Wachezaji wa Eritrea wakiwa jukwaani Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa wiki iliyopita |
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
WACHEZAJI 14
wa Eritrea wametoweka kambini kwao, baada ya kutolewa kwenye Kombe la Mataifa
ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mjini hapa Jumamosi.
Ofisa Habari
wa Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), waandaaji wa mashindano ya mwaka huu, Rogers
Mulindwa ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, hawakufanikiwa kuwapata wachezaji hao
wakati wanatakiwa kuondoka leo mara tu baada ya kutolewa.
Mulindwa alisema
kambini wamebaki kocha Ngash Teklit na viongozi wengine wanne tu, lakini
wachezaji wote hawapo.
“Wachezaji
14 wametoweka kambini na hatujui walipo kwa sasa. Ndege yao inatarajiwa
kuondoka leo, lakini tunaendelea na jitihada za kuwasaka kwa kushirikiana na
Polisi,”alisema.
Eritrea ilikuwa
kundi moja na Rwanda, Zanzibar na Malawi na wakashika mkia katika kundi hilo,
wakifungwa mechi zote na kutoa sare moja tu Zanzibar katika mechi ya kwanza.
Sasa hii
inakuwa desturi sugu ya nchi hiyo kuzamia nchi za watu wanapokwenda kwenye
mashindano, kwani awali wachezaji wanne walizamia walipokwenda kucheza na Tusker
nchini Kenya kwenye Ligi ya Mabingwa mwaka 2006 mjini Nairobi na wengine zaidi
ya 10 walizamia kwenye michuano kama hii mwaka 2007 mjini Dar es Salaam.
Waliwahi kuzamia
pia walipokwenda Angola mwaka 2007 kucheza mechi ya kuwania kufuzu Fainali za
Kombe la Dunia.
Timu hiyo
ilifanya hivyo hivyo mwaka 2009 nchini Kenya na katika kambi nzima alibaki
kocha na mchezaji mmoja tu. Kutokana na mfululizo wa matukio hayo, walijitoa
kwenye mashindano ya kimataifa mwaka 2010 na mashindano ya mwaka huu ya Challenge
ndio ya kwanza kushiriki baada ya kurudi.
Serikali ya Eritrea
ilisema ili kudhibiti tabia hiyo, kila mchezaji atatakiwa kuweka bondi fedha za
nchi hiyo 100,000 kabla ya kusafiri kwenda kuiwakilisha nchi, lakini hiyo nayo
inaonekana bado haijawa tiba.