Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
MWENYEKITI
wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe anatarajiwa kutua mjini
hapa kesho, kwa ajili ya mambo mawili makubwa, usajili wa wachezaji na kocha
mpya, atakayerithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY jana kwa simu kutoka Dar es Salaam, Kapteni huyo wa zamani wa
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) anakuja Kampala kufanya kazi za Simba SC.
Ingawa Hans
Poppe hakutaka kuzugumzia kwa undani ujio wake hapa, lakini BIN
ZUBEIRY inatambua anakuja kufanya mazungumzo na kocha Mmalawi, Kinnah
Phiri na wachezaji kadhaa waliowavutia katika mashindano haya, akiwemo
mshambuliaji Mganda Brian Umony.
Lakini pia,
Hans Poppe anakuja kumalizana na mshambuliaji wao Mganda, Emmnanuel Okwi ambaye
amemaliza mkataba wake.
Vyombo vya
habari Dar es Salaam vimeripoti kuwa, Okwi atasaini mkataba wa mwaka mmoja
zaidi Simba SC kwa dau la dola za Kimarekani 40,000 pamoja na nyongeza ya
mshahara.
Okwi amekuwa
akihusishwa na habari za kuhamia Yanga na Azam FC baada ya kumaliza mkataba
wake Simba SC, lakini wakati huo huo inaelezwa amekwishafikia makubaliano na
Wekundu wa Msimbazi kuongeza mkataba.