• HABARI MPYA

  Jumatatu, Aprili 13, 2009

  JABIR AZIZ AIBEBA SIMBA


  BAO lililofungwa na kiungo wa ulinzi, Jabir Aziz (pichani) katika dakika ya 89, jana liliipa Simba pointi tatu muhimu baada ya kuilaza Toto Afrika ya Mwanza 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliokuwa mtamu kupita maelezo ambao ulifanyika Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ulikuwa ni mchezo wa pande zote, timu zikishambuliana kwa zamu tangu mwanzo, ingawa Toto ndio walioonekana kulijaribu lango la wenyeji mara nyingi zaidi.
  Hata hivyo, Toto walishindwa kuendeleza makali yao baada ya kupata pengo la mchezo wao, Juma Seif kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje kwa kadi nyekundu mapema kipindi cha pili, hivyo Simba kuanza kulisakama kama nyuki kwenye mzinga lango la vijana hao wa Mwanza.
  Sifa ziwaendee makipa wa timu zote, Hamisi Msafiri wa Toto na Ally Mustafa ‘Barthez’ ambao waliokoa mabao kadhaa ya wazi kwenye mchezo huo. Kwa matokeo hayo, Simba sasa imetimiza pointi 36 hivyo inangoja kushinda mechi zake mbili za mwisho, dhidi ya Yanga na Polisi Dodoma ili kujihakikishia nafasi ya pili.
  Huo ulikuwa mchezo wa marudiano wa ligi hiyo na katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Simba ilichapwa 4-1.


  REKODI YA SIMBA NA TOTO:
  Aprili 12/2009
  Simba Vs Toto 1-0
  MFUNGAJI: Jabir Aziz dk 89
  Okt 19/2008
  Toto Afrika Vs Simba 4-1
  WAFUNGAJI:
  Toto: Hamisi Msafiri dk. 8, Juma Seif dk. 28 Oscar Samuel dk. 44, Said Dilunga dk. 79
  Simba: Orji Obina dk. 88
  Apr 14/2008
  Simba Vs Toto Afrika 3-0
  WAFUNGAJI: Moses Odhiambo dk. 12, 45pen, Mohammed Kijuso dk. 51.
  Okt 28/2007
  Toto Afrika 3-2 Simba
  WAFUNGAJI:
  Toto: Philipo Alando dk. 45, 59, Said Kokoo 57(alijifunga);
  Simba: Joseph Kaniki 79, Haruna Moshi 90
  (Toto ilirejea Ligi Kuu msimu wa 2006/2007 na tangu hapo imekuwa mwiba mkali kwa Simba)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: JABIR AZIZ AIBEBA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top