• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 07, 2009

  SIMBA WAPATA AJALI WAKITOKEA BUKOBA

  WACHEZAJI wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam juzi usiku walipata ajali wakiwa njiani kurejea nyumbani, kutoka Bukoba walikokwenda kumenyana na wenyeji Kagera Sugar ambako waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
  Akizungumza kwa simu kutoka eneo la tukio, mchezaji mwandamizi wa Simba, Ulimboka Alfred Mwakingwe alisema kwamba basi la abiria walilokuwamo, liligonga ng’ombe maeneo ya Kahama hivyo kulazimika kusimama kwa muda kuweka mambo sawa.
  “Kwanza wanatengeneza tengeneza kule mbele, maana kumeharibika, yaani hii leo tulitegemea tungelala Dodoma, lakini kwa hali ilivyop sijui kama tutaweza,”alisema Mwakingwe majira ya saa 1.30 usiku juzi, alipozungumza na DIMBA.
  Wachezaji hao wa Simba, wakati wanakwenda pia Bukoba, ilielezwa kwamba walitaka kuvamiwa na kutekwa na majambazi, katika pori moja eneo la Biharamulo, lakini jitihada za askari mmoja aliyefyatua risasi ziliwaokoa na wakaweza kuepuka jaribio hilo.
  Simba iliyotarajiwa kutua jana mjini Dar es Salaam, moja kwa moja itaanza kujinoa kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Toto Afrika ya Mwanza, kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa Jijini Jumapili.
  Simba yenye pointi 33 sasa, inahitaji kushinda mchezo na mingine miwili iliyosalia dhidi ya Polisi Dodoma na Yanga, ili kujihakikishia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ambayo itawawezesha kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mwakani.
  Katika nafasi hiyo, Simba inafukuziwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro yenye pointi 31, Kagera Sugar ya Bukoba na Prisons ya Mbeya, ambazo kila moja ina pointi 28.
  Tayari ubingwa wa Ligi hiyo umekwishachukuliwa na Yanga iliyofikisha pointi 47, ambazo haziwezi kufikiwa na tim yoyote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WAPATA AJALI WAKITOKEA BUKOBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top