• HABARI MPYA

    Thursday, April 16, 2009

    MGOSI AONDOKA KESHO KWENDA INDIA


    MSHAMBULIAJI bora nchini, Mussa Hassan Mgosi (pichani akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Harambee Stars ya kenya) wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, anatarajiwa kuondoka kesho nchini kwenda India kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Mahindra United inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.
    Mgosi aliiambia bongostaz kwa simu leo mchana kwamba mambo yote yamekamilika na anaomba dua za Watanzania, ili aende kufanya vizuri huko.
    “Nashukuru wakala wangu amefanikisha mipango ya mimi kwenda kucheza soka la kulipwa nje, naomba dua za Watanzania niende kufanya vizuri huko, kwa sababu kama Tanzania itakuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje, timu yetu ya taifa itakuwa nzuri,”alisema.
    Mapema Jumatatu, alisema: “Nimeambiwa kuna mchezaji Mwafrika alikuwa kule, amepata timu Ufaransa, sasa nakwenda kuziba pengo lake, jamaa kaniambia yule aliyeondoka alikuwa analipwa dola 8,000 (za Kimarekani) kwa mwezi. Sasa mimi sijui nitaenda kulipwa kiasi gani,” alisema Mgosi.
    Mgosi ambaye aling’ara kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) iliyomalizika Februari, mwaka huu mjini Abidjan, Ivory Coast, aliteuliwa kwenye kikosi cha nyota 18 wa michuano hiyo, akiwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba.
    Akiwa huko, alipata wakala, Moustapha Fall, raia wa Senegal ambaye aliahidi kumtafutia timu haraka iwezekanavyo kati ya nchi za Ufaransa, India, Norway na Falme za Kiarabu.
    Mgosi, ambaye ni mchezaji pekee wa Tanzania kuingia kwenye kikosi hicho, mafanikio yake yametokana na subira, nidhamu, kujituma na kusikiliza kwa makini maelekezo ya walimu.
    Mwaka 2005 alikwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Meritzburg Classic ya huko, lakini mambo hayakuwa mazuri na mwaka jana alikwenda Oman kujiunga na Oman Club, lakini pia mipango haikwenda vizuri.
    Mgosi, aliyezaliwa Agosti 20, 1985 wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Pasua, Moshi, kabla ya kujiunga na Sekondari ya Makongo, Dar es Salaam alikohitimu kidato cha Nne,
    Kabla ya kutua Simba mwaka 2005, Mgosi aliichezea Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa msimu mmoja wa 2004, ambayo alijiunga nayo kutoka klabu iliyomuibua kisoka, JKT Ruvu, aliyoanza kuichezea 2001, akitokea sekondari ya Makongo.
    JKT ilivutiwa na Mgosi akiwa kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, enzi hizo kikinolewa na Mnigeria, Ernest Mokake (sasa marehemu). Baadaye alipandishwa timu ya chini ya miaka 20, kabla ya kuchukuliwa timu ya wakubwa, Taifa Stars mwaka 2005.
    Mgosi, ambaye ni mume wa Jasmin Elias, waliyezaa naye watoto wawili hadi sasa, Hassan na Nailat, akifanikiwa kununuliwa na Mahindra, atakuwa Mwafrika wa nne kwenye timu hiyo baada ya beki Lamine Tamba wa Senegal, kiungo Pierre Djidjia Douhou wa Ivory Coast na mshambuliaji Chidi Edeh wa Nigeria. Mgeni mwingine kwenye timu hiyo inayonolewa na Wabrazil, Denis D'Souza akisaidiwa Derrick Pereira na mzalendo, Mahesh Lonitkar, ni kiungo Arata Izumi wa Japan.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MGOSI AONDOKA KESHO KWENDA INDIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top