Taddy Etkiama jana Lugogo |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MFUNGAJI
bora wa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Taddy Etikiama
amewaambia Yanga SC ya Dar es Salaam, wasikosee kusajili mshambuliaji mwingine
yeyote zaidi yake, kwani yeye ndiye mkali anayewafaa zaidi.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana mijini hapa, Taddy anayechezea Rwanda katika Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge alisema kwamba huu
ni wakati mzuri Yanga kumsajili, kwani amemaliza mkataba na klabu yake A.S.
Vita ya DRC.
Alisema
anaijua Yanga vizuri na mfumo wake wa uchezaji pia na anaamini akijiunga nayo
atawafungia sana mabao. “Najua wana wapinzani wao wakubwa, Simba, mimi
nikisajiliwa Yanga nitakuwa nawafunga sana hao Simba,”alisema Etikiama na
kuongeza.
“Mimi ni
mkali kweli, nimekuwa mfungaji bora wa Kongo (DRC), nimefunga mabao 15 ligi
yenye timu nzuri kama TP Mazembe, St Eloi Lupopo na DC Motema Pembe,
nimewashinda akina Mbwana Samatta, Yanga wakinipata watapata mchezaji mzuri wa
ushindi,”alisema.
Taddy
alikuwa na A.S. Vita kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati,
Kombe la Kagame, ambayo Yanga iliibuka bingwa.
Katika
mashindano hayo yaliyofanyika mjini Dar es Salaam Taddy alikaribia kuwa
mfungaji bora baada ya kushika nafasi ya pili kwa mabao yake sita, nyuma ya
Said Bahanuzi wa Yanga aliyefunga saba na kutwaa kaitu cha dhahabu cha michuano
hiyo.
Taddy
alifunga idadi sawa ya mabao na mshambuliaji mwingine wa Yanga, Hamisi Kiiza
‘Diego‘, ambaye katika Challenge hii naye anachezea nchi yake, Uganda.