• HABARI MPYA

    Thursday, September 11, 2014

    YANGA SC WAINGIA KAMBINI KATIKATI YA JIJI

    Na Nagma Khalid, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imeingia kambini Tansoma Hotel, eneo la Gerezani, Dar es Salaam jioni ya leo kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii, dhidi ya Azam FC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Jerry Tegete pekee ndiye hajaingia kambini kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya nyonga, lakini wengine wote wapo kambini hadi majeruhi Andrey Coutinho ambaye anaendelea na matibabu kuangalia uwezekano wa kucheza mechi hiyo. Hata hivyo, kuna uwezekano Tegete akaingia kambini baadaye.
    Kiungo huyo Mbrazil aliumia katika mchezo wa kirafiki asubuhi ya jana dhidi ya Polisi ya Dar es Salaam Uwanja wa sekondari Loyola, Mabibio, Dar es Salaam na leo amefanya mazoezi ya gym.
    Jerry Tegete pekee hajaingia kambini kwa sababu ya maumivu ya nyonga

    Coutinho alikuwa anajaribu kugeuka apige mpira, akateguka kifundo cha mguu na kushindwa kuendelea na mchezo uliomalizika kwa sare ya 0-0 jana.
    Yanga SC ndio washindi mara nyingi zaidi wa Ngao, mara ya kwanza wakitwaa mwaka 2001 walipoifunga mabao 2-1 Simba SC, enzi hizo Ligi Kuu inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager. 
    Baada ya hapo, haikuchezwa tena mechi ya Ngao hadi mwaka 2009 wakati Mtibwa Sugar ilipoilaza 1-0 Yanga SC.
    Mwaka 2010 Yanga walirejesha Ngao kwenye himaya yao, baada ya kuwachapa tena wapinzani wao wa jadi, Simba kwa penalti 3-1 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
    Simba SC walitwaa mara mbili mfululizo Ngao na kufikia rekodi ya watani, kwanza 2011 walipoifunga 2-0 Yanga na 2012 walipotoka nyuma kwa 2-0 na kuilaza Azam 3-2.
    Mwaka jana, Yanga SC ikaweka rekodi ya kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi Ngao ya Jamii, baada ya kuilaza 1-0 Azam FC, bao pekee la kiungo Salum Abdul Telela ‘Master’.
    Na mwaka huu, tena Azam FC na Yanga SC zinarudia mechi ya Ngao ya msimu uliopita, zitakapokutana tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAINGIA KAMBINI KATIKATI YA JIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top