• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 07, 2009

  POLISI WAKAMATWA KWA KULANGUA TIKETI ZA YANGA NA AL AHLY

  ASKARI Polisi wawili wametiwa mbaroni jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za ulanguzi wa tiketi za mchezo wa Yanga na Al Ahly uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
  Katika mchezo huo, Sh182,787,000 zilipatikana na Yanga kuchuma Sh100,532,850 kati ya hizo kutokana na pambano hilo la Jumamosi iliyopita.
  Wawakilishi hao wa Tanzania walijikuta wakishindwa kuhimili vishindo vya Waarabu na kulazwa bao 1-0 na kusukumiwa nje ya michuano ya Afrika kwa maba0 4-0.
  Askari hao waliokuwa wakisimamia uuzaji wa tiketi za mchezo huo, kituo cha Ubungo wanashikiliwa makao makuu ya jeshi hilo baada ya kukamatwa wakijihusisha na ulanguzi wa tiketi hizo ambazo walizinunua kwa Shilingi 3,000 na kuziuza kwa Shilingi 3,500 na 4,000.
  Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela alisema jana kuwa shirikisho lake limewasilisha majina ya askari polisi hao na namba zao kwa mwajiri wao na tayari wameshaanza kuhojiwa kutokana na kujihusisha na ulanguzi huo wa tiketi, kitendo ambacho kimetafsiriwa kama hujuma.
  Siku moja kabla ya mchezo huo, uongozi wa Yanga kupitia kwa katibu mkuu wake, Lucas Kisasa ulitahadharisha watu kutojihusisha na ulanguzi wa tiketi na kueleza kuwa atakayepatikana atajuta kuifahamu dola.
  Kauli hiyo ya Kisasa, kwa mujibu waTFF ilionekana kupuuzwa na askari hao ambao walipewa jukumu la kuhakikisha wanadhibiti vitendo hivyo ikiwemo kulinda amani sehemu za uuzaji wa tiketi.
  "Polisi ndio tunaowategemea katika kutulindia tusihujumiwe mapato, lakini ndio hao hao baadhi yao wamekuwa si waaminifu wamekuwa mstari wa mbele kutuhujumu, tutahakikisha hao waliokamatwa watakuwa mfano wa wenzao wenye tabia kama yao kuacha," alieleza kiongozi huyo wa TFF.
  Wakati huo huo, shirikisho hilo limelaani kitendo cha mashabiki wa Simba kuishangilia Al Ahly wakati wa mchezo wao dhidi ya Yanga na kudai kuwa wamekosa moyo wa kizalendo.
  "Ni kweli mashabiki wanao uhuru wa kushangilia timu wanayoipenda, lakini wenzetu hawa walivuka mpaka na kupitiliza wakafikia hatua ya kubeba hata bendera ya nchi ya wenzetu (Misri), kitendo kile si cha kiuanamichezo.
  "Kuna wakati pamoja na kwamba kila mtu ana uhuru wa kushangilia timu anayoitaka inapofika suala la utaifa, lazima busara itumike zaidi,"alisema Mwakalebela.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: POLISI WAKAMATWA KWA KULANGUA TIKETI ZA YANGA NA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top