• HABARI MPYA

  Thursday, April 16, 2009

  REFA WA SIMBA, YANGA UTATA MTUPU  MWAMUZI Israel Nkongo wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi ya watani wa jadi nchini Simba na Yanga itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Habari za uhakika zilizopatikana jana ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zilieleza kuwa mwamuzi huyo ameteuliwa kuchukua nafasi ya Oden Mbaga aliyekuwa amepangwa awali kupuliza filimbi katika mchezo huo. Mara kwa mara linapofika suala la waamuzi wa mechi ya watani kila upande huwa makini kujua nani atakuwa na jukumu la kupuliza filimbi na wakati mwingine baadhi ya viongozi hudiriki hata kukataa baadhi ya waamuzi. Imedaiwa kuwa Mbaga amebadilishwa kwa madai kuna mechi ya kimataifa anaenda kuchezesha, ingawa chanzo chetu hakikuweka wazi mechi hiyo. Waamuzi wote hao wana beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Alipoulizwa suala hilo jana, Katibu Mkuu wa TFF Frederick Mwakalebelan (pichani) alisema, mwamuzi wa mechi hiyo atatangazwa. “Mwamuzi mtatangaziwa nyie subirini tu,” alisema. Na alipoulizwa kwanini mwamuzi wa mechi hiyo atangazwe tena wakati alishapangwa tangu mwanzo kama ilivyokuwa kwenye mechi zingine, Mwakalebela alisema: “Unajua kuna mambo yamebadilika, kuna wengine wamepata nafasi za CAF (Shirikisho la Soka Afrika), lakini mwamuzi atatangazwa,”alisema. Mechi hiyo inatarajiwa kuvuta hisia za wadau wengi wa soka kutokana na umuhimu wake kwa Simba inayotafuta nafasi ya pili ili kupata uwakilishi wa michuano ya kimataifa mwakani. Wakati huohuo, Mwakalebela alisema, Kamati ya Mashindano ya TFF, inatarajiwa kukutana kesho kujadili masuala mbalimbali ya ligi likiwamo lile la mchezaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba na kipa Shaaban Kado wa Mtibwa Sugar wanaodaiwa kupigana wakati wa mechi iliyozikutanisha timu zao Machi mwaka huu. Mwakalebela alisema, kamati hiyo itakutana chini ya Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho hilo, Ramadhani Nassib. Hata hivyo Katibu huyo hakutaka kulizungumzia kwa undani suala hilo na kusema usubiriwe uamuzi ya kamati hiyo. Kanuni za ligi zinaeleza kuwa mchezaji atakayethibitika kupigana uwanjani atafungiwa michezo sita au miezi mitatu hadi mwaka mmoja au adhabu ya faini kulingana na Kamati ya Mashindano itakavyoona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: REFA WA SIMBA, YANGA UTATA MTUPU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top