John Bocco 'Adebayor' |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
JOHN Raphael
Bocco amezidi kuwa gumzo kubwa katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge yanayoendelea mjini hapa.
Wapiga picha
wa Televisheni ya SuperSport wanamsifia sana Bocco na wanasema kuna uwezekano
sasa klabu ya SuperSport United ya Afrika Kusini ikamgeukia tena.
“Amefunga
katika kila mechi aliyocheza, huyu ni mfungaji wa uhakika, ni mshambuliaji
mwenye nguvu, kasi na uwezo wa kumiliki mpira, anapiga sana vichwa, ana kiwango
cha kucheza PSL (Ligi Kuu ya Afrika Kusini),”alisema mmoja wa wapiga picha hao
jana.
Jamaa wa
SuperSport wanemuhesabia Bocco hata bao ambalo alifunga kwenye mechi dhidi ya
Burundi lakini refa akakataa, ndiyo maana wanasema amefunga katika kila mechi.
Hadi sasa,
rasmi Bocco ana mabao manne, ukiondoa hilo ambalo refa ameminya. Alifunga mabao
mawili katika mechi dhidi ya Sudan na akarudia kufunga idadi hiyo dhidi ya
Somalia.
Bocco
anazidiwa bao moja tu na Mrisho Khalfan Ngassa, aliyefunga matano, lakini yote
katika mechi moja dhidi ya Somalia.
Bocco maarufu
kwa jina la utani ‘Adebayor’ anayechezea Azam FC ya Dar es Salaam, alifanya
vizuri katika majaribio yake kwenye klabu ya SuperSport United ya Afrika Kusini
Agosti mwaka huu, lakini klabu hiyo ikashindwa kufika dau la kumng’oa Chamazi.
SuperSport
ilivutiwa na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu mjini Dar es Salaam hivyo
kumuita kwa majaribio, ambayo alifuzu.
Katika Kombe
la Kagame, Bocco alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika
wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza aliyefungana na Tadi Etikiama kwa mabao
sita, na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora kwa mabao yake saba.
Lakini Bocco
pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita,
kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo
msimu huo, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.
Tangu
aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka
mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za
kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace
Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa
tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa
mfungaji bora wa ligi hiyo.
Iwapo
atanunuliwa na SuperSport, Bocco ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa
Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea
Simba SC.