• HABARI MPYA

  Saturday, April 18, 2009

  MGOSI AENDA INDIA AKIITAKIA HERI SIMBA


  MSHAMBULIAJI bora nchini, Mussa Hassan Mgosi wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, aliondoka jana jioni kwenda India kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Mahindra United, inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.
  Akiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam dakika chache kabla ya kupanda ndege, Mgosi aliiambia bongostaz kwamba anaitakia kila la heri, timu yake, Simba katika mchezo wa kesho dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga.
  “Ningependa kuwa sehemu ya mchezo huo, lakini TFF imenisimamisha, nimeona tu bora niwahi kwenye majaribio yangu India,” alisema Mgosi.
  Mgosi amekwenda huko kwa ajili ya kuziba pengo la mchezaji mmoja kutoka Afrika ambaye ameuzwa Ufaransa. Mapema Jumatatu Mgosi, alisema: “Nimeambiwa kuna mchezaji Mwafrika alikuwa kule, amepata timu Ufaransa, sasa nakwenda kuziba pengo lake, jamaa kaniambia yule aliyeondoka alikuwa analipwa dola 8,000 (za Kimarekani) kwa mwezi. Sasa mimi sijui nitaenda kulipwa kiasi gani,” alisema Mgosi.
  Mgosi ambaye aling’ara kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) iliyomalizika Februari, mwaka huu mjini Abidjan, Ivory Coast, aliteuliwa kwenye kikosi cha nyota 18 wa michuano hiyo, akiwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba.
  Akiwa huko, alipata wakala, Moustapha Fall, raia wa Senegal ambaye aliahidi kumtafutia timu haraka iwezekanavyo kati ya nchi za Ufaransa, India, Norway na Falme za Kiarabu.
  Mgosi, ambaye ni mchezaji pekee wa Tanzania kuingia kwenye kikosi hicho, mafanikio yake yametokana na subira, nidhamu, kujituma na kusikiliza kwa makini maelekezo ya walimu.
  Mwaka 2005 alikwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Meritzburg Classic ya huko, lakini mambo hayakuwa mazuri na mwaka jana alikwenda Oman kujiunga na Oman Club, lakini pia mipango haikwenda vizuri.
  Mgosi, aliyezaliwa Agosti 20, 1985 wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Pasua, Moshi, kabla ya kujiunga na Sekondari ya Makongo, Dar es Salaam alikohitimu kidato cha Nne,
  Kabla ya kutua Simba mwaka 2005, Mgosi aliichezea Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa msimu mmoja wa 2004, ambayo alijiunga nayo kutoka klabu iliyomuibua kisoka, JKT Ruvu, aliyoanza kuichezea 2001, akitokea sekondari ya Makongo.
  JKT ilivutiwa na Mgosi akiwa kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, enzi hizo kikinolewa na Mnigeria, Ernest Mokake (sasa marehemu). Baadaye alipandishwa timu ya chini ya miaka 20, kabla ya kuchukuliwa timu ya wakubwa, Taifa Stars mwaka 2005.
  Mgosi, ambaye ni mume wa Jasmin Elias, waliyezaa naye watoto wawili hadi sasa, Hassan na Nailat, akifanikiwa kununuliwa na Mahindra, atakuwa Mwafrika wa nne kwenye timu hiyo baada ya beki Lamine Tamba wa Senegal, kiungo Pierre Djidjia Douhou wa Ivory Coast na mshambuliaji Chidi Edeh wa Nigeria. Mgeni mwingine kwenye timu hiyo inayonolewa na Wabrazil, Denis D'Souza akisaidiwa Derrick Pereira na mzalendo, Mahesh Lonitkar, ni kiungo Arata Izumi wa Japan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MGOSI AENDA INDIA AKIITAKIA HERI SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top