• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 02, 2009

  AL AHLY WATUA NA MAJIGAMBO, MCHECHETO


  MABINGWA wa soka Afrika, Al Ahly ya Misri (baadhi ya wachezaji wake kushoto) waliwasili mjini Dar es Salaam jana kwa ajili ya mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya wenyeji wao Yanga utakaofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wakali hao waliwasili saa 3:20 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) na kulakiwa na Katibu wa Mashindano wa Yanga, Emmanuel Mpangala na Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Idd Mshangama.
  Akizungumza uwanjani hapo, kocha wa timu hiyo, Manuel Jose ambaye mwanzoni aligoma kuzungumza lolote akisema wamechoka, alisema kwa ufupi: ''Tuliiona Yanga kwetu, tunaiheshimu, lakini hapa tumekuja kwa nia moja, ushindi''.
  ''Wajue kwamba hatukufuata sare hapa wala kufungwa hapa tumekuja kutwaa ushindi na kusonga mbele'' .
  Kocha huyo alikiri kuwa Yanga ni timu nzuri, lakini hawako makini katika ushambuliaji. ''Niliona wanaingia hata kwenye 18, lakini wanakosa umakini wa kufunga, ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri,'' alisema.
  Alisema hawaihofii hali ya hewa kwa kuwa nchi zote za ukanda wa pwani ya bahari zina mazingira na hali ya hewa inayofanana.
  Kikosi kilichowasili jana kinaundwa na makipa: Ramzy Saleh, Amir Abdel Hamid na Ahmed Adel
  Mabeki: Mohamed Samir, Wael Gomaa, Ahmed El Saied na Shady Mohamed ambaye ni nahodha wakati viungo ni; AbouTrika, Barakat, Fathi, Gilberto, Saied Moawad, Motaz Eno, Hossam Ashoor na Ahmed Seddik.
  Washambuliaji wa timu hiyo wanaokamilisha kundi la watu 39 pamoja na jopo la waandishi wa habari, linaundwa na Ahmed Belal, Osama Hosni, Flavio na Hani El Eguizi.
  Timu hiyo itapambana na Yanga ikiwa ni mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mchezo wa awali, Yanga ilitandikwa mabao 3-0.
  Baada ya kuwasili, kikosi chake cha wachezaji 19 kilikwenda moja kwa moja kwenye basi walilokuwa wameandaliwa, lakini maofisa wake wakikataa kupanda gari dogo aina ya Toyota Cresta la wenyeji wao.
  Lakini, baada ya majadiliano na mama mmoja ambaye hakuwa tayari kujitambulisha na anahisiwa kuwa ni mmoja wa maofisa wa ubalozi wa Misri nchini, viongozi hao walikubali kupanda gari hilo.
  Hata hivyo, viongozi wa Ahly walieleza kuwa wasingeweza kufikia Hoteli ya Durban iliyoko Kariakoo, Dar es Salaam waliyokuwa wameandaliwa na wenyeji wao na kudai watakwenda Movenpick.
  Mpangala alisema: "Sisi hatuko tayari kuwalipia gharama za Movenpick, tutalipa zile za Durban na sehemu itakayozidi watajilipia wenyewe.
  Aliongeza: "Sijui kwanini wamekataa hoteli hii, labda wana sababu zao nyingine."
  Katika kikosi hicho, beki Wael Gomaa, Barakat na Ahmed Fathi wako katika matibabu makali kuhakikisha wanapona haraka baada ya kuumia katika mechi dhidi ya Zambia kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Dunia.
  Abou Trika aliungana na wenzake Uwanja wa Ndege wa Cairo muda mfupi kabla ya kuondoka akitokea Algeria alikokwenda kupokea tuzo yake ya Mchezaji Bora wa Kiarabu mwaka 2008, zinazotolewa na gazeti la Al Hadaaf.
  Kiungo huyo alitangazwa na gazeti hilo kuwa mchezaji bora kwa kuiwezesha nchi yake kutwaa ubingwa wa Afrika Ghana 2008, ubingwa wa ligi ya Misri, ubingwa wa Afrika na kufanya vizuri katika Klabu Bingwa ya Dunia nchini Japan 2008.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AL AHLY WATUA NA MAJIGAMBO, MCHECHETO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top