• HABARI MPYA

    Tuesday, September 09, 2014

    JONAS MKUDE AANZA KUMNOLEA MAKALI KWIZERA, NI SHIDA VITA YA NAMBA VIUNGO SIMBA SC

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imepata kiungo mpya wa ulinzi ‘babu kubwa’ kutoka Burundi, Pierre Kwizera aliyekuwa anacheza Ivory Coast na tayari amekwishaziteka nyoyo za wana Msimbazi.
    Bahati nzuri kwake, Kwizera alifika Dar es Salaam, kipindi ambacho kiungo chaguo la kwanza wa ulinzi wa Simba SC, Jonas Mkude ni majeruhi, hivyo ikamuwia rahisi kwake kuchukua nafasi na kuonyesha uwezo wake.
    Sasa wana Simba SC wanaamini Kwizera ndiye anayefaa zaidi katika nafasi hiyo kwa kuwa wamesahau sahau kuhusu Mkude- lakini kiungo wa kimataifa wa Tanzania amepona maumivu ya goti na ameanza mazoezi rasmi.
    Mashine kazini; Kiungo Jonas Mkude akijifua katika gym tayari kurudi uwanjani kugombea namba na Pierre Kwizera

    Mkude aliumia akiichezea timu ya taifa, Taifa Stars katika mchezo wa kirafiki nchini Botswana mjini Gaborone Juni mwaka huu na baada ya vipimo na tiba, akatakiwa kupumzika kwa wiki sita.
    Na jana mchezaji huyo mahiri wa sehemu ya kiungo wa ulinzi, amejiunga na wachezaji wenzake wa Simba SC kambini Mbezi mjini Dar es Salaam kuanza rasmi kujifua kurudi katika kiwango chake, ili amshawishi kocha Mzambia, Patrick Phiri kumrejesha kwenye kikosi cha kwanza.
    Phiri amerejea Simba SC kipindi ambacho Mkude ni majeruhi, hivyo hajawahi kufanya naye kazi na tayari amemuamini kiungo mpya Mrundi, Kwizera katika nafasi ya kiungo mkabaji.
    Mwenye namba anarudi; Kwizera alichukua nafasi ya Jonas Mkude ambaye amepona, sasa ana kazi ya kutetea nafasi hiyo

    Tayari kiungo mwingine wa ulinzi, William Lucian ‘Gallas’ amejitoa kwenye kinyang’anyiro cha namba na kukubali kuwa chaguo la tatu, kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango cha kulinganisha na wawili hao.
    Vita ya namba kwa viungo Simba SC haishii dimba la chini tu, bali hata huko juu ni balaa. Katikati kuna Shaaban Kisiga ‘Malone’, Amri Kiemba, Said Ndemla na Abdallah Seseme.
    Pembeni kuna Twaha Shekuwe, Ramadhani Singano wote majina ya utani Messi, Uhuru Suleiman na Haroun Chanongo, ambao angalau wawili wanaweza kuanza na wengine wakatokea benchi.
    Vita hiyo inaendelea hadi kwenye safu ya ushambuliaji, ambako Paul Kiongera, Amisi Tambwe, Emannuel Okwi, Elias Maguri na Ibrahim Ajibu wanachuana vikali, ambao kati yao wawili tu wanatakiwa kuanza.
    Mkude anaweza kukosa mechi za mwanzo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, Simba SC ikifungua dimba na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Septemba 21.
    Mabingwa watetezi, Azam FC wataanza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
    Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20.
    Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JONAS MKUDE AANZA KUMNOLEA MAKALI KWIZERA, NI SHIDA VITA YA NAMBA VIUNGO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top