• HABARI MPYA

    Sunday, August 12, 2012

    KILA LA HERI NGORONGORO NIGERIA LEO


    Tegemeo la Ngorongoro leo; Ramadhan Singano 'Messi'
    Na Prince Akbar
    TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo inashuka dimbani nchini Nigeria kumenyana na wenyeji, Flying Eagles katika mchezo wa marudiano kuwania tiketi ya kucheza fainali za vijana wa umri huo, mwakani Algeria.
    Ngorongoro iliwasili asubuhi ya juzi kwa ndege ya Overland Airways kwenye mji wa Ilorin, Jimbo la Kwara lililo Kusini mwa 
    Mechi hiyo ya raundi ya pili ya michuano ya U20 ya Afrika itachezwa kwenye Uwanja wa Township kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa hapa ambapo Tanzania itakuwa ni saa 12 kamili jioni. Ngorongoro Heroes ilitua jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Lagos ambapo ililala kabla ya kuja hapa.
    Msafara wa Ngorongoro Heroes wenye watu 27 ukiongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) ulipokea na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria, Jones Mndeme na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF) umefikia hoteli ya Kingstone Grand Suites.
    Chini ya kocha wake, Mdenmark Jakob Michelsen, timu hiyo ilifanya mazoezi juzi na jana jioni kwenye uwanja ambao utatumika kwa mechi ya Jumapili.
    Hadi jana asubuhi, wachezaji wote walikuwa katika hali nzuri isipokuwa Issa Rashid na Aishi Manula ambao waliokuwa wanasumbuliwa na tumbo baada ya timu kufika juzi mijini Nairobi, Kenya ambako ilibadili ndege kuelekea Nigeria. 
    Hata hivyo, ilielezwa jana kwamba hali zao zinaendelea vizuri na huenda wakawa sehemu ya kikosi cha kwanza kitakachoivaa Flying Eagles.
    Mbali ya Rashid na Manula, wachezaji wengine walioko hapa kwenye kikosi cha Ngorongoro Heroes ni Barwany Khomeiny, Samir Ruhava, Dizana Yarouk, Leonard Muyinga, Hassan Ramadhan, Jamal Mroki, Omari Kheri, Frank Domayo, nahodha Omega Seme, Abdallah Kilala, Hassan Dilunga, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Said Zege, Atupele Gren na Ramadhan Salum.
    Mbali ya Michelsen, Benchi la Ufundi linaundwa na Mohamed Rishad 'Adolf' (Kocha Msaidizi), Peter Manyika (Kocha wa makipa), Nassoro Matuzya (Daktari), Joakim Mshanga (Physio), Juma Kizwezwe (Mtunza vifaa) na Meneja wa timu John Lyimo.
    Flying Eagles ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1 nayo ilikuwa ya kwanza kuwasili Ilorin ikitokea Lagos kwa mechi hiyo ambayo matokeo yake yataamua timu ipi itaingia raundi ya tatu ambayo ni ya mwisho kabla ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Algeria. 
    Timu itakayovuka itacheza raundi hiyo na mshindi kati ya Congo Brazzavile na Afrika Kusini.Katika mchezo huo utakaochezwa Jumapili, Ngorongoro inahitaji kushinda 2-0 ili kusonga mbele, baada ya awali kufungwa na Nigeria mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita, mabao ya mshambuliaji wa Enugu Rangers, Achaji Gero katika dakika ya pili na 44.
    Bao la Ngorongoro lililofungwa na mshambuliaji mpya wa Coastal Union ya Tanga, Atupele Green aliyesajiliwa kutoka Yanga B, dakika ya 50, akimalizia krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Ngorongoro wangeweza kupata mabao zaidi kwenye mechi hiyo, kama wangecheza soka ya chini, lakini kutia krosi za juu kwenye lango la Nigeria ilikuwa ni kuwatesa washambuliaji wao wafupi, Atupele na Simon Msuva.
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark Jakob Michelsen alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kuwaita wachezaji wawili wanaocheza nje, kiungo Adam Nditi wa Chelsea na Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), sambamba na nyota wengine waliokwenda Ujerumani n TSU kwenye michuano ya Fallerhof.
    Bahati mbaya kwake, siyo tu Chelsea haijamruhusu Nditi, bali hata Mazembe, safari hii imegoma kumpandisha ndege Ulimwengu.
    Katika mchezo wa kwanza, vikosi vilikuwa; Ngorongoro; Barwany Khomein, Omega Seme, Jamal Mroki, Issa Rashid, Ruhana Samir, Yarouk Ramadhan, Kheri Salum/Jerome Lambele, Frank Damayo, Simon Msuva, Atupele Green na Ramadhan Singano.
    Flying Eagles; Samuel Okani, Hassan Abubakar, Ahiyu Mohamed, Ikechukwu Okine, Chizoba Amaefule, Agboyi Oubokha, Moses Orkuma, Chidi Osochukwu, Yahaya Adam/Harrison Egbune, Achaji Gero na Aminu Omar/Uche Agbo. Kila la heri Ngorongoro Heroes.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI NGORONGORO NIGERIA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top