• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 10, 2009

  ETI KIPIGO CHA AZAM KIMEMUUMA SANA KISASA YANGA


  KATIBU Mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa amesema kipigo ilichokipata timu yake kutoka kwa Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara juzi, ni cha aibu. Yanga, ambayo tayari imeshatwaa ubingwa wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47, juzi ilichapwa mabao 3-2 na Azam katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu, mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Akizungumza na gazeti hili jana, Kisasa alisema alikasirika baada ya matokeo hayo, kwani alitarajia timu yake isingepoteza mechi hata moja baada ya kutwaa ubingwa. “Nilikasirika sana sikufichi, ni aibu kufungwa mabao matatu, hata kama tumefungwa 3-2 lakini mabao hayo ni mengi, hata kocha (Dusan Kondic) alikasirika sana,” alisema Kisasa. Alisema, lengo lilikuwa kumaliza ligi wakiwa wamefikisha pointi 60 na kwamba walipanga kumaliza msimu wakiwa wamefungwa mechi moja dhidi ya Kagera Sugar. “Lakini hilo ni funzo, sasa naona wachezaji wamejifunza haiwezekani wewe mwenzako anataka kushuka daraja halafu unamlegezea, ile mechi ilikuwa muhimu sana kwa Azam maana wakicheza watashuka daraja,” alisema. “Yanga ilicheza vizuri lakini mwishoni wakalegeza na hayo ndio matokeo yake sasa, lakini hatufungwi tena na hivi leo (jana) tunaenda Dodoma,” alisema. Aidha Kisasa alisema si kweli kama baadhi ya watu wanavyodai kwamba mechi hiyo ilikuwa hujuma. “Niamini, hakuna mchezaji wa Yanga aliyehujumu mechi, nakwambia kama wangehujumu mimi nawajua wachezaji, ningegundua tu, kwanza ukiwaona hata wao waliumia sana,” alisema. Yanga kesho inatarajiwa kucheza na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo. Kwa ushindi wa Azam, timu hiyo sasa inaanza kujinasua kwenye timu zitakazoshuka daraja kwani sasa iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi ikiwa imefikisha pointi 25. Timu zilizo kwenye hatari zaidi ya kushuka daraja ni Moro United yenye pointi 16, Polisi Dodoma na Villa Squad zenye pointi 15 kila moja. Timu zinazoshuka daraja ni tatu. Polisi Moro inashika nafasi ya nne kutoka chini ikiwa na pointi 22. Naye Evance Ng’ingo anaripoti kuwa timu za JKT Ruvu na Prisons ya Mbeya jana zilifungana bao 1-1 katika mchezo wa ligi hiyo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. JKT Ruvu ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 25 mfungaji akiwa Greyson Haule kwa shuti kutokana na pasi ya Bakari Kondo. Prisons ilisawazisha dakika ya 73 mfungaji akiwa Summa Ado kwa njia ya penalti baada ya Yona Ndabila kuchezewa madhambi. Kwa matokeo hayo, JKT Ruvu imefikisha pointi 26 ikishika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi, wakati Prisons imefikisha pointi 29 ikiwa nafasi ya tatu.(IMETOKA GAZETI LA HABARI LEO)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ETI KIPIGO CHA AZAM KIMEMUUMA SANA KISASA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top