• HABARI MPYA

    Tuesday, April 14, 2009

    KONDIC ANATISHIWA MAISHA YANGA


    KOCHA wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Profesa Dusan Kondic (pichani akiwa Flavio wa Angola) amesema kwamba kuna watu wanamtumia ujumbe wa maandishi (sms) na kumpigia simu za vitisho, jambo ambalo linamfanya ajifikirie kama kuna haja ya kusaini mkataba mpya na klabu hiyo au la.
    Katika mahojiano maalum na bongostaz jana, Hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam, Kondic alisema kwamba ametunza namba na simu anazopigiwa kupewa vitisho na sms anazotumiwa pia, kwamba aliihujumu Yanga dhidi ya Al Ahly.
    “Sikufichi, hata Obren (Curkovic) nadhani ameondoka kwa sababu hii, yeye alikuwa anapigiwa simu na kutukanwa na watu, wanamuambia ondoka hatukutaki Yanga umehujumu timu yetu. Hata Serdan (Civojnov) pia, naye alikuwa anapigiwa simu kupewa vitisho,”alisema.
    Kondic alisema kweli Obren yupo kwenye mpango wa wachezaji 11 wa kuuzwa Ulaya na Yanga, lakini ilikuwa aondoke baada ya kumaliza mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ila kutokana na vitisho ameamua kuondoka.
    “Obren ameondoka, ni kipa mzuri sana, amedaka mechi kumi za Ligi Kuu, amefungwa goli moja tu, nani mwingine kwenye ligi hii amefanya hivyo?”alihoji Kondic kuhusu kipa huyo Mserbia mwenzake.
    Kondic alisema mkataba wake na Yanga unaisha Novemba mwaka huu, lakini kwa sasa hana jibu kama atasaini tena au la, ila kabla ya kufika kipindi hicho atakuwa amekwishajua hatima yake.
    “Kuna wengine wengi wananipenda, wananiambia, watu wabaya kwenye Yanga ni wapi, wananiambia haya ndio matatizo ya kufanya kazi Tanzania, wanasema nivumilie, na nikae nikujua yataendelea tu, yote nayafikiria, kwa sababu kuna timu nyingine zinanitaka.
    Nina ofa za wazi tatu, tena nzuri, lakini ninapenda kuisaidia Yanga, ila baadhi ya watu wananikatisha tamaa, hapa nilipo ninaumwa malaria wiki ya pili ya sasa, lakini ninafanya kazi hivyo hivyo.
    Ila mimi ni mkongwe na mwanataaluma, nimebobea, naangalia mkataba wangu kwanza, nimeipa Yanga ubingwa mara mbili mfululizo, tangu nimefika hapa sijafungwa na Simba, mechi ya kwanza tulitoka sare, ya pili nikawafunga. Najiamini kwa kazi yangu,”alisema kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Angola na klabu ya Primiero de Agosto ya nchini humo.
    Obren alikuwa kipa wa Yanga wakati Serdan alikuwa kocha msaidizi ambao waliondoka wiki iliyopita kwenda kwao Serbia. Wakati anaondoka Obren alisema baadaye atakwenda Austria kufanya majaribio kwenye klabu moja ya huko.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KONDIC ANATISHIWA MAISHA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top