• HABARI MPYA

    Saturday, September 06, 2014

    OKWI ALIVYOANZA KAZI SIMBA SC LEO KWA DUA NZITO KABLA YA KESI YAKE YA KUANZA KUUNGURUMA KESHO TFF

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI mtata, Emmanuel Arnold Okwi leo ameichezea tena kwa mara ya kwanza klabu yake ya zamani, Simba SC katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya.
    Okwi alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa 3-0 na dakika ya kwanza alifunga bao akiwa ameotea, refa akamshitukia na kulikataa.
    Okwi alipoingia uwanjani kabla ya kuvuka mstari wa kuingia eneo la kuchezea mpira, alisali kwa sekunde kadhaa na pasi nzuri ya kwanza alipewa yeye kwa bahati mbaya alikuwa tayari ameotea, akautupia mpira nyavuni na kukimbia kuanza kushangilia.
    Dua ya kurejea Msimbazi; Emmanuel Okwi akisali kabla ya kuingia uwanjani leo

    Ajabu hakuona wenzake kumfuata kushangilia naye, na alipogeuka akakutana na refa kanyoosha mkono wa kuashiria halikuwa bao. Akalalamika kidogo, akarejea mchezoni.
    Mwanzoni, mchezo ulikuwa mgumu kwake, aliharibu mipira kadhaa, alitoa pasi mbovu na kupiga mafyongo kutokana na kuzomewa na mashabiki wa Yanga SC.
    Bahati mbaya zaidi kwake Simba SC ilianza kupeleka mashambulizi eneo ambalo huketi mashabiki wa Yanga SC na kwa ujumla dakika 45 za kwanza zilikuwa nzito kwake uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ila kipindi cha pili baada ya kuhamia eneo ambalo hujazana manazi wa Simba SC, Okwi alianza kuona raha ya mchezo. 
    Kwa nini Yanga SC walikuwa wanamzomea Okwi?
    Baada ya kusali alibusu kwenye chaki, akaingia uwanjani
    Tabasamu la mawazo; Okwi akiingia uwanjani tayari kuanza tena kazi Simba SC kabla ya kesi yake kuanza kesho TFF

    Okwi alisajiliwa na Yanga SC Desemba mwaka jana kutoka SC Villa ya Uganda, ambako alikuwa anacheza kwa ruhusa maalum ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), baada ya kuingia kwenye mgogoro na klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia iliyomnunua kwa dola za Kimarekani 300,000 kutoka Simba SC Januari mwaka jana.
    Etoile haikilipa fedha hizo Simba SC hadi wakafunguliwa kesi ya madai FIFA inayoendelea hadi leo na Okwi naye wakashitakiana na klabu hiyo, mchezaji akidai kutolipwa mishahara ya miezi kadhaa na klabu ikimtuhumu kutoonekana kazini kwa muda fulani baada ya ruhusa fupi ya kurejea nyumbani kuchezea timu ya taifa.
    Ndipo Okwi akaomba, wakati kesi hiyo ikiendelea, aruhusiwe kucheza kwa muda klabu nyingine kulinda chake, akakubaliwa na akajiunga na SC Villa ambayo ndiyo iliyomuibua kabla ya kumuuza Simba SC mwaka 2009.
    Baada ya kutua Yanga SC, Okwi alipewa dola 60,000 kati ya dola 100,000 za makubaliano ya miaka miwili na nusu, huku sehemu iliyobaki akiahidiwa kupewa Januari mwaka huu.
    Lakini kufika Januari hakupewa fedha hizo na anadai aliendelea kuzungushwa hadi kufika Machi, akaamua kususa kushinikiza malipo yake.
    Amerudi na moto wake; Okwi kulia akimtoka beki wa Gor Mahia
    Okwi akiwania mpira wa juu dhidi ya kipa wa Gor Mahia
    Yanga watamkumbuka? Okwi akiingia kwenye eneo la penalti la Gor Mahia

    Julai, Yanga SC ikamshitaki mchezaji huyo TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ikiomba kuvunja naye mkataba na kurejeshewa fedha zake za usajili na mishahara aliyochukua kimakosa pamoja na kulipa fidia ya dola 200,000.
    Okwi baada ya kupatiwa barua za kuitwa na TFF kwenye kesi dhidi ya Yanga SC- akaamua kwenda kuomba kusajiliwa Simba SC wakati kesi yake ikiendelea, ili kulinda kipaji chake.
    Yanga SC ikaja juu na kusema huyo bado mchezaji wao halali na kwa kitendo cha kwenda Simba SC, itashitaki upya TFF, ikitaka mchezaji na klabu wafungiwe. Yanga pia imetaka Okwi alipe fidia ya dola 500,00 badala ya 200,000.
    Kesi ya Okwi na Yanga SC inaanza kusikilizwa kesho katika kikao cha Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji mjini Dar es Salaam.
    Kamati hiyo inaundwa na Mwenyekiti, Wakili Richard Sinamtwa, Makamu wake Wakili Moses Kaluwa na Wajumbe Zacharia Hans Poppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega.
    Okwi amecheza kwa dakika 77 leo kabla ya kumpisha Ibrahim Ajibu na alichangia mabao mawili, moja la Kiongera la kwanza na Ramadhani Singano ‘Messi’ lililokuwa la pili kwenye mchezo wa leo.
    Bao la kwanza, alimtoka beki wa Gor Mahia pembeni kushoto akatia krosi nzuri ikaunganishwa na Paul Kiongera na la pili aliuanganisha kwa shuti kali krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, kipa akatema Messi akamalizia.
    Nini mustakabali wa Okwi katika saka hili- akiwa tayari ameanza kuitumikia Simba SC? Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji itatoa majibu baada ya vikao vyake. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI ALIVYOANZA KAZI SIMBA SC LEO KWA DUA NZITO KABLA YA KESI YAKE YA KUANZA KUUNGURUMA KESHO TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top