Miyeyusho kulia akimuadhibu Nassib jana |
Na Mahmoud Zubeiry
Mbwana |
BINGWA wa
zamani wa dunia wa WBU, Mbwana Matumla ‘Golden Boy’, amesema ana wasiwasi
Francis Miyeyusho na Francis Cheka wanatumia daw za kuongeza nguvu, zinazopigwa
marufuku michezoni.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana, Golden Boy alisema kwamba umefika wakati Tanzania kuwe na
utaratibu wa kuwapima mabondia kabla na baada ya michezo, kwani inawezekana
kutokuwa na utaratibu huo kukatoa mwanya kwa mabondia wengine kutumia dawa
hizo.
“Mimi
nilipigana na Francis, kweli alinipiga, ila nilipata wasiwasi sana juu ya nguzu
zake, kwa kweli hazikuwa za kawaida, sisemi kwamba anatumia, inawezekana ni
uwezo wake, lakini nasema nina wasiwasi, yeye na Francis Cheka wanatumia hizo
dawa,”alisema Mbwana.
Golden Boy
alipigwa na Miyeyusho Oktoba 30, mwaka jana ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam,
kwa pointi, jaji Omari Yazidu akitoa 113-114, Said Chaku 110-117 na Jalus
Lugongo 109-118.
Katika
pambano hilo, Francis Miyeyusho alienda chini raundi ya pili, wakati Mbwana
Matumla alidondoka raundi ya pili na ya nane na hilo ndilo lilikuwa pambano la
mwisho la Golden Boy hadi sasa.
Miyeyusho
‘Chichi Mawe’ jana aliendeleza ubabe wake , baada ya kufanikiwa kutetea taji lake
la WBF uzito wa Bantam, kwa kumpiga Nassib Ramadhan kwa Techinical Knockout
(TKO) raundi ya 10 kwenye ukumbi wa PTA, Saba Saba, Temeke mjini Dar es Salaam
usiku huu.
Nassib
alionekana kuishiwa pumzi tangu raundi ya nane, lakini alijikongoja kutaka
kumaliza raundi 12 za pambano hilo, ila kwa bahati mbaya, safari ikaishia
raundi ya 10.
Hata hivyo,
Nassib bondia kutoka Mabibo, Dar es Salaam, alilianza vizuri pambano hilo
akimsukumia mpinzani wake makonde mazito yaliyoonekana kumyumbisha.
Naasib
aliendelea kutawala pambano hadi raundi ya sita, ila baada ya hapo, mwelekeo wa
pambano ulianza kubadilika taratibu, Chichi, Mtoto wa Kinondoni akianza
kumuadhibu mpinzani wake kwa makonde yake yaliyoshiba uzito.
Nassib
alijitahidi mara moja moja kujibu, lakini zaidi alitumia ujanja wa kumkumbatia
Chichi ili kumpunguza kasi.
Hata hivyo,
Nassib hakushindwa kwa kupigwa ngumi, bali aliishiwa pumzi jambo ambalo
linaashiria kijana huyo ni bondia imara na anaweza kuwa mpinzani wa kweli wa
Chichi Mawe.
Kwa ujumla
lilikuwa pambano zuri ambalo kwa muda mrefu halijapatikana katika ardhi ya
Tanzania- mabondia walikuwa wakipigana, hakukuwa na ujanja ujanja. Wote ni
mafundi na mamia waliohudhuria pambano hilo, waliburudika kwa mchezo mzuri.
Katika
mapambano ya awali, Deo Samuel alitoka sare na Freddy Sayuni, Mohamed Matumla
alimpiga kwa Knockout (KO) raundi ya pili Deo Miyeyusho, Fadhil Majiha alimpiga
kwa pointi Juma Fundi na Ibrahim Classic alimpiga kwa pointi Said Mbugi.
Mgeni rasmi,
Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alimvalisha mkanda
wa ubingwa Miyeyusho baada ya pambano hilo, lililohudhuriwa pia na Makamu
Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.