Mrisho Ngassa |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MRISHO
Khalfan Ngassa amesema kama Simba wanampenda sana, wapande dau walilotoa El
Merreikh ili aghairi kwenda Sudan.
Akizungumza
hapa, Ngassa alisema kwamba yeye kama mchezaji anaangalia maslahi na kwa
mshahara mzuri pamoja na dau nono la usajili alilopewa Matajiri wa Sudan
amelainika na kukubali kujiunga nayo.
Wakati Azam
FC imemuuza Ngassa kwa dola za Kimarekani 75,000 kwenda El Merreikh ambako
amesaini mkataba wa miaka miwili, kiungo huyo mshambuliaji amepewa dau la
kusaini mkataba wa miaka miwili, dola 50,000 na atakuwa analipwa mshahara wa
dola 4,000 kwa mwezi.
Awali,
Merreikh walitaka kumpa mkataba wa miaka mitatu Ngassa wenye thamani ya dola
100,000, lakini wakala wake Alhaj Yussuf Said Bakhresa akakataa akisema
utambana mchezaji wake aking’ara na kutakiwa na klabu nyingine.
Sasa Ngassa
baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge
mwishoni mwa wiki hii, atakwenda Sudan kufanyiwa vipimo tayari kujiunga na
klabu hiyo, ambayo ni jambo la kawaida kucheza hatua ya makundi ya michuano ya
klabu Afrika.
Azam FC
imesema imeweka mbele maslahi ya mchezaji na taifa kwa ujumla katika maamuzi ya
kumuuza Sudan, kutoka Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo. “Hii timu (Merreikh)
kila mwaka inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, maana yake
huyu mchezaji atakwenda kupata maendeleo na kuja kuisaidia zaidi Tanzania
katika mashindano ya kimataifa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam.
Alipoulizwa
kuhusu Simba SC aliyokuwa anaichezea klabu hiyo, kiongozi huyo alisema wao
walimtoa kwa mkopo Ngassa kwenda kwa Wekundu wa Msimbazi hadi Mei 31, mwakani
na mkataba wao ndio unasema hivyo.
“Sisi
tuliwapa Simba huyu mchezaji kwa mkopo hadi Mei 31 na wakatupa Sh. Milioni 25,
ila tuko tayari kuwarudishia fedha zao walizota, lakini huyu mchezaji ni mali
yetu na hata TFF wa natambua hilo, na
tumekwishamuuza Merreikh,”alisema.
Alipoulizwa
kuhusu Simba kusaini mkataba mpya na Ngassa, alisema; “We uliona wapi dunia
nzima timu inapewa mchezaji kwa mkopo halafu inamsainisha mkataba? Simba lazima
ifike wakati waache kurudia makosa, haya ndio mambo ya Mbuyu Twite
sasa,”alisema kiongozi huyo wa Azam.
Azam
walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na
kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika
Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi
ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifanya
hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam
kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara
nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
Ilielezwa
kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa
baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji
huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni
30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
Ngassa
anang’ara katika Challenge ya mwaka huu mjini hapa, hadi sasa akiwa amefunga
mabao matano sawa na John Bocco wa Azam na wafungana kileleni.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE
2012
John Bocco Tanzania 5
Mrisho
Ngassa Tanzania 5
Brian Umony Uganda 3
Suleiman
Ndikumana Burundi 3 (1 penalti)
Chris
Nduwarugira Burundi 3
Geoffrey
Kizito Uganda 2
Robert
Ssentongo Uganda 2
Khamis Mcha Zanzibar 2
David
Ochieng Kenya 2
Clifton
Miheso Kenya 2
Dadi Birori Rwanda 2