• HABARI MPYA

    Thursday, April 02, 2009

    MWALALA AREJEA YANGA AKIWA MGONJWA


    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Kenya, Ben Mwalala (pichani), amerejea Jumatatu jioni mjini Dar es Salaam kujiunga na klabu yake, Yanga, kwa ajili ya mchezo wa marudiano raundi ya awali, Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Al Ahly ya Misri, lakini akiwa hana matumaini ya kucheza kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.
    “Nimerudi, lakini siko fiti, niliumia kwenye mazoezi, hata mechi ya Jumamosi sijui kama nitacheza,” alisema Mwalala, katika mahojiano na DIMBA jana mjini Dar es Salaam, baada ya kurejea kutoka Nairobi, alikokwenda kuichezea timu yake ya taifa, Harambee Stars, iliyofungwa 2-1 na Tunisia, katika mchezo wa kuwania kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, Afrika Kusini.
    Mbali na Mwalala, wachezaji wengine wa Yanga waliokuwa Kenya ni beki George Owino na mshambuliaji Boniphace Ambani, ambao wote walicheza dhidi ya Tunisia Jumamosi. Mwalala aliukosa mchezo huo baada ya kuumia mazoezini.
    Wakati Yanga ikipata habari mbaya kuhusu mshambuliaji huyo mwenye kasi uwanjani, Ahly nayo ilipata pigo baada ya nyota wake, Ahmed Hassan, kuumia mguu, alipoichezea timu yake ya taifa, Misri, katika mechi ya kuwania kucheza fainali za Afrika Kusini dhidi ya Zambia mjini Cairo, ambao ulimalizika kwa sare 1-1.
    Kiungo huyo wa zamani wa Anderlecht ya Ubelgiji, ndiye aliyetoa pasi murua ya sekunde ya kwanza iliyomfikia Mohamed Barakat na kuandika bao la mapema siku walipocheza na Yanga mjini Cairo, wakati mabingwa wa Tanzania wakilala 3-0.
    Mbali na huyo, wachezaji wengine nyota wa timu hiyo, Ahmed Sedik, Sayed Moawad, Shadi Mohamed, Gilberto na Flavio nao wako chini ya uangalizi maalumu kutokana na sababu mbalimbali.
    Jumamosi iliyopita, Ahly, iliyotaka kutumia mapumziko ya Ligi Kuu ya nchi hiyo kwa maandalizi dhidi ya Yanga, ililazimika kufuta mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya daraja la pili ya Canal Mooring & Lights (CML) kutokana na ukweli kuwa wachezaji wake wengi hawako sawasawa kimchezo.


    Yanga SC: Tulificha makucha
    kwa ajili ya Al Ahly Jumamosi

    KOCHA wa Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Kondic amesema hakutaka wachezaji wake wacheze kwa nguvu katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo tayari wamekwishatwaa ubingwa, ili kuhifadhi nguvu zao.
    Katika mahojiano maalum na DIMBA juzi usiku, hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam, Profesa Kondic alisema kwamba akili yake yote ipo kwenye mechi dhidi ya mabingwa mara sita Afrika, Al Ahly, kwani amedhamiria kuwang’oa kwenye mchezo wa marudiano Jumamosi hii, Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa, Dar es Salaam.
    “Sikutaka wachoke sana, hapa walipo wamechoka hawa vijana, wametumika sana, hawakuwa na muda kupumzika, niliwaambia wacheze pole pole, hii tangu Mwanza (kwenye mechi dhidi ya Toto),”alisema.
    Kondic alisena anajua wapinzani wake hao katika Raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, watakuja kucheza kwa nguvu katika mechi hiyo ya marudiano kulazimisha bao la mapema ili kuivuruga timu yake kisaikolojia, lakini amejiandaa kwa hilo.
    Alisema Yanga ipo tayari kwa mchezo wa marudiano na matarajio ya kupata matokeo mazuri, siku hiyo.
    “Tulipoteza mchezo wa kwanza, hayo ni matokeo ya mpira wa miguu, nasikitika wachezaji wangu watakuwa wana kazi ngumu mno, kuzuia na kushambulia kutafuta mabao, tumejipanga kwa hilo, siwezi kukueleza kila kitu, utaona mambo Jumamosi,”alisema Kondic.
    Kondic alisema wachezaji wake waliokuwa wagonjwa hivi sasa wamepona na wengine aliwapumzisha makusudi kwenye mechi za Ligi kama Nsajigwa Shadrack ili warejee kwenye hali nzuri.
    “Nimekwishasahu kuhusu mchezo wa kwanza, sasa naingia vitani kutafuta ushindi mkubwa na wa kihistoria, najua unajua hakuna lisilowezekana, vijana wapo kwenye ari, na wanataka kufanya mambo makubwa,”aliongeza.
    Yanga baada ya kulala 3-0 kwenye mchezo wa awali wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Ahly, itakuwa na deni la kulipa kisasi hicho kwa ushindi wa 4-0, ili isonge mbele kwenye michuano hiyo au ilazimishe sare kwa kushinda 3-0, ili mshindi aamuliwe kwa mikwaju ya penalti.
    Mabao yaliyoizamisha Yanga kwenye Uwanja wa International mjini Cairo yalitiwa kimiani na Mohamed Barakat mawili na lingine lilifungwa na Muangola, Flavio Amado.
    Katika mechi tano ambazo Yanga imekutana na Al Ahly, imefungwa tatu ugenini na imetoka sare mara mbili nyumbani na ugenini. Mara ya kwanza Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1982, katika michuano hii, enzi hizo ikijulikana bado kama Klabu Bingwa na mchezo wa kwanza mjini Cairo wavaa jezi za njano na kijani walitandikwa mabao 5-0 na mchezo wa pili, uliokuwa wa marudiano mjini Dar es Salaam, walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.
    Mara ya tatu, Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1988 na katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, Aprili 9 mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na kwenye mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo, uliokuwa wa marudiano, Aprili 22, watoto wa Jangwani walitandikwa 4-0.
    Si Yanga tu, hata timu nyingine zote zilizowahi kukutana na Ahly hazikuweza kuvuka, wakiwemo Simba, Pamba FC na Majimaji ya Songea. Mwaka 1985, Simba iliifunga Al Ahly mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, katika michuano ya Kombe la Washindi, kabla ya kwenda kufungwa 2-0 mjini Cairo. Mwaka 1993, Al Ahly iliifunga 5-0 Pamba mjini Cairo katika Kombe la Washindi pia, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Mwanza, wakati mwaka 1999, Waarabu hao walianza kwa kuichapa 3-0 Majimaji ya Songea, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuwaongeza 2-0 mjini Cairo. Na hilo ndilo lilikuwa jicho la mwisho la Watanzania kwa Ahly, ambao wanatarajiwa kuonekana tena nchini wiki mbili zijazo kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

    Santos: Hakuna mwanasoka ‘staa’ Tanzania

    KOCHA wa klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, Neider dos Santos amesema hakuna mchezaji ‘staa’ katika soka ya Tanzania na asitokee yeyote akajidanganya kwa hilo.
    “Tanzania hakuna mchezaji staa, nani niambie amecheza fainali ngapi za Kombe la dunia?”alihoji Santos katika mahojiano na DIMBA juzi, Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa Dar es Salaam.
    Santos alikuwa akijibu swali la mwandishi wa DIMBA kwa nini hamtumii kwenye kikosi chake mchezaji nyota wa nafasi ya kiungo, Shaaban Kisiga ‘Malone’.
    Akiuzungumzia mchezo wa juzi kwa ujumla, ambao timu yake ilichapwa 3-0 na Simba katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Mbrazil huyo alisema kwamba wapinzani wake walitumia mwanya wa kadi nyekundu, aliyopewa beki wake, Cyprian Odura.
    “Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza, nilikuwa ninajua Simba watakuwa kushambulia kwa nguvu kwa sababu wanataka nafasi ya pili, nikaamua nitumie mfumo wa kuwabana sana na kushambulia kwa kushitukiza.
    Lakini bahati mbaya ilikuja baada ya beki wangu kupewa kadi nyekundu,”alisema Santos aliyekuwa kocha wa Simba, msimu wa 2006/2007.
    Hata hivyo, Santos alisema kwa sababu ana uhakika wa kubaki Ligi Kuu, msimu ujao anaamini atakuwa na timu nzuri, kwani ameandaa vijana wadogo kwa ajili ya kuunda Azam ya 2010.
    “Kuna vijana wadogo kama Tumba Luois Sued na Himid Mao, nimekwishaanza kuwatumia, wapo na wengine naowandaa pia, nataka kutengeneza Azam kali ya baadaye,”alisema.
    Santos alisema kwamba ni vigumu kwa timu kupanda Ligi Kuu na moja kwa moja kuwa juu kwenye msimamo, hivyo Azam itaanza kuonyesha cheche zake kuanzia msimu ujao.


    Chuji atamani kurudi darasani

    KIUNGO wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Athumani Iddi Athumani ‘Chuji’, amesema kwamba kwa sasa anatamani kurudi kuendelea na masomo, kwani alikomea kidato cha Nne.
    Akizungumza kwenye kambi ya klabu hiyo, Tamal Hotel, Mwenge mjini Dar es Salaam, Chuji alisema kwamba akitokea mtu wa kumsomesha kwa sasa atakubali mara moja.
    “Mimi rafiki yangu akitokea mtu sasa hivi aniambie ananipeleka shule, naenda tu, yaani nataka sana kurudi darasani,”alisema kiungo huyo wa zamani wa Polisi Dodoma na Simba ya Dar es Salaam.
    Chuji ambaye amekuwa na desturi ya kufanya mazoezi ya zaida wakati mwingine akidamka alfajiri ili kujiweka fiti zaidi kisoka, alisema kwamba pamoja na kufikiria kufika mbali kisoka, ikiwemo kucheza Ulaya, lakini elimu pia anaipa umuhimu mkubwa.
    Chuji na kiungo mwingine wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ wamekuwa wakitawala vichwa vya habari kwenye magazeti kutokana na kutibuana na kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Mbrazil Marcio Maximo, Februari mwaka huu nchini Ivory Coast timu hiyo ilipokwenda kushiriki Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).
    Katika fainali hizo ambazo Stars ilitolewa kwenye raundi ya Kwanza katika Kundi A, ikizidiwa pointi moja na Zambia na Senegal zilizofuzu, Chuji na Boban walijikuta wanageuka watalii nchini humo kutokana na kutochezeshwa baada ya kutibuana na Maximo, aliyewatuhumu kwa utovu wa nidhamu.
    Chuji aliyezaliwa Februari 18, mwaka 1988 mjini Tanga ni miongoni mwa wachezaji wa Tanzania wanaotarajiwa kupata timu za kuchezea Ulaya wakati wowote kutokakana na soka yao muruwa uwanjani.

    Mgosi atinga kambini Yanga

    KATIKA siku ambayo Simba ilikuwa inamenyana na Azam FC, Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, saa chache kabla, kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mussa Hassan Mgosi alikuwa kwenye kambi ya watani wa jadi, Yanga, Hotel ya Tamal, Mwenge mjini Dar es Salaam akimjulia hali swahiba wake, kipa Juma Kaseja.
    Mgosi ambaye hakushiriki mchezo dhidi ya Azam kutokana na kuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro, alifika Tamal Hotel ambako Yanga imeweka kambi kumsalimia Kaseja aliyekuwa na Simba msimu uliopita.
    Wakati wachezaji wa Yanga wakiwa wametulia kambini, wengine ndani ya hoteli, wengine vyumbani na wengine nje ya jengo la Tamal, gari aina ya GX100 iliwasili na kupaki mbele ya miguu yao.
    Baada ya hapo, mmoja kati ya wachezaji 18 walioteuliwa kwenye kikosi cha nyota wa Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), iliyomalizika Ivory Coast, Februari mwaka huu, alitoa shingo yake nje na kusalimia.
    Wakati huo ni kama ilikuwa tayari amekwishamjulisha kipa wa Yanga, Kaseja kama amefika nje ya jengo la Tamal, kwani wakati akiendelea na mazungumzo na wachezaji wengine wa kjlabu hiyo, Kaseja alitokea na kuanza kuteta na swahiba wake siku nyingi.
    Baada ya mazungumzo yao, Mgosi aliwaaga wachezaji wa Yanga waliokuwa nje, akagaeuza gari lake na kuondoka zake.
    Mgosi na Kaseja ni marafiki walioshibana, walianza tangu wanasoma sekondari ya Makongo na kisoka waliinuka pamoja, ingawa kipa wa Yanga alianza kufanikiwa.
    Waliteuliwa pamoja timu ya vijana chini ya umri wa miaak 17, mwaka 2001 enzi hizo ikinolewa na Mnigeria, Ernest Mokake (sasa marehemu) na wakati Kaseja anachukuliwa Moro United, Mgosi alienda JKT Ruvu.
    Baadaye Mgosi alihamia Mtibwa Sugar 2004 wakati Kaseja alichukuliwa na Simba mwaka 2002, misimu mitatu baadaye, yaani 2005 nyota wa CHAN naye alitua Msimbazi. Hata hivyo, Kaseja alifungasha viragio vyake msimu huu na kuhamia Yanga.


    Kisiga atupiwa virago Azam

    HAMKANI si shwari kwa kiungo wa zamani wa kimataifa Tanzania, Shaaban Kisoga ‘Malone’, kwani ni kama amekwishatupiwa virago kwenye klabu yake, Azam FC baada ya kutofautiana na kocha, Neider dos Santos wa Brazil.
    Kiongozi mmoja wa juu wa Azam, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, aliiambia DIMBA kwamba Santos hampendi Kisiga na hamtaki.
    “Yupo, lakini kocha hamtaki, eti anasema hana nidhamu,”alisema kiongozi huyo alipoulizwa na mwandishi wa DIMBA kuhusu Kisiga.
    Ingawa Kisiga hakupatikana kuzungumzia mustakabali wake kwenye timu hiyo, lakini DIMBA ilipozungumza na Santos alisema: “Yupo, ni mchezaji wa Azam,”.
    Alipoulizwa kwa nini hamtumii kwenye mechi za Ligi Kuu karibu tangu mzunguko wote wa pili ulipoanza, alisema: “Nina wachezaji 30, siyo lazima yeye acheze,”.
    DIMBA: Lakini infahamika Kisiga ni mchezaji mzuri, kama yuko fiti kwa nini hachezi?
    Santos: Kama mzuri mbona hayupo timu ya taifa, muulize Maximo
    DIMBA: Kuna tatizo lolote kati yako na yeye
    Santos: Hapana
    DIMBA: Kwa nini hachezi naye ni staa
    Santos: “Tanzania hakuna mchezaji staa, nani niambie amecheza fainali ngapi za Kombe la dunia?”
    DIMBA:vipi msimu ujao utabaki naye kwenye timu?
    Santos: sifahamu


    Santos afanya kama Kondic Cairo

    KOCHA wa Azam FC, Neider dos Santos Jumtatu wiki hii alifanya kitu kama anachodaiwa kufanya kocha wa Yanga, Profesa Dusan Kondic kwenye mchezo wa awali wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji Al Ahly mjini Cairo.
    Mjini Cairo, Kondic alikwenda kumkumbatia mchezaji wa Al Ahly, Flavia Amado wakati wa mapumziko, walipokutana njiani kuelekea kwenye vyumba vya kupumzikia, wakati huo Al Ahly inaongoza 2-0.
    Tukio hilo lilizua gumzo kwa wapenzi wa Yanga wamshutumu Kondic kwa nini alifanya hivyo, lakini juzi baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Santos alidhihirisha kwamba hayo ni mambo ya kiunamichezo.
    Baada ya mchezo huo, Azam ikiwa imetota 3-0, Santos akiwa anatoka nje alikutana na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ na wakakumbatiana na kusalimiana kwa shangwe, tukio ambalo liliwafanya mashabiki wachache waliokuwa wamebaki uwanjani kushangilia.
    Santos alikuwa kocha wa Boban Simba msimu wa 2006/2007 kabla hajarejea kwao Brazil alipomaliza mkataba wake. Ni msimu huu Santos amerejea Tanzania akihamia Azam FC.


    Barthez ataka jezi yake Stars

    KIPA wa Simba, Ally Mustafa ‘Barthez’, baada ya kurejesha namba yake kwenye kikosi cha Simba ya Dar es Salaam, sasa amedhamiria pia kurejesha na nafasi yake kwenye timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
    Akizungumza na DIMBA mjini Dar es Salaam baada ya kuiongoza Simba kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam FC, Barthez alisema kwamba amefurahi sasa ni kipa wa kwanza wa klabu yake tena.
    “Kwa kweli nimefurahi kuona naaminiwa tena kwenye timu yangu, kiu yangu ni kupata mafanikio zaidi na kurejeshewa nafasi yangu kwenye timu ya taifa pia,”alisema Barthez.
    Barthez amepokonywa nafasi yake timu ya taifa na kipa mwenzake wa Simba, Deo Munishi ‘Dida’. Dida alimfanya Marcio Maximo aghairi kumuita Barthez Stars, baada ya kuanza kupangwa mfululizo kwenye mechi za Simba.
    Hata hivyo, mambo yalianza kugeuka kwa chipukizi huyo kwenye mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Vancouver Whitecaps ya Canada alipotunguliwa mabao mawili ya kizembe, hivyo Mzambia Patrikc Phiri kuamua kumuingiza Barthez, aliyedaka vizuri.
    Tangu siku hiyo, lango la Simba limerejeshwa kwa Barthez tena, aliyeiongoza Smba katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Mtibwa Sugar na Azam FC. Mechi dhidi ya Mtibwa, Simba ililala 1-0 mjini Morogoro.


    MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM:
    P W D L GF GA GD Pts
    YANGA 18 15 2 1 33 8 24 47
    SIMBA 18 9 3 6 25 19 6 30
    KAGERA 18 8 4 6 17 15 2 28
    MTIBWA 18 8 4 6 24 16 8 28
    PRISONS 18 8 4 6 19 22 -5 28
    JKT RUVU 17 6 6 5 25 21 4 24
    TOTO 18 7 3 8 18 19 -1 24
    AZAM FC 18 6 4 8 24 25 -1 22
    POLISI MORO 18 5 7 6 20 18 2 22
    MORO UTD 17 3 6 8 23 24 -1 15
    VILLA SQUAD 18 4 2 12 14 43 -29 14
    POLISI DOM 18 1 9 8 10 21 -11 12
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWALALA AREJEA YANGA AKIWA MGONJWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top