• HABARI MPYA

  Monday, April 13, 2009

  NURDIN: MIMI NABAKI YANGA

  BEKI anayemudu kucheza kama kiungo pia, Nurdin Bakari Hamadi (pichani mwenye rasta) amesema kwamba hana mpango wa kurejea klabu yake ya zamani na kwamba ataendelea kuichezea klabu yake ya sasa, Yanga ambayo aliingia nayo mkataba wa miaka mitatu mwaka jana.
  Katika mahojiano maalum na bongostaz, Nurdin alisema kwamba amekuwa akisikia tu taarifa kwamba yeye anataka kurejea Simba msimu ujao, lakini hazina ukweli wowote kwani yeye ni mchezaji halali wa Yanga na huko ndiko akili yake ilipolalia.
  “Kama nitatoka Yanga kwa sasa, basi ujue mipango yangu ya kwenda nje imefanikiwa, lakini kusema niondoke hapa nijiunge na klabu nyingine ya hapa Tanzania, huo ni uzushi mtupu,”alisema Nurdin.
  Nurdin aliyejiunga na Yanga msimu huu akitokea Simba, aliachwa na klabu yake zamani ikidai eti ana matatizo ya moyo hawezi tena kucheza soka.
  Hata hivyo, Yanga ilimchukua na ameweza kucheza vizuri kiasi cha kurejeshwa timu ya taifa, ambako amekuwa chaguo la kwanza la kocha Marcio Maximo katika safu ya kiungo wa ulinzi.
  Nyota huyo alizaliwa Julai 7, mwaka 1988 eneo la Soweto mjini Arusha na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Meru kabla ya kujiunga na Sekondari ya Bondeni alikosoma hadi Kidato cha Nne.
  Kama ilivyo kwa nyota wengi nchni, Nurdin naye alianza na soka ya chandimu na kuendelea hadi akiwa shule, kabla ya kuanza kuchezea klabu za mtaani.
  Klabu zake za awali zilikuwa ni Soweto Kids, Kaloleni Rangers Kids na Mandela Kids zote za Arusha.
  Mwaka 2002, akiwa na umri wa miaka 14 alisajiliwa na klabu ya AFC ya Arusha iliyokuwa Ligi Kuu na mwaka mmoja baadaye aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17.
  Mwishoni mwa mwaka huo huo 2003 pia alisajiliwa na klabu ya Simba ya Dar es Salaam kwa ajili ya msimu wa 2004, ambayo aliichezea hadi mwaka 2007 alipohamia kwa watani wa jadi, Yanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NURDIN: MIMI NABAKI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top