• HABARI MPYA

    Saturday, April 04, 2009

    YANGA USHINDI TU LEO DHIDI YA AL AHLY


    HAKUNA kingine!, kwa Yanga zaidi ya ushindi wa mabao 4- 0 ili iweze kusonga mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakapoivaa Al Ahly ya Misri leo.
    Mchezo huo wa marudiano baada ya ule wa awali Yanga kuchapwa mabao 3 - 0 nchini Misri, utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam majira ya saa 9: 00 alasiri.
    Wingi wa mashabiki wa Yanga wanaoshangilia kwa nguvu bila kuchoka, uimara wa kikosi chenyewe na motisha ya Sh 500,000 waliyopewa wachezaji kabla ya mchezo huo vyote vinaweza vikaisimamisha Al Ahly leo na kuwaacha watu wakishangaa na kutoamini kinachotokea mbele yao.
    Licha ya uimara wa kikosi cha vigogo hao wa Misri, Yanga inaweza ikajitutumua na kufunga mabao manne yatakayowawezesha kusonga mbele katika michuano hiyo na kuifanya Afrika ikipatwa na mshangao.
    Pamoja na kusaka mabao hayo Yanga wanatakiwa kuweka ulinzi mkali langoni kwao na wasiruhusu bao lolote kama kweli wanataka kusonga mbele.
    Mchezo wa leo unaweza ukawa mkali na mgumu kwa pande zote mbili kwani Al Ahly watataka kulinda ushindi wao ili waweze kuendelea katika safari yao ya kusaka ubingwa wa saba Afrika huku Yanga nayo ikitafuta magoli kwa udi na uvumba kuhakikisha wanakata ngebe za waarabu hao.
    Kocha wa Yanga, Dusan Kondic huenda akaanzisha kikosi kile kichoanza Misri, huku nafasi ya golikipa ikiwa na kitendawili kikubwa ni nani adake kati ya Obren Curcovic au Juma Kaseja.
    Watu wengi wamekuwa wakimtaka kocha huyo amwanzishe Juma Kaseja ambaye alifunga bao la umbali wa mita zaidi 82 dhidi ya Toto Afrika na kuipa Yanga ubingwa wa Tanzania Bara mapema.
    Shutuma nyingi alizopewa kipa Msebria, Obren kwamba alikuwa akizurula usiku pamoja na makocha wake kabla ya mechi ya kwanza nchini Misri hali iliyochangia kupata matokeo mabaya, zinaweza zikamshawishi Kondic kumuweka benchi na kumuanzisha Kaseja, lakini uamuzi upo kwa kocha.
    Safu ya ulinzi hapana shaka itaongozwa na Nadir Haroub 'Canavaro' akisaidiana na Wisdom Ndlovu au George Owino ili kuhakikisha washambuliaji Mohamed Barakat, Aboutrika na Flavio hawaleti madhara zaidi, huku Athuman Iddi 'Chuji', Godfrey Bonny na Mrisho Ngassa wakipeleka mashambulizi mbele.
    Mshambuliaji mwenye kasi na anayeongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu Bara, Boniface Ambani ataiongoza vema timu yake kuibuka na ushindi huku akiapa kuwa ni lazima atoke na mabao yake mawili.
    " Hakuna kinachoshindikana mimi nakuambia wale tutawafunga kinachotakiwa ni ushirikiano, watu watashangaa, mimi nina goli zangu mbili lazima nifunge, Mungu anisaidie," alisema
    Naye nahodha wa timu hiyo Abdi Kassim 'Babi' amewataka Watanzania wote kuwaombea ili waweze kuuangusha mti mkubwa ulio mbele yao.
    "Tuna kazi kweli kweli, si mchezo yahitaji moyo, kujituma ari na maombi ya Watanzania naamini kabisa tunaweza wote tukiwa na nia, hakuna linaloshindikana kama ukiweka nia, naamini Mungu atatusaidia na kuweza kushinda na kusonga mbele katika michuano hii.
    Wakati Yanga wakisema hayo kocha wa Al Ahly, Manuel Jose alisema amekuja hapa kukamilisha ushindi wao na lazima waifunge tena Yanga.
    " Hatuidharau mechi hii tunajua itakuwa ngumu kwa sababu wako nyumbani, lakini sisi tumekuja kukamilisha ushindi wetu, hatutabweteka tutacheza kufa na kupona hadi mwisho ili tuweze kusonga mbele," alisema Mreno huyo.(imeandikwa na oliver albert wa mwananchi)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA USHINDI TU LEO DHIDI YA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top