili hao wakigombea mpira.
    Na Mwadui FC wakatumia fursa hiyo kujipatia bao la kufutia machozi kwa shambulizi la kushitukiza, mfungaji Charles Ilamfya dakika ya 81 baada ya kumzidi mbio na ujanja, beki wa Simba SC, Serge Wawa Pascal.
    Mwadui ikauteka mchezo na kupeleka mashambulizi mawili ya nguvu langoni mwa Simba SC, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi. 
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Tafadzwa Kutinyu dakika ya 59 limeipa ushindi wa 1-0 Azam FC dhidi ya wenyeji, Alliance FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na sasa timu hiyo ya Aljah Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inafikisha pointi tisa baada ya mechi tano.
    Nayo Mbeya City imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Kagera Sugar ya Bukoba Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wenyeji wakitangulia kwa bao la Eliud Ambokile dakika ya 34 kabla ya Suleiman Mangoma kuwasawazishia wageni dakika ya 52. 
    Mechi ya mwisho ya Ligi Kuu leo inafuatia Saa 1:00 usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya Singida United. 
    Kikosi cha Mwadui FC kilikuwa; Arnold Massawe, Revocatus Richard, Iddi Mfaume, Joram Mgeveke, Miraj Maka, Jean Marie Gurukwishaka, Salim Salum, Abdallah Omar, Charles Ilamfya, Edwin Innocent/John Elias dk67 na Ibrahim Irokoze/Leonard Bhoke dk86.
    Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascla Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Cletus Chama, John Bocco, Meddie Kagere na Shiza Kichuya/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk63.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO AFUNGA MAWILI NA KUFIKISHA MABAO 100 LIGI KUU SIMBA SC YASHINDA 3-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top