Kazimoto mazoezini leo |
KIUNGO wa timu
ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mwinyi Kazimoto amepona na leo amefanya
mazoezi na wenzake Kim, Uwanja wa Chuo Kikuu cha Kyambogo mjini hapa tayari
kucheza mechi ya Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge dhidi ya Rwanda kesho.
Kocha Mkuu
wa Stars, Mdenmark, Kim Poulsen amefurahia kupona kwa kiungo huyo wa Simba SC
na anaamini itakuwa moja ya silaha zake katika mchezo wa kesho dhidi ya Rwanda
Uwanja wa Lugogo, ambao utaanza saa 8:00 mchana.
Kazimoto aliumia
katika mechi dhidi ya Burundi na akakosa mechi ya mwisho ya Kundi B dhidi ya Somalia
jana, lakini kesho atakuwa kazini tena.
“Rwanda ina timu nzuri na tunaiheshimu sana
lakini tuko tayari kupambana nao katika mechi ya kesho na ninaamini vijana
wataendelea kufunga mabao kama ilivyofanyika katika mechi dhidi ya Somalia,”
alisema.
Kocha huyo
alisema wachezaji wote wako katika hali nzuri na wana ari ya kushinda mechi hii
ili watinge katika hatua ya nusu fainali.
“Vijana wana
morali na wamejiandaa vizuri na mechi hii ya kesho na tuna imani watatupa raha
tena kama Jumamosi.
Katika hatua
nyingine, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kaishe ambaye Bia
ya kampuni yake inaidhamini Kilimanjaro
Stars, alitoa pongezi kwa Stars kwa kutinga hatua ya robo fainali.
“Tumekuwa
tukifuatilia mashindano haya kwa njia ya runinga na kwa kweli yameleta hamasa
kubwa sana hasa mchezo wa Jumamosi tulipoifunga Somaliake kwa vya 7-0,” alisema
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Kavishe
alisema Stars ina uwezo mkubwa wa kutinga fainali na kurejea nyumbani na kombe
hili la Cecafa.
“Watanzania wote lazima wawe na imani na
waiombee dua njema timu yetu ili ishinde…sisi tukiwa wadhamini tutaendelea
kuipa nguvu timu wao watuletee kombe tu,” alisema.