• HABARI MPYA

    Monday, April 13, 2009

    MGOSI APIGWA STOP NA TFF


    WAKATI zimebaki siku saba kabla ya mechi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, klabu ya Simba imepata pigo kutokana na nyota wake mwenye ngekewa ya kuwafunga wapinzani wao hao, Mussa Hassan Mgosi kuwa hatarini kufungiwa kati ya miezi mitatu hadi 12, kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Kanuni ya 25 ya Ligi Kuu, kifungu (e) inasema; “Mchezaji yeyote atakayempiga mchezaji mwenzake au kiongozi yeyote kabla, wakati au baada ya mchezo atafungiwa kucheza mpira kwa kipindi cha miezi 3 – 12 au atafungiwa kucheza idadi ya michezo ambayo kamati ya utendaji itaona inafaa au atalipa faini kama itakavyopangwa na kamati ya utendaji au vyote kwa pamoja,”.
    Mgosi alipewa kadi nyekundu baada ya kupigana na kipa wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado na jana Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema kwamba wameziandikia barua klabu zote, kuzitahadharisha zisiwatumie wachezaji hao, hadi hapo Kamati ya Mashindano itakapokutana na kutoa uamuzi.
    “Kwa kuwa ripoti za mwamuzi na Kamisaa wa mchezo huo zinaonyesha kwamba wachezaji hao walipigana, ni lazima kamati hiyo ikae kwa mujibu wa kanuni. Sasa baadhi ya wajumbe walitoa udhuru.
    “Badala yake, tumewaandikia barua viongozi wa Simba na Mtibwa kuwataka kutowatumia kwanza wachezaji hao kwa michezo yao ijayo hadi hapo uamuzi utakapochukuliwa,” alisema Mwakalebela kwa njia ya simu, akiwa njiani kuelekea Iringa kwa mapumziko ya Pasaka.
    Mgosi na Kado walijikuta wakipewa kadi nyekundu wakati wa mchezo baina ya timu zao uliofanyika Morogoro Machi 22 mwaka huu ambao Simba walikubali kipigo cha bao 1-0.
    Mwakalebela alisema kikao cha kuwajadili wachezaji hao kilishindwa kufanyika jana kutokana na kutotimia kwa idadi ya wajumbe, lakini watahakikisha wanakutana mapema wiki ijayo.
    Mbali na Mgosi, mchezaji mwingine mkongwe wa Simba, Ulimboka Alfred Mwakingwe ataukosa mchezo wa leo dhidi ya Toto Afrika, Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
    Lakini Mwakingwe anatarajiwa kurejea dimbani kwa ajili ya mechi dhidi ya watani wa jadi, Yanga Jumapili ijayo, akiwa mmoja kati ya wachezaji wanaowatia hofu kubwa watani wao hao.
    Ulimboka alizusha balaa kubwa Oktoba 24, mwaka 2007 kwa watani wao hao wa jadi, baada ya kufunga bao pekee kwenye mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati timu yake, Simba ikishinda 1-0.
    Uli aliyepokea pasi ya Nurdin Bakari ambaye sasa anachezea Yanga, baada ya mchezo huo alisababisha wachezaji watano wasimamishwe kabla ya mmoja kufukuzwa kabisa na wengine wawili kufungiwa kwa miezi sita, wakati wawili walisamehewa baada ya kujitetea.
    Aliyefukuzwa ni Edwin Mukenya, waliofungiwa ni Ivo Mapunda ambaye sasa anachezea St George ya Ethiopia na Nsajigwa Shadrack wakati waliosamehewa baada ya kujitetea ni Ben Mwalala na Amir Maftah.
    Uli pia aliwahi kuwaliza Yanga Agosti 7, mwaka 2004 katika ligi hiyo wakati, Simba inaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya watani.
    Siku hiyo, Pitchou Kongo alitangulia kuifungia Yanga bao Uwanja wa Taifa, kabla ya Shaaban Kisiga kusawazisha dakika ya 64 na Uli kupiga la pili dakika ya 76.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MGOSI APIGWA STOP NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top