Kikosi cha Tanzania Bara |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
DUA njema za
Watanzania kwa ujumla, leo zitaelekezwa mjini hapa, wakati timu mbili kutoka
Jamhuri ya Muungano wetu, Bara na Zanzibar zitakapokuwa zikipigana katika Robo
Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker
Challenge kwenye Uwanja wa Lugogo.
Bara,
maarufu Kilimanjaro Stars watakuwa wa kwanza kutupa kete yao leo kuanzia saa
8:00 mchana kwa kumenyana na Rwanda, kwa jina la utani Amavubi, yaani Nyigu,
wakati Zanzibar Heroes watasubiri hadi saa 10:00 kukipiga na Burundi, Int’hamba
Murugamba, yaani Mbayuwayu.
Robo Fainali
nyingine zinatarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kenya
ikianza na Malawi saa 10:00 jioni kabla wenyeji Uganda kumenyana na Ethiopia
saa 1:00 usiku.
Zanzibar wakiomba dua kabla ya mechi na Rwanda waliyoshinda 2-1 |
Mchezo kati
ya Burundi na Zanzibar unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua, na zaidi
Mashujaa wa Visiwani wanatakiwa kumchunga sana Nahodha wa Mbayuwayu, Suleiman
Ndikumana kwa sababu ndiye amekuwa akiiongoza vema timu yake.
Ndikumana
amekuwa akihaha Uwanja wa mzima, akicheza kwa kuwahamasisha wadogo zake na hadi
sasa ndiye Nahodha bora zaidi katika mashindano haya.
Hazina ya
Zanzibar ni safu nzuri ya kiungo inayoongozwa na Suleiman Kassim Selembe na
Khamis Mcha ‘Vialli ’bila kusahau ukuta imara chini ya mabeki Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Aggrey Morris na hata kipa hodari, Mwadini Ally.
Safu ya
ushambuliaji leo hakuna shaka itaongozwa na Jaku Juma, mkali wa mabao katika
Ligi Kuu ya Zanzibar na Seif Abdallah, nyota wa Ruvu Shooting ya Bara aliye
mbioni kuhamia Azam FC.
Mambo zaidi
ni Rwanda na Bara; jezi namba nane (8) leo zinatarajiwa kuwa kila kitu. Jezi
hiyo kwa upande wa Rwanda anavaa Haruna Hakizimana Niyonzima na Bara Mrisho
Khalfan Ngassa.
Wawili hawa
ndio wamekuwa kama roho ya timu zao katika mashindano haya na leo wanatarajiwa
kuendelea kubeba jukumu hilo.
Ngassa
anacheza wingi ya kushoto kwa sasa kwenye kikosi cha Bara, wakati Niyonzima
anapangwa wingi ya kulia katika kikosi cha Rwanda. Niyonzima huwa anabadilika
na kuingia ndani na wakati mwingine upande wa pili na kwa ujumla huhaha Uwanja
mzima, vivyo hivyo kwa Ngassa.
Dadi Birori au
Taddy Etikiama kwa jina lingine atasimama mbele bila kuongoza mashambulizi kwa
Rwanda na langoni atakuwapo kipa mgumu kufungika, Jean Claude Ndoli.
Kocha wa
Bara, Mdenmark Kim Poulsen anacheza na mshambuliaji mmoja, John Bocco, lakini
anatumia mawinga wenye kushambulia mno- Ngassa na Simon Msuva, wakati Micho pia
hutumia washambuliaji wawili na hana viungo wenye kasi sana, ila mafundi.
Mabeki wa
pembeni wa Rwanda wanapitika kwa urahisi na leo Ngassa na Msuva washindwe
wenyewe tu. Beki ya kati ya Rwanda ni ugonjwa wa moyo, maana yake John Bocco
leo ni umakini wake tu.
Kwa ujumla,
Bara ina nafasi kubwa ya kuitoa Rwanda, tena kwa kuipa kipigo kitakatifu tu
kama watatumia vyema nafasi zao.
Mwinyi
Kazimoto amepona na bila shaka atakuwa mmoja wa viungo watatu leo, wengine
Frank Domayo na Amri Kiemba maana yake, kwenye benchi watakuwapo Athumani Iddi
‘Chuji’ na Shaaban Nditi.
Piga, ua
Juma Kaseja atasimama langoni, kulia Erasto Nyoni na kushoto uzoefu utambeba
Amir Maftah ingawa Issa Rashid anakuja vizuri, wakati katikati Kevin Yondan
atacheza pacha na Shomary Kapombe.
Hii ni mara
ya pili ndani ya miaka mitatu Bara kukutana na Rwanda katika hatua hii na mara
ya mwisho ilikuwa Desemba 8, mwaka 2010 wakati bao pekee la mkwaju wa penalti
la aliyekuwa Nahodha wa Stars, Nsajigwa Joel Shadrack Mwandemele dakika ya 61
lilipoipa Bara ushindi wa 1-0 na kutinga Nusu Fainali hadi kutwaa ubingwa Dar
es Salaam.
Lakini mwaka
jana pia timu hizo zilikutana Dar es Salaam katika michuano hii, Kundi A na
Rwanda iliilaza Bara 1-0 Novemba 26, katika michuano ambayo wenyeji waliboronga
vibaya na kutolewa mapema.
Tangu mwaka
2001, timu hizi zimekutana mara tisa katika Challenge na Rwanda imeshinda mechi
sita, wakati Bara imeshinda mechi tatu tu. Idadi kubwa ya mabao Tanzania
kuifunga Rwanda ni 3-0, wakati Amavubi wamewahi kuichapa Bara 5-1.
Pamoja na
yote, Robo Fainali za leo ni nzuri- zaidi Watanzania kwa ujumla Bara na
Visiwani, wanatakiwa kuziombea dua njema timu zao zivuke hatua hii, kwani
katika soka lolote hutokea. Mungu
ibariki Bara na Zanzibar, ibariki Tanzania. Amin.
REKODI YA
TANZANIA NA RWANDA CHALLENGE:
Desemba 17, 2001; Nusu Fainali Rwanda
Tanzania 1-2
Rwanda B
Desemba 11, 2002; Nusu Fainali Mwanza
Tanzania 3-0
Rwanda
Desemba 19, 2004; Kundi A Ethiopia
Tanzania 1-5
Rwanda
Desemba 6, 2005; Kundi A Rwanda
Tanzania 1-3
Rwanda
Desemba 5, 2006; Robo Fainali Ethiopia
Tanzania 1-2
Rwanda
Januari 7, 2009; Kundi A Uganda
Tanzania 2-0
Rwanda
Desemba 10, 2009: Nusu Fainali Kenya
Tanzania 1-2
Rwanda
Desemba 8, 2010; Robo Fainali Dar es Salaam
Tanzania 1– 0 Rwanda
Novemba 26, 2011; Kundi A, Dar es Salaam
Tanzania 0 – 1 Rwanda
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE
2012
Mrisho
Ngassa Tanzania 5
John Bocco Tanzania 4
Suleiman
Ndikumana Burundi 3 (1 penalti)
Brian Umony Uganda 3
Chris
Nduwarugira Burundi 3
Khamis Mcha Zanzibar 2
David
Ochieng Kenya 2
Clifton
Miheso Kenya 2
Dadi Birori Rwanda 2