• HABARI MPYA

  Sunday, April 05, 2009

  KONDIC KUUZA WACHEZAJI 11 YANGA


  KOCHA wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Kondic (pichani kulia) amesema kwamba baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika sasa ana mipango miwili mikubwa, ambayo ni kuuza wachezaji na kuanza kutengeneza timu ya msimu ujao.
  Katika mahojiano maalum na bongostaz New Africa Hotel, mjini Dar es Salaam jana usiku, kocha huyo raia wa Serbia alisema kwamba tayari ana ‘dili’ za kuuza wachezaji 11, sita zikiwa za uhakika zaidi.
  Aliwataja wachezaji walio sokoni zaidi kuwa ni kipa Mserbia Obren Curkovic anayetakiwa Austria, mabeki Nsajigwa Shadrack anayetakiwa Albania, Nurdin Bakari, George Owino wanaotakiwa Serbia, kiungo Mrisho Ngassa anayetakiwa Uingereza, Israel na nchi Scandinavia na mshambuliaji Boniphace Ambani anayetakiwa China.
  “Hawa ninaokuambia mambo yao yako safi kabisa, lakini kuna wengine wanne nao mipango iko katikat hadi sasa, najua nikiuza hawa wachezaji nitaiingizia Yanga fedha nyingi na tutapata fedha za wachezaji wengine imara kwa ajili ya msimu ujao,”alisema kocha huyo wa zamani wa Primiero de Agosto ya Angola.
  Kondic aliwataja wachezaji wengine kuwa ni Mike Barasa, Hamisi Yussuf na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wanaotakiwa Canada, wakati Jerry Tegete na Kiggi Makasy alisema muda si mrefu atajua wanakwenda wapi, amekwishawaombea nafasi kadhaa.
  Mbali na mpango huo, Kondic alisema kwamba pia ameanza mchakato wa kutengeneza timu ya msimu ujao na katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo tayari klabu yake imekwishatwaa ubingwa, atakuwa akiwapa nafasi chipukizi zaidi.
  Alisema anao chipukizi watano aliowatoa timu B, ambao amewapandisha kikosi cha kwanza na wataanza kuonekana kwenye mechi za Ligi Kuu.
  Aliwataja chipukizi hao kuwa ni viungo Nurdin Msigwa, Razack Khalfan na mshambuliaji Iddi Mbaga ambao wapo kwenye usajili wa kikosi cha kwanza msimu huu, wakati wengine aliwataja kwa jina moja moja tu, Sunday na Edward.
  “Edward ni kiungo na Sunday ni mshambuliaji, nilikwishaanza kuwaunganisha na kikosi cha kwanza mara moja moja, ila sasa watajiunga rasmi moja kwa moja,”alisema.
  Aidha, Kondic alisema kwamba atazitumia pia mechi zilizobaki za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kujua ni wachezaji gani anastahili kubaki nao kikosini baada ya wale anaowauza na kufanya tathmini ya wachezaji anaowataka kutoka timu nyingine, ikiwemo nje ya nchi.
  “Pamoja na matatizo, bado nina mipango mizuri tu ya kuifanya Yanga iwe zaidi ya hapa, hakuna ubishi kwa hapa Tanzania sisi ndio timu bora, kocha wa Ahly aliniambia, Yanga ni moja ya timu tano bora za Afrika, tumewapa ushindani wa kweli na wametuheshimu.
  Kwangu msimu utaisha siku tunacheza mechi ya mwisho, baada ya hapo ni moja kwa moja kuanza mikakati ya msimu mpya, kwa misimu hii miwili nimejifunza mengi Tanzania,”alisema Kondic anayesaidiwa na Waserbia wenzake, Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan.
  Wakati Ligi Kuu inaelekea ukingoni, Yanga tayari imekwishatwaa ubingwa, kutokana na kufikisha pointi ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote, 47, kwani zote zikijitutumia zitafikisha 45 tu.
  Yanga iliyotolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, Raundi ya Kwanza na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-0, imebakiza mechi nneza Ligi Kuu, ambazo ni dhidi ya Azam mjini Dar es Salaam, keshokutwa, Polisi mjini Dodoma Jumamosi, watani wao wa jadi, Simba ama Aprili 19 au 23 na Villa Squad Aprili 26.
  ...Yanga, Ahly waingiza Mil 182
  MCHEZO wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly ya Misri umeingiza Sh 182, 787,000 na Yanga kupata Sh 100, 532, 850, wachezaji wa timu hiyo hawatopata kitu, imefahamika. Kulingana na mchanganuo uliotolewa jana na Katibu Mkuu wa Yanga ya Dar es Salaam, Lucas Kisasa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ni kuwa makisio ya Yanga ilikuwa kupata Sh 305, 440,000 kama wangeuza tiketi zote 55,748. Hata hivyo alieleza kuwa tiketi zilizouzwa ni 43,481 na kwamba katika mgawanyo huo Uwanja wa Taifa ulipata Sh 36,557,400, ambazo ni sawa na asilimia 20 ya mapato na Sh 18,278,700 zilikuwa gharama za mchezo ambazo ni asilimia 10. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilipata asilimia 10, ambazo ni Sh 18,278, 700 huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF), likikusanya Sh 9,139, 350 ambazo kwa mujibu wa Kisasa ni sawa na asilimia tano ya mapato na Yanga imepata asilimia 55 ambayo ni Sh 100, 532, 850. Hata hivyo Kisasa hakuzungumzia suala la mgawanyo wa mapato hayo kwa wachezaji wao, wakati wa mkutano huo, lakini alipobanwa nje ya mkutano, alieleza kuwa suala la wachezaji ni mambo ya ndani ya klabu. Lakini wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wachezaji wa Yanga walisema licha ya kuingiza fedha hizo wao hawatapewa chochote kutokana na kufungwa bao 1-0 katika mchezo huo. "Viongozi wameweka utaratibu kwamba timu ikishinda kuna asilimia ya mapato tunachukua, pia tukitoka sare nayo tunachukua asilimia fulani, lakini tukifungwa hatuchukui chochote. "Hilo halina ubishi kwamba tumeumia, lakini tunajaribu kuwashawishi viongozi wetu watutizame katika hili, maana kama zimeingia Sh milioni 100, tunapaswa angalau kufikiriwa, maana tumepambana sana, ila bahati haikuwa yetu," alisema mchezaji mmoja mwandamizi na kuungwa mkono na wenzake. Naye mchezaji mwingine mahiri wa timu hiyo aliyejijengea jina katika muda mfupi, alisema mfumo wa asilimia huwa unawaumiza na kueleza kuwa wana imani kulingana na mapato yaliyopatikana mwishoni mwa wiki, wachezaji watafaidika vya kutosha na kueleza kuwa mapato ya Uwanja wa Taifa ni tofauti na Uwanja wa Uhuru, kwani idadi ya watazamaji inatofautiana. Hata hivyo wachezaji hao wa Yanga walitofautiana kuhusiana na asilimia ambazo wanapata kama wakishinda, ambapo baadhi walisema ni asilimia 60, huku wengine wakisema asilimia 30 ya mapato na kwamba timu ikitoka sare ni asilimia 10. Wachezaji hao walipewa Sh 500,000 kila mmoja ikiwa ni motisha kabla ya mchezo wa Jumamosi. Alipotafutwa baadaye Kisasa, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa na alipotafutwa Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega, atoe ufafanuzi, alisema alikuwa nje ya Dar es Salaam na asingeweza kutoa msaada wowote kwa wakati huo, kwani hakuwa akielewa kinachoendelea. Lakini jana, Katibu huyo alikaririwa na gazeti moja akisema klabu hiyo ilitumia zaidi ya Sh milioni 100 kwa maandalizi ya mchezo huo, ambapo ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 4-0 na Al Ahly ya Misri, baada mchezo wa kwanza kufungwa mabao 3-0 na ziliporudiana ilifungwa bao 1-0 na kwamba ilikuwa na madeni.Viingilio katika mchezo huo vilikuwa Sh 30,000, Sh 20,000, Sh 5,000 na Sh 3,000. Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema polisi wawili walikamatwa wakituhumiwa kulangua tiketi za Sh 3000 katika mchezo huo na kwamba wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi. Katika hatua nyingine, Yanga leo inarejea katika Ligi Kuu Tanzania Bara, itakapocheza na Azam FC katika mfululizo wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Yanga ambayo tayari imeshatwaa ubingwa ikiongoza ligi ikiwa na pointi 47, inakutana na timu iliyopo nafasi ya tano kutoka chini katika msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 22 na ipo katika hatari ya kushuka daraja. Ni wazi mchezo huo utakuwa na ushindani wa aina yake, hasa baada ya Azam kufungwa mabao 3-0 na Simba katika mchezo wake wa mwisho, wakati Yanga ilifungana bao 1-1 na Kagera Sugar. Kama Azam itafungwa leo itakuwa imejiweka katika nafasi mbaya kwenye janga la kushuka daraja, kwani timu za Polisi Dodoma, Moro United na Villa Squad zinazoshika nafasi za chini katika msimamo, zinaweza kuzipita pointi za Azam kama zikishinda michezo yao iliyobaki. Timu tatu za chini zitashuka daraja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KONDIC KUUZA WACHEZAJI 11 YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top