• HABARI MPYA

    Wednesday, September 17, 2014

    NATAMANI KUMUONA ZAIDI JAJA AKIIONGOZA SAFU YA USHAMBULIAJI YANGA SC

    KWA mara ya kwanza namuona Genilson Santana Santos ‘Jaja’ anatuliza mpira na kuumiliki vizuri bila wasiwasi mbele ya wachezaji wa timu pinzani, kisha anatoa pasi nzuri na kuhama upande kwa kasi kidogo.
    Hiyo ilikuwa ni Jumapili ya Septemba 14, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wake wa tano kati ya minne niliyomshuhudia awali.
    Niliona mchezaji tofauti na yule niliyemuona katika muda wote wa awali kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC siku hiyo, kiasi cha mashabiki wa Yanga SC kuanza kumzomea kipindi cha kwanza wakitaka atolewe.
    Niliona mchezaji ambaye amechangamka, akili imerudi uwanjani, amepata hali ya kujiamini, ameacha mchecheto na kutulia kucheza kwa utashi wake bila shinikizo lolote.

    Hiyo ilifuatia kufunga mabao mawili katika mchezo huo mgumu, ambao Yanga SC haikupewa kabisa nafasi ya kushida.
    Mara moja nikakumbuka alichokisema kocha Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo kabla ya mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Nilimsikia Maximo anamuhamasisha Jaja wakati timu zinaingia uwanjani kuanza mchezo; “Go, goo, top scoorer,”. Nilimtazama Maximo na kukutana na sura iliyokuwa inamaanisha anamaanisha anachokizungumza, nilitamani kuona Jaja atafanya nini uwanjani.
    Sikuona mchezaji wa kunivutia, mzito na anayeogopa hata mipira, asiye na kasi na asiyeweza hata kurukia mipira ya juu yake kidogo, zaidi anaelekeza sana apelekewe mipira alipo kila inapompita.
    Nilipomuona tena katika mchezo na Thika United ya Kenya akifunga bao pekee la ushindi kama lile la awali kwa mpira wa kutokea pembeni, kidogo nikaanza kujenga imani naye.
    Na nikaandika, kuwaambia wana Yanga SC wamvutie subira mchezaji huyo.
    Bao la kwanza dhidi ya Azam FC alifunga kwa staili yake ile ya kumalizia mipira ya kutokea pembeni, lakini bao la pili lilikuwa tofauti.
    Alipewa pasi na Mrisho Ngassa, akaimiliki vizuri, akavuta kidogo na bahati nzuri kwake, kipa Mwadini Ali akatoka kidogo langoni, wakati wengi wakitarajia Jaja angefumua shuti, lakini alipiga ile tunaita kitaalamu akiupitisha mpira juu ya kipa ‘kipimo’.
    Amefunga mabao manne katika mechi tano, na yote ni tofauti. Katika mechi na Chipukizi Uwanja wa Gombani, Pemba inaelezwa alifunga kwa kichwa akimalizia kona ya Haruna Niyonzima.
    Katika mechi na Thika, alikwenda mzima mzima kuiunganshia pasi ya Simon Msuva kutokea pembeni kulia.
    Bao la kwanza mechi na Azam FC aliunganisha mpira uliombabatiza beki Aggrey Morris, wakati bao la pili siku hiyo, alifunga kitaalamu, akimpima Mwadini Ali ‘kanzu’.
    Imekuwaje Jaja aliwafunga Azam FC mabao mawili? Hilo ni swali ambalo bila shaka wengi walijiuliza zaidi yangu. Kitu kimoja ambacho kwa haraka kilinijia ni labda, baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza Jaja kutokuwa sumu kiasi cha mashabiki wa timu yake mwenyewe kuanza kumzomea, wachezaji wa Azam FC nao walimdharau na hawakuona umuhimu wa kumchunga, ndiyo maana akapata nafasi ya kufunga kiulaini.
    Lakini pia nikakumbuka Maximo alisema Jaja ni kama Toni Kroos wa  Bayern Munich wa Ujerumani, hajui kupiga chenga anajua kufunga tu. Nikakumbuka Maximo alikuwa tayari kuondoka Yanga SC iwapo Jaja angeachwa katika usajili baada ya viongozi wa klabu hiyo kutilia shaka uwezo wake.            
    Maximo amekuwa mwenye kujiamini mno juu ya mchezaji huyo tangu mwanzoni kabisa- na akiwa mtu mwenye dhamana ya matokeo Yanga SC kama kocha Mkuu, bila shaka hatahitaji wachezaji wa kutia mchanga kitumbua chake.
    Maximo amefanya kazi Tanzania kwa miaka minne tangu 2006 hadi 2010 akiwa kocha wa Taifa Stars, anaijua sika ya nchi hii vizuri- bila shaka imani yake kwa Jaja ina siri nzito nyuma yake.
    Baada ya Jaja kufunga mabao mawili dhidi ya Azam FC, sasa mabeki wa timu za Ligi Kuu hawatamdharau tena Mbrazil huyo, na atarajie kuwekewa ulinzi mkali katika mechi zijazo.
    Na hiyo ndiyo kiu yangu- nataka kumuona Jaja akicheza huku analindwa vikali na mabeki. Nataka kumuona Jaja akicheza mechi ngumu dhidi ya mabeki ‘wandava’ wale ‘wapiga kiatu’ kama Juma Nyosso anakuwaje.
    Nataka kumuona Jaja akicheza michuano ya Afrika dhidi ya mabeki wazuri wa Kaskaini, Kusini, Magharibi mwa Afrika na hata ukanda wetu huu. Kwa ufupi, nina kiu ya kumuona zaidi Jaja akiiongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga SC ili kuujua uwezo wake zaidi. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NATAMANI KUMUONA ZAIDI JAJA AKIIONGOZA SAFU YA USHAMBULIAJI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top