• HABARI MPYA

  Jumamosi, Aprili 11, 2009

  STARS KUJIPIMA KWA MABINGWA WA CHAN


  TIMU ya Soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Timu ya Soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mei 9. Kongo ndio mabingwa wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani iliyofanyika Ivory Coast Februari 22 - Machi 8. Kongo ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo mipya kwa kuichapa Ghana mabao 2-0 katika fainali. Stars, ilishiriki kwenye fainali hizo lakini iliishia hatua ya makundi baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Fredrick Mwakalebela alisema mechi hiyo ni ya maandalizi ya mechi dhidi ya New Zealand iliyopangwa kuchezwa Juni 3. mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Taifa. “Timu hiyo ya Taifa ya Kongo itawasili hapa nchini Mei 6 ambapo itakuwa ni siku ya Jumatano ili kucheza mechi hiyo ya kupimana nguvu dhidi ya timu yetu ya hapa nyumbani,” alisema Mwakalebela. Alisema kutokana na TFF kubeba gharama za usafiri, malazi na chakula kwa timu hiyo, wamekubaliana walete kikosi bora kilichonyakua ubingwa wa CHAN pamoja na wachezaji wao wanaosakata kandanda nje ya nchi hiyo. Alisema kikosi cha Stars kitaingia kambini mapema baada ya mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Aprili 26 na kwamba Kocha Mkuu wa Stars Marcio Maximo aliyepo mapumzikoni Brazil anatarajiwa kurejea wiki ijayo. Mwakalebela alisema TFF inaendelea na juhudi za kuipatia Stars mechi zaidi ambapo Agosti 10 inatarajiwa kushuka tena dimbani kuumana na timu itakayotangazwa baadaye. Wakati huohuo Evance Ng’ingo anaripoti kuwa TFF leo inatarajia kuanza kufunga vifaa vya mazoezi (GYM) kwa ajili ya wachezaji wa timu za taifa za vijana, ya wakubwa na wanawake. Mwakalebela alisema kuwa vifaa hivyo vina thamani ya Sh milioni 30 na fedha hizo wamepewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Mwakalebela alisema kuwa vifaa hivyo vitafungwa katika ofisi za shirikisho hilo zilizopo Karume, Ilala na chumba kitakuwa wazi kwa ajili wa wachezaji kushiriki masaa yote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: STARS KUJIPIMA KWA MABINGWA WA CHAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top